Maonyo Kwamba Utumwa ni Hakika (continued)
Unabii mbalimbali na miito kwa Wayahudi, ikitangaza kwamba utumwa wao na uharibifu wa Yerusalemu ni hakika.
609 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Hili ndilo neno la Bwana kwa Yeremia kuhusu ukame:
2 “Yuda anaomboleza,
miji yake inayodhoofika;
wanaomboleza kwa ajili ya nchi,
nacho kilio kinapanda kutoka Yerusalemu.
3 Wakuu wanawatuma watumishi wao maji;
wanakwenda visimani
lakini humo hakuna maji.
Wanarudi na vyombo bila maji;
wakiwa na hofu na kukata tamaa,
wanafunika vichwa vyao.
4 Ardhi imepasuka nyufa
kwa sababu hakuna mvua katika nchi;
wakulima wana hofu
na wanafunika vichwa vyao.
5 Hata kulungu mashambani
anamwacha mtoto wake aliyezaliwa wakati huo huo
kwa sababu hakuna majani.
6 Punda-mwitu wanasimama juu ya miinuko iliyo kame
na kutweta kama mbweha;
macho yao yanakosa nguvu za kuona
kwa ajili ya kukosa malisho.”
7 Ingawa dhambi zetu zinashuhudia juu yetu,
Ee Bwana, tenda jambo kwa ajili ya jina lako.
Kwa kuwa kukengeuka kwetu ni kukubwa,
nasi tumetenda dhambi dhidi yako.
8 Ee Tumaini la Israeli,
Mwokozi wake wakati wa taabu,
kwa nini unakuwa kama mgeni katika nchi,
kama msafiri anayekaa kwa usiku mmoja tu?
9 Mbona unakuwa kama mtu aliyeshtukizwa,
kama shujaa asiye na uwezo wa kuokoa?
Wewe uko katikati yetu, Ee Bwana,
nasi tunaitwa kwa jina lako;
usituache!
10 Hili ndilo Bwana asemalo kuhusu watu hawa:
“Wanapenda sana kutangatanga,
hawaizuii miguu yao.
Hivyo Bwana hawakubali;
sasa ataukumbuka uovu wao
na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.”
11 Kisha Bwana akaniambia, “Usiombe kwa ajili ya mafanikio ya watu hawa. 12 Ingawa wanafunga, sitasikiliza kilio chao; hata wakitoa dhabihu za kuteketezwa na dhabihu za nafaka, sitazikubali. Badala yake, nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.”
13 Lakini nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, manabii wanaendelea kuwaambia, ‘Hamtaona upanga wala kukabiliwa na njaa. Naam, nitawapa amani ya kudumu mahali hapa.’ ”
14 Ndipo Bwana akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma, wala sikuwaweka, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi, maono ya sanamu zisizofaa kitu, na madanganyo ya mawazo yao wenyewe. 15 Kwa hiyo, hili ndilo Bwana asemalo kuhusu manabii wanaotabiri kwa jina langu: Mimi sikuwatuma, lakini wanasema, ‘Hakuna upanga wala njaa itakayoigusa nchi hii.’ Manabii hao hao watakufa kwa upanga na njaa. 16 Nao watu hao wanaowatabiria watatupwa nje katika barabara za Yerusalemu kwa sababu ya njaa na upanga. Hapatakuwepo yeyote wa kuwazika wao au wake zao, wana wao au binti zao. Nitawamwagia maafa wanayostahili.
17 “Nena nao neno hili:
“ ‘Macho yangu na yatiririkwe na machozi
usiku na mchana bila kukoma;
kwa kuwa binti yangu aliye bikira, yaani watu wangu,
amepata jeraha baya,
pigo la kuangamiza.
18 Kama nikienda mashambani,
ninaona wale waliouawa kwa upanga;
kama nikienda mjini,
ninaona maangamizi ya njaa.
Nabii na kuhani kwa pamoja
wamekwenda katika nchi wasiyoijua.’ ”
19 Je, umemkataa Yuda kabisa?
Umemchukia Sayuni kabisa?
Kwa nini umetuumiza
hata hatuwezi kuponyeka?
Tulitarajia amani,
lakini hakuna jema lililotujia;
tulitarajia wakati wa kupona
lakini kuna hofu kuu tu.
20 Ee Bwana, tunatambua uovu wetu
na kosa la baba zetu;
kweli tumetenda dhambi dhidi yako.
21 Kwa ajili ya jina lako usituchukie kabisa;
usikidharau kiti chako cha enzi kilichotukuka.
Kumbuka agano lako nasi
na usilivunje.
