Kwa Sardi na Makanisa Ambayo Bidii Yao Inapungua
Ujumbe kwa kanisa la Sardi, na kwa makanisa yote yanayoacha bidii na uaminifu wao kupungua.
96 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika:
“Haya ndiyo maneno ya aliye na zile Roho saba za Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa. 2 Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyosalia na yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu. 3 Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia, yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwizi wala hutajua saa nitakayokuja kwako.
4 “Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili. 5 Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao. Sitafuta jina lake kutoka kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake. 6 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.
Kwa Filadelfia na Makanisa Yenye Uaminifu na Bidii
Ujumbe kwa kanisa la Filadelfia, na kwa makanisa yote yanayotenda kwa bidii na uaminifu, kadiri nafasi na uwezo wao unavyoruhusu.
7 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika:
“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, yeye aliye na ufunguo wa Daudi. Anachokifungua hakuna awezaye kukifunga, wala anachokifunga hakuna awezaye kukifungua. 8 Nayajua matendo yako. Tazama, nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, wala hakuna awezaye kuufunga. Ninajua kwamba una nguvu kidogo lakini umelishika neno langu wala hukulikana Jina langu. 9 Nitawafanya wale wa sinagogi la Shetani, wale ambao husema kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali ni waongo, nitawafanya waje wapige magoti miguuni pako, na wakiri ya kwamba nimekupenda. 10 Kwa kuwa umeshika amri yangu ya kuvumilia katika saburi, nitakulinda katika saa ya kujaribiwa inayokuja ulimwenguni pote, ili kuwajaribu wote wakaao duniani.
11 “Ninakuja upesi. Shika sana ulicho nacho, ili mtu asije akaichukua taji yako. 12 Yeye ashindaye nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo kamwe. Nitaandika juu yake Jina la Mungu wangu na jina la mji mkubwa wa Mungu wangu, Yerusalemu mpya, ambao unashuka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Nami pia nitaandika juu yake Jina langu jipya. 13 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.
Kwa Laodikia na Makanisa Tajiri, Yenye Kiburi na Uvuguvugu
Ujumbe kwa kanisa la Laodikia, na kwa makanisa yote yaliyo tajiri, yenye kiburi na uvuguvugu.
14 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika:
“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu. 15 Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa moja au lingine. 16 Hivyo kwa kuwa u vuguvugu, si baridi wala moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu. 17 Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi. 18 Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.
19 “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu. 20 Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu yeyote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.
21 “Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi. 22 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.”
Uumbaji Wote Unamwabudu Yesu Kristo
Maono ya Yohana yanaanza kwa picha ya viumbe vyote vikiungana katika kumwabudu Yesu Kristo, Mungu wa Ukristo.
1 Baada ya mambo hayo nilitazama, nami nikaona mbele yangu mlango uliokuwa wazi mbinguni. Nayo ile sauti niliyokuwa nimeisikia hapo mwanzo ikisema nami kama tarumbeta ikasema, “Njoo, huku, nami nitakuonyesha yale ambayo hayana budi kutokea baada ya haya.” 2 Ghafula nilikuwa katika Roho, na hapo mbele yangu kilikuwepo kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa na mtu. 3 Aliyekuwa amekikalia alikuwa anaonekana kama yaspi na akiki. Kukizunguka kile kiti cha enzi palikuwa na upinde wa mvua ulioonekana kama zumaridi.
4 Kukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti vingine vya enzi ishirini na vinne, na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne. Walivaa mavazi meupe, na walikuwa na taji za dhahabu vichwani mwao. 5 Kwenye kile kiti cha enzi palikuwa panatoka miali ya umeme wa radi, ngurumo na sauti za radi. Mbele ya kiti cha enzi, taa saba zilikuwa zinawaka. Hizi ndizo roho saba za Mungu. 6 Pia mbele ya kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama bilauri.
Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wakiwa wamejawa na macho mbele na nyuma. 7 Kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ngʼombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka. 8 Kila mmoja wa hawa viumbe wanne wenye uhai alikuwa na mabawa sita, na kujawa na macho pande zote hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawaachi kusema:
“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
ni Bwana Mungu Mwenyezi,
aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”
9 Kila mara viumbe hao wanne wenye uhai wanapomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aketiye kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele, 10 wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake aketiye kwenye kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi, wakisema:
11 “Bwana wetu na Mungu wetu,
wewe unastahili kupokea utukufu
na heshima na uweza,
kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,
na kwa mapenzi yako viliumbwa
na vimekuwako.”
Hakuna Mwanadamu Anayeweza Kufungua Hati ya Kukunjwa Iliyotiwa Mihuri
Katika maono yake, Yohana anaona hati ya kukunjwa yenye mihuri saba, iliyo na historia ya wakati ujao ya kanisa la Mungu, ambayo hakuna mwanadamu aliyeweza kuifungua.
1 Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na upande wa nje, kikiwa kimefungwa kwa lakiri saba. 2 Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, akisema, “Ni nani anayestahili kuzivunja hizo lakiri na kukifungua kitabu?” 3 Lakini hapakuwa na yeyote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu wala hata kutazama ndani yake.
Mwana-Kondoo Anafungua Hati ya Kukunjwa
Mwana wa Mungu, anayeonyeshwa kama mwana-kondoo akitolewa dhabihu, analifungua lile gombo ili kulionyesha kanisa historia ya jinsi Mungu atakavyoliongoza kwa maongozi yake hadi mwisho wa nyakati. Uumbaji wote unamsifu na kumheshimu upya Mwana-Kondoo wa Mungu aliyetolewa dhabihu.
4 Nikalia sana sana kwa sababu hakuonekana yeyote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake. 5 Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja hizo lakiri zake saba.”
6 Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne na miongoni mwa wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba za Mungu zilizotumwa duniani pote. 7 Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka kwenye mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi. 8 Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu. 9 Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema:
“Wewe unastahili kukitwaa kitabu
na kuzivunja lakiri zake,
kwa sababu ulichinjwa
na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu
kutoka kila kabila, kila lugha,
kila jamaa na kila taifa.
10 Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani
wa kumtumikia Mungu wetu,
nao watatawala duniani.”
11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. 12 Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema:
“Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,
kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu
na heshima na utukufu na sifa!”
13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba:
“Sifa na heshima na utukufu na uweza
ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi
na kwa Mwana-Kondoo,
milele na milele!”
14 Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.