Maonyo Kwamba Utumwa ni Hakika (continued)
Unabii mbalimbali na miito kwa Wayahudi, ikitangaza kwamba utumwa wao na uharibifu wa Yerusalemu ni hakika.
609 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Kisha neno la Bwana likanijia: 2 “Kamwe usioe na kuwa na wana wala binti mahali hapa.” 3 Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana kuhusu wana na binti wazaliwao katika nchi hii, na kuhusu wale wanawake ambao ni mama zao, na wale wanaume ambao ni baba zao: 4 “Watakufa kwa magonjwa ya kufisha. Hawataombolezewa wala kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyosambaa juu ya ardhi. Watakufa kwa upanga na kwa njaa, nazo maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi.”
5 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Usiingie katika nyumba ambayo kuna chakula cha matanga, usiende kuwaombolezea wala kuwahurumia, kwa sababu nimeziondoa baraka zangu, upendo wangu na huruma zangu kutoka kwa watu hawa,” asema Bwana. 6 “Wakubwa na wadogo watakufa katika nchi hii. Hawatazikwa wala kuombolezewa, na hakuna atakayejikatakata au kunyoa nywele za kichwa chake kwa ajili yao. 7 Hakuna yeyote atakayewapa chakula ili kuwafariji wale waombolezao kwa ajili ya wale waliokufa, hata akiwa amefiwa na baba au mama, wala hakuna yeyote atakayewapa kinywaji ili kuwafariji.
8 “Usiingie katika nyumba ambayo kuna karamu, na kuketi humo ili kula na kunywa. 9 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli: ‘Mbele ya macho yako na katika siku zako, nitakomesha sauti zote za shangwe na za furaha, na pia sauti za bibi arusi na bwana arusi mahali hapa.’
10 “Utakapowaambia watu hawa mambo haya yote na wakakuuliza, ‘Kwa nini Bwana ameamuru maafa makubwa kama haya dhidi yetu? Tumefanya kosa gani? Tumetenda dhambi gani dhidi ya Bwana, Mungu wetu?’ 11 Basi waambie, ‘Ni kwa sababu baba zenu waliniacha mimi, wakafuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu. Waliniacha mimi na hawakuishika sheria yangu,’ asema Bwana. 12 ‘Lakini ninyi mmetenda uovu zaidi kuliko baba zenu. Tazama jinsi ambavyo kila mmoja wenu anafuata ukaidi wa moyo wake mbaya, badala ya kunitii mimi. 13 Kwa hiyo nitawaondoa katika nchi hii na kuwatupa katika nchi ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua, nako huko mtaitumikia miungu mingine usiku na mchana, kwa maana sitawapa fadhili zangu huko.’
14 “Hata hivyo, siku zinakuja,” asema Bwana, “wakati ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’ 15 bali watasema, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewatoa wana wa Israeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia.’ Maana nitawarudisha katika nchi niliyowapa baba zao.
16 “Lakini sasa nitawaagiza wavuvi wengi,” asema Bwana, “nao watawavua. Baada ya hilo, nitawaagizia wawindaji wengi, nao watawawinda kwenye kila mlima na kilima, na katika nyufa za miamba. 17 Macho yangu yanaziona njia zao zote, hazikufichika kwangu, wala dhambi yao haikusitirika. 18 Nitawalipiza maradufu kwa ajili ya uovu wao na dhambi yao, kwa sababu wameinajisi nchi yangu kwa maumbo yasiyo na uhai ya vinyago vyao vibaya, na kuujaza urithi wangu na sanamu za kuchukiza.”
19 Ee Bwana, nguvu zangu na ngome yangu,
kimbilio langu wakati wa taabu,
kwako mataifa yatakujia
kutoka miisho ya dunia na kusema,
“Baba zetu hawakuwa na chochote zaidi ya miungu ya uongo,
sanamu zisizofaa kitu
ambazo hazikuwafaidia lolote.
20 Je, watu hujitengenezea miungu yao wenyewe?
Naam, lakini hao si miungu!”
21 “Kwa hiyo nitawafundisha:
wakati huu nitawafundisha
nguvu zangu na uwezo wangu.
Ndipo watakapojua
kuwa Jina langu ndimi Bwana.
17:1 “Dhambi ya Yuda imechorwa kwa kalamu ya chuma,
imeandikwa kwa ncha ya almasi,
kwenye vibao vya mioyo yao
na kwenye pembe za madhabahu zao.
2 Hata watoto wao wanakumbuka madhabahu zao
na nguzo za Ashera,
kandokando ya miti iliyotanda
na juu ya vilima virefu.
3 Mlima wangu katika nchi pamoja na utajiri
na hazina zako zote nitazitoa ziwe nyara,
pamoja na mahali pako pa juu pa kuabudia miungu
kwa sababu ya dhambi katika nchi yako yote.