22 Je, kuna sanamu yoyote isiyofaa kitu ya mataifa
iwezayo kuleta mvua?
Je, anga peke yake zaweza kutoa mvua?
La hasha, ni wewe peke yako,
Ee Bwana, Mungu wetu.
Kwa hiyo tumaini letu liko kwako,
kwa kuwa wewe ndiwe ufanyaye haya yote.
15:1 Kisha Bwana akaniambia: “Hata kama Mose na Samweli wangesimama mbele zangu, moyo wangu usingewaelekea watu hawa. Waondoe mbele za macho yangu! Waache waende! 2 Nao kama wakikuuliza, ‘Twende wapi?’ Waambie, ‘Hili ndilo Bwana asemalo:
“ ‘Wale waliowekwa kwa ajili ya kufa, wakafe;
waliowekwa kwa ajili ya upanga, kwa upanga;
waliowekwa kwa ajili ya njaa, kwa njaa:
waliowekwa kwa ajili ya kutekwa, watekwe.’ ”
3 Bwana asema, “Nitatuma aina nne za waharabu dhidi yao: nazo ni upanga ili kuua na mbwa ili wakokote mbali, ndege wa angani na wanyama wa nchi ili kula na kuangamiza. 4 Nitawafanya wawe machukizo kwa falme zote za dunia kwa sababu ya kile alichofanya Manase mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda huko Yerusalemu.
5 “Ni nani atakayekuhurumia, ee Yerusalemu?
Ni nani atakayeomboleza kwa ajili yako?
Ni nani atakayesimama ili kuuliza
kuhusu hali yako?
6 Umenikataa mimi,” asema Bwana.
“Unazidi kukengeuka.
Hivyo nitanyoosha mkono wangu juu yako na kukuangamiza,
siwezi kuendelea kukuonea huruma.
7 Nitawapepeta kwa uma wa kupepetea
kwenye malango ya miji katika nchi.
Nitaleta msiba na maangamizi juu ya watu wangu,
kwa maana hawajabadili njia zao.
8 Nitawafanya wajane wao kuwa wengi
kuliko mchanga wa bahari.
Wakati wa adhuhuri nitamleta mharabu
dhidi ya mama wa vijana wao waume;
kwa ghafula nitaleta juu yao
maumivu makuu na hofu kuu.
9 Mama mwenye watoto saba atazimia
na kupumua pumzi yake ya mwisho.
Jua lake litatua kungali bado mchana,
atatahayarika na kufedheheka.
Wale wote waliobaki nitawaua kwa upanga
mbele ya adui zao,”
asema Bwana.
10 Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa,
mtu ambaye ulimwengu wote
unashindana na kugombana naye!
Sikukopa wala sikukopesha,
lakini kila mmoja ananilaani.
11 Bwana akasema,
“Hakika nitakuokoa kwa kusudi jema,
hakika nitawafanya adui zako wakuombe msaada
nyakati za maafa na nyakati za dhiki.
12 “Je, mtu aweza kuvunja chuma,
chuma kitokacho kaskazini, au shaba?
13 Utajiri wako na hazina zako nitavitoa kuwa nyara,
bila gharama,
kwa sababu ya dhambi zako zote
katika nchi yako yote.
14 Nitakufanya uwe mtumwa wa adui zako
katika nchi usiyoijua,
kwa kuwa katika hasira yangu moto umewashwa
utakaowaka juu yako daima.”
15 Wewe unafahamu, Ee Bwana,
unikumbuke na unitunze mimi.
Lipiza kisasi juu ya watesi wangu.
Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali;
kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.
16 Maneno yako yalipokuja, niliyala;
yakawa shangwe yangu
na furaha ya moyo wangu,
kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako,
Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.
17 Kamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe,
wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao;
niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako ulikuwa juu yangu,
na wewe ulikuwa umenijaza hasira.
18 Kwa nini maumivu yangu hayakomi,
na jeraha langu ni la kuhuzunisha,
wala haliponyeki?
Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu,
kama chemchemi iliyokauka?
19 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana:
“Kama ukitubu, nitakurejeza
ili uweze kunitumikia;
kama ukinena maneno yenye maana,
wala si ya upuzi,
utakuwa mnenaji wangu.
Watu hawa ndio watakaokugeukia,
wala si wewe utakayewageukia wao.
20 Nitakufanya wewe uwe ukuta kwa watu hawa,
ngome ya ukuta wa shaba;
watapigana nawe
lakini hawatakushinda,
kwa maana mimi niko pamoja nawe
kukuponya na kukuokoa,”
asema Bwana.
21 “Nitakuokoa kutoka mikono ya waovu,
na kukukomboa kutoka makucha ya watu wakatili.”