Maonyo Kwamba Utumwa ni Hakika (continued)

Unabii mbalimbali na miito kwa Wayahudi, ikitangaza kwamba utumwa wao na uharibifu wa Yerusalemu ni hakika.

609 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yeremia 18–19

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana: 2 “Shuka uende mpaka nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu.” 3 Kwa hiyo nikashuka mpaka kwenye nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake. 4 Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake, hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kama vile ilivyoonekana vyema kwake yeye.

5 Kisha neno la Bwana likanijia kusema: 6 “Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?” asema Bwana. “Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, ee nyumba ya Israeli. 7 Ikiwa wakati wowote nikitangaza kuwa taifa au ufalme utangʼolewa, utaangushwa na kuangamizwa, 8 ikiwa lile taifa nililolionya litatubia uovu wake, ndipo nitakapokuwa na huruma, wala sitawapiga kwa maafa niliyokuwa nimewakusudia. 9 Ikiwa wakati mwingine nitatangaza kuwa taifa ama utawala ujengwe na kuwekwa wakfu, 10 ikiwa utafanya maovu mbele zangu na hukunitii, ndipo nitakapoghairi makusudio yangu mema niliyokuwa nimeyakusudia.

11 “Basi kwa hiyo waambie watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Tazama! Ninaandaa maafa kwa ajili yenu, nami ninabuni mabaya dhidi yenu. Kwa hiyo geukeni kutoka njia zenu mbaya, kila mmoja wenu, tengenezeni njia zenu na matendo yenu.’ 12 Lakini wao watajibu, ‘Hakuna faida. Tutaendelea na mipango yetu wenyewe, kila mmoja wetu atafuata ukaidi wa moyo wake mbaya.’ ”

13 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana:

“Ulizia miongoni mwa mataifa:

Ni nani alishasikia jambo kama hili?

Jambo la kutisha sana limefanywa

na Bikira Israeli.

14 Je, barafu ya Lebanoni iliwahi kutoweka

kwenye miteremko yake ya mawe wakati wowote?

Je, maji yake baridi yatokayo katika vyanzo vilivyo mbali

yaliwahi kukoma kutiririka wakati wowote?

15 Lakini watu wangu wamenisahau mimi,

wanafukizia uvumba sanamu zisizofaa kitu,

zilizowafanya wajikwae katika njia zao

na katika mapito ya zamani.

Zimewafanya wapite kwenye vichochoro

na kwenye barabara ambazo hazikujengwa.

16 Nchi yao itaharibiwa,

itakuwa kitu cha kudharauliwa daima;

wote wapitao karibu nayo watashangaa

na kutikisa vichwa vyao.

17 Kama upepo utokao mashariki,

nitawatawanya mbele ya adui zao;

nitawapa kisogo wala sio uso,

katika siku ya maafa yao.”

18 Wakasema, “Njooni, tutunge hila dhidi ya Yeremia; kwa kuwa kufundisha sheria kwa kuhani hakutapotea, wala shauri litokalo kwa mwenye hekima, wala neno la manabii. Hivyo njooni, tumshambulie kwa ndimi zetu na tusijali chochote asemacho.”

19 Nisikilize, Ee Bwana,

sikia wanayosema washtaki wangu!

20 Je, mema yalipwe kwa mabaya?

Lakini wao wamenichimbia shimo.

Kumbuka kwamba nilisimama mbele yako

na kunena mema kwa ajili yao,

ili wewe ugeuze hasira yako kali mbali nao.

21 Kwa hiyo uwaache watoto wao waone njaa;

uwaache wauawe kwa makali ya upanga.

Wake zao wasiwe na watoto, na wawe wajane;

waume wao wauawe,

nao vijana wao waume

wachinjwe kwa upanga vitani.

22 Kilio na kisikike kutoka kwenye nyumba zao

ghafula uwaletapo adui dhidi yao,

kwa kuwa wamechimba shimo ili kunikamata

na wameitegea miguu yangu mitego.

23 Lakini unajua, Ee Bwana,

hila zao zote za kuniua.

Usiyasamehe makosa yao

wala usifute dhambi zao

mbele za macho yako.

Wao na waangamizwe mbele zako;

uwashughulikie wakati wa hasira yako.

19:1 Hili ndilo asemalo Bwana: “Nenda ukanunue gudulia la udongo kutoka kwa mfinyanzi. Wachukue baadhi ya wazee wa watu na wa makuhani 2 na mtoke mwende mpaka kwenye Bonde la Ben-Hinomu, karibu na ingilio la Lango la Vigae. Huko tangaza maneno ninayokuambia, 3 nawe useme, ‘Sikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda na watu wa Yerusalemu. Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Sikilizeni! Nitaleta maafa mahali hapa, ambayo yatafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yawashe. 4 Kwa kuwa wameniacha na kupafanya mahali hapa kuwa pa miungu ya kigeni. Wameiteketezea sadaka miungu ambayo wao wala baba zao wala wafalme wa Yuda kamwe hawakuijua, nao wamelijaza eneo hili kwa damu isiyo na hatia. 5 Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia miungu pa Baali ili kuteketeza wana wao katika moto kama sadaka kwa Baali, kitu ambacho sikukiamuru wala kukitaja, wala hakikuingia akilini mwangu. 6 Hivyo jihadharini, siku zinakuja, asema Bwana, wakati watu hawatapaita tena mahali hapa Tofethi ama Bonde la Ben-Hinomu, bali Bonde la Machinjo.

7 “ ‘Nitaiharibu mipango ya Yuda na Yerusalemu mahali hapa. Nitawafanya waanguke kwa upanga mbele ya adui zao, katika mikono ya wale watafutao uhai wao, nami nitaitoa mizoga yao kuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi. 8 Nitauharibu mji huu na kuufanya kitu cha kudharauliwa. Wote wapitao karibu watashangaa na kuudhihaki kwa sababu ya majeraha yake yote. 9 Nitawafanya wao kula nyama ya wana wao na binti zao; kila mmoja atakula nyama ya mwenzake wakati wa dhiki ya kuzungukwa na jeshi lililowekwa juu yao na adui wanaotafuta uhai wao.’

10 “Kisha livunje lile gudulia wale walio pamoja nawe wakiwa wanaangalia, 11 uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: Nitalivunja taifa hili na mji huu kama gudulia hili la mfinyanzi lilivyovunjwa, nalo haliwezi kutengenezeka tena. Watawazika waliokufa huko Tofethi hata isiwepo nafasi zaidi. 12 Hivi ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na kwa wale waishio ndani yake, asema Bwana. Nitaufanya mji huu kama Tofethi. 13 Nyumba zilizoko Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, Tofethi: yaani nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani, na kumimina dhabihu za vinywaji kwa miungu mingine.’ ”

14 Kisha Yeremia akarudi kutoka Tofethi, mahali ambapo Bwana alikuwa amemtuma kutoa unabii, akasimama katika ua wa Hekalu la Bwana na kuwaambia watu wote, 15 “Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya mji huu pamoja na vijiji vinavyouzunguka kila maafa niliyosema dhidi yake, kwa sababu wamekuwa na shingo ngumu, na hawakuyasikiliza maneno yangu.’ ”