4 Kwa kosa lako mwenyewe utaupoteza
urithi niliokupa.
Nitakufanya mtumwa wa adui zako
katika nchi usiyoijua,
kwa kuwa umeiwasha hasira yangu,
nayo itawaka milele.”
5 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu,
ategemeaye mwenye mwili
kwa ajili ya nguvu zake,
ambaye moyo wake
umemwacha Bwana.
6 Atakuwa kama kichaka cha jangwani;
hataona mafanikio yatakapokuja.
Ataishi katika sehemu zisizo na maji,
katika nchi ya chumvi ambapo
hakuna yeyote aishiye humo.
7 “Lakini amebarikiwa mtu ambaye tumaini lake ni katika Bwana,
ambaye matumaini yake ni katika Bwana.
8 Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji
uenezao mizizi yake karibu na kijito cha maji.
Hauogopi wakati wa joto ujapo;
majani yake ni mabichi daima.
Hauna hofu katika mwaka wa ukame
na hautaacha kuzaa matunda.”
9 Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote,
ni mwovu kupita kiasi.
Ni nani awezaye kuujua?
10 “Mimi Bwana huchunguza moyo
na kuzijaribu nia,
ili kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake,
kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”
11 Kama kware aanguaye mayai asiyoyataga,
ndivyo alivyo mtu apataye mali kwa njia zisizo za haki.
Maisha yake yafikapo katikati, siku zitamwacha,
na mwishoni atabainika kuwa mpumbavu.
12 Kiti cha enzi kilichotukuzwa, kilichoinuliwa tangu mwanzo,
ndiyo sehemu yetu ya mahali patakatifu.
13 Ee Bwana, uliye tumaini la Israeli,
wote wakuachao wataaibika.
Wale wanaogeukia mbali nawe wataandikwa mavumbini
kwa sababu wamemwacha Bwana,
chemchemi ya maji yaliyo hai.
14 Uniponye, Ee Bwana, nami nitaponyeka;
uniokoe nami nitaokoka,
kwa maana wewe ndiwe ninayekusifu.
15 Wao huendelea kuniambia,
“Liko wapi neno la Bwana?
Sasa na litimie!”
16 Sijakukimbia na kuacha kuwa mchungaji wako;
unajua sijaitamani siku ya kukata tamaa.
Kile kipitacho midomoni mwangu
ki wazi mbele yako.
17 Usiwe kwangu kitu cha kunitia hofu kuu;
wewe ndiwe kimbilio langu katika siku ya maafa.
18 Watesi wangu na waaibishwe,
lakini nilinde mimi nisiaibike;
wao na watiwe hofu kuu,
lakini unilinde mimi na hofu kuu.
Waletee siku ya maafa;
waangamize kwa maangamizi maradufu.
19 Hili ndilo Bwana aliloniambia: “Nenda ukasimame kwenye lango la watu, mahali ambako wafalme wa Yuda huingilia na kutokea, simama pia kwenye malango mengine yote ya Yerusalemu. 20 Waambie, ‘Sikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda, nanyi watu wote wa Yuda, na kila mmoja aishiye Yerusalemu apitaye katika malango haya. 21 Hili ndilo asemalo Bwana: Jihadharini msije mkabeba mzigo siku ya Sabato, wala kuingiza mzigo kupitia malango ya Yerusalemu. 22 Msitoe mizigo nje ya nyumba zenu wala kufanya kazi yoyote wakati wa Sabato, lakini itakaseni siku ya Sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu. 23 Hata hivyo hawakusikiliza wala kujali, walishupaza shingo zao, na hawakutaka kusikia wala kukubali adhabu. 24 Lakini mkiwa waangalifu kunitii, asema Bwana, nanyi msipoleta mzigo wowote kupitia malango ya mji huu wakati wa Sabato, lakini mkaitakasa siku ya Sabato kwa kutofanya kazi siku hiyo, 25 ndipo wafalme wakaao juu ya kiti cha enzi cha Daudi wataingia kupitia malango ya mji huu, pamoja na maafisa wao. Wao na maafisa wao watakuja wakiwa wamepanda magari na farasi, wakiandamana na watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu, nao mji huu utakaliwa na watu daima. 26 Watu watakuja kutoka miji ya Yuda na vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, kutoka nchi ya Benyamini na chini ya vilima vya magharibi, kutoka nchi ya vilima na Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa na dhabihu, sadaka za nafaka, uvumba na sadaka za shukrani kwenye nyumba ya Bwana. 27 Lakini ikiwa hamtanitii mimi kwa kuitakasa Sabato na kwa kutochukua mzigo wowote mnapoingia katika malango ya Yerusalemu wakati wa Sabato, basi nitawasha moto usiozimika katika malango ya Yerusalemu utakaoteketeza ngome zake.’ ”