Hatima ya Pashuri Yatabiriwa

609 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yeremia 20

1 Ikawa kuhani Pashuri mwana wa Imeri, mkuu wa maafisa wa Hekalu la Bwana, alipomsikia Yeremia akitoa unabii juu ya mambo haya, 2 akaamuru Yeremia nabii apigwe na kufungwa kwenye mkatale katika Lango la Juu la Benyamini huko Hekaluni la Bwana. 3 Siku ya pili Pashuri alipomwachia kutoka kwenye mkatale, Yeremia akamwambia, “Bwana hakukuita jina lako kuwa Pashuri bali Magor-Misabibu. 4 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: ‘Nitakufanya kuwa hofu kuu kwako wewe mwenyewe na rafiki zako wote, na kwa macho yako mwenyewe utawaona wakianguka kwa upanga wa adui zao. Nitawatia Yuda wote mikononi mwa mfalme wa Babeli, ambaye atawachukua na kuwapeleka Babeli, ama awaue kwa upanga. 5 Nitatia utajiri wote wa mji huu kwa adui zao: yaani mazao yao yote, vitu vyao vyote vya thamani, na hazina zote za wafalme wa Yuda. Watavitwaa kwa nyara na kuvipeleka Babeli. 6 Nawe Pashuri pamoja na wote waishio katika nyumba yako mtakwenda uhamishoni Babeli. Mtafia humo na kuzikwa, wewe na rafiki zako wote ambao umewatabiria uongo.’ ”

7 Ee Bwana, umenidanganya,

nami nikadanganyika;

wewe una nguvu kuniliko,

nawe umenishinda.

Ninadharauliwa mchana kutwa,

kila mmoja ananidhihaki.

8 Kila ninenapo, ninapiga kelele

nikitangaza ukatili na uharibifu.

Kwa hiyo neno la Bwana limeniletea matukano

na mashutumu mchana kutwa.

9 Lakini kama nikisema, “Sitamtaja

wala kusema tena kwa jina lake,”

neno lake linawaka ndani ya moyo wangu kama moto,

moto uliofungwa ndani ya mifupa yangu.

Nimechoka sana kwa kulizuia ndani mwangu;

kweli, siwezi kujizuia.

10 Ninasikia minongʼono mingi,

“Hofu iko pande zote!

Mshtakini! Twendeni tumshtaki!”

Rafiki zangu wote wananisubiri niteleze,

wakisema,

“Labda atadanganyika;

kisha tutamshinda

na kulipiza kisasi juu yake.”

11 Lakini Bwana yu pamoja nami

kama shujaa mwenye nguvu;

hivyo washtaki wangu watajikwaa

na kamwe hawatashinda.

Watashindwa, nao wataaibika kabisa;

kukosa adabu kwao hakutasahauliwa.

12 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,

wewe umjaribuye mwenye haki

na kupima moyo na nia,

hebu nione ukilipiza kisasi juu yao,

kwa maana kwako

nimeliweka shauri langu.

13 Mwimbieni Bwana!

Mpeni Bwana sifa!

Yeye huokoa uhai wa mhitaji

kutoka mikononi mwa waovu.

14 Ilaaniwe siku niliyozaliwa!

Nayo isibarikiwe ile siku

mama yangu aliyonizaa!

15 Alaaniwe mtu yule aliyemletea baba yangu habari,

yule aliyemfanya afurahi sana, akisema,

“Mtoto amezaliwa kwako,

tena mtoto wa kiume!”

16 Mtu huyo na awe kama miji ile

ambayo Bwana Mungu

aliiangamiza bila huruma.

Yeye na asikie maombolezo asubuhi

na kilio cha vita adhuhuri.

17 Kwa sababu hakuniua nikiwa tumboni,

hivyo mama yangu angekuwa kaburi langu,

nalo tumbo lake la uzazi

lingebaki kuwa kubwa daima.

18 Kwa nini basi nilitoka tumboni

ili kuona taabu na huzuni,

na kuzimaliza siku zangu katika aibu?

Hatima ya Shalumu na Yehoyakimu Yatabiriwa

Yeremia 22:1–23

1 Hili ndilo asemalo Bwana: “Shuka kwenye jumba la kifalme la mfalme wa Yuda, utangaze ujumbe huu huko: 2 ‘Sikia neno la Bwana, ee mfalme wa Yuda, wewe uketiye kwenye kiti cha enzi cha Daudi: wewe, maafisa wako na watu wako mnaopitia malango haya. 3 Hili ndilo Bwana asemalo: Tenda haki na adili. Mwokoe mkononi mwa mdhalimu yeye aliyetekwa nyara. Usimtendee mabaya wala ukatili mgeni, yatima au mjane, wala usimwage damu isiyo na hatia mahali hapa. 4 Kwa kuwa ukiwa mwangalifu kushika maagizo haya, ndipo wafalme watakaokalia kiti cha enzi cha Daudi watakapoingia kupitia malango ya jumba hili la kifalme, wakiwa wamepanda magari na farasi, huku wakifuatana na maafisa wao na watu wao. 5 Lakini kama hutayatii maagizo haya, asema Bwana, ninaapa kwa nafsi yangu kwamba jumba hili litakuwa gofu.’ ”

6 Kwa kuwa hili ndilo Bwana asemalo kuhusu jumba la kifalme la mfalme wa Yuda:

“Ingawa uko kama Gileadi kwangu,

kama kilele cha Lebanoni,

hakika nitakufanya uwe kama jangwa,

kama miji ambayo haijakaliwa na watu.

7 Nitawatuma waharabu dhidi yako,

kila mtu akiwa na silaha zake,

nao watazikata boriti zako nzuri za mierezi

na kuzitupa motoni.

8 “Watu kutoka mataifa mengi watapitia karibu na mji huu na kuulizana, ‘Kwa nini Bwana amefanya jambo la namna hii juu ya mji huu mkubwa?’ 9 Nalo jibu litakuwa: ‘Kwa sababu wameliacha agano la Bwana, Mungu wao, na wameabudu na kuitumikia miungu mingine.’ ”

10 Usimlilie yeye aliyekufa, wala usimwombolezee;

badala yake, afadhali umlilie kwa uchungu

yule aliyepelekwa uhamishoni,

kwa sababu kamwe hatairudia

wala kuiona tena nchi yake alikozaliwa.

11 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana kuhusu Shalumu mwana wa Yosia, aliyeingia mahali pa baba yake kuwa mfalme wa Yuda, lakini ameondoka mahali hapa: “Yeye kamwe hatarudi tena. 12 Atafia huko mahali walipompeleka kuwa mateka; hataiona tena nchi hii.”

13 “Ole wake yeye ajengaye jumba lake la kifalme kwa njia ya dhuluma,

vyumba vyake vya juu kwa udhalimu,

akiwatumikisha watu wa nchi yake pasipo malipo,

bila kuwalipa kwa utumishi wao.

14 Asema, ‘Nitajijengea jumba kuu la kifalme,

na vyumba vya juu vyenye nafasi kubwa.’

Hivyo anaweka ndani yake madirisha makubwa,

huweka kuta za mbao za mierezi,

na kuipamba kwa rangi nyekundu.

15 “Je, inakufanya kuwa mfalme

huko kuongeza idadi ya mierezi?

Je, baba yako hakuwa na chakula na kinywaji?

Alifanya yaliyo sawa na haki,

hivyo yeye akafanikiwa katika yote.

16 Aliwatetea maskini na wahitaji,

hivyo yeye akafanikiwa katika yote.

Je, hiyo si ndiyo maana ya kunijua mimi?”

asema Bwana.

17 “Lakini macho yako na moyo wako vimeelekezwa tu

katika mapato ya udhalimu,

kwa kumwaga damu isiyo na hatia,

kwa uonevu na ukatili.”

18 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda:

“Hawatamwombolezea wakisema:

‘Ole, ndugu yangu! Ole, umbu langu!’

Hawatamwombolezea wakisema:

‘Ole, bwana wangu! Ole, fahari yake!’

19 Atazikwa maziko ya punda:

ataburutwa na kutupwa

nje ya malango ya Yerusalemu.”

20 “Panda Lebanoni ukapige kelele,

sauti yako na isikike huko Bashani,

piga kelele toka Abarimu,

kwa kuwa wote waliojiunga nawe wameangamizwa.

21 Nilikuonya wakati ulipojisikia kwamba uko salama,

lakini ulisema, ‘Mimi sitasikiliza!’

Hii imekuwa kawaida yako tangu ujana wako;

hujanitii mimi.

22 Upepo utawaondoa wachungaji wako wote,

na wale ulioungana nao wataenda uhamishoni.

Kisha utaaibika na kufedheheka

kwa sababu ya uovu wako wote.

23 Wewe uishiye Lebanoni,

wewe uliyetulia kwenye majengo ya mierezi,

tazama jinsi utakavyoomboleza

maumivu makali yatakapokupata,

maumivu kama yale ya mwanamke

mwenye utungu wa kuzaa!