Yohana Anaandika Ufunuo
Mtume Yohana anaandika Ufunuo (yaelekea mwaka wa 96 BK) ili uchukue nafasi ya mfululizo unaoendelea wa manabii katika kanisa la Kikristo hadi kuja kwa Kristo mara ya pili kuuhukumu ulimwengu.
96 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Kila Mtu Anaambiwa Ajifunze Ufunuo
Wanadamu wote wanaamriwa kujifunza Ufunuo.
1 Ufunuo wa Yesu Kristo aliopewa na Mungu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo ni lazima yatukie hivi karibuni. Alijulisha mambo haya kwa kumtuma malaika wake kwa Yohana mtumishi wake, 2 ambaye anashuhudia kuhusu kila kitu alichokiona, yaani, Neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu Kristo. 3 Amebarikiwa yeye asomaye maneno ya unabii huu, na wamebarikiwa wale wanaoyasikia na kuyatia moyoni yale yaliyoandikwa humo, kwa sababu wakati umekaribia.
Yohana Anayasalimu Makanisa
Yohana anayasalimu makanisa na kuthibitisha uungu wa Mwokozi wao, atakayekuja kuhukumu ulimwengu.
4 Yohana, kwa makanisa saba yaliyoko Asia:
Neema na amani iwe kwenu kutoka kwake aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, na kutoka kwa wale roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi, 5 na kutoka kwa Yesu Kristo ambaye ni yule shahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, mtawala wa wafalme wa dunia.
Kwake yeye anayetupenda na ambaye ametuweka huru kutoka dhambi zetu kwa damu yake, 6 akatufanya sisi kuwa ufalme na makuhani, tumtumikie Mungu wake ambaye ni Baba yake. Utukufu na uwezo ni vyake milele na milele! Amen.
7 Tazama! Anakuja na mawingu,
na kila jicho litamwona,
hata wale waliomchoma;
na makabila yote duniani
yataomboleza kwa sababu yake.
Naam, ndivyo itakavyokuwa! Amen.
8 “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu, “aliyeko, aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.”
Kristo Anamtokea Yohana huko Patmo
Yohana anaeleza jinsi Kristo alivyomtokea katika kisiwa cha Patmo, na kuhusu kupewa kwake jukumu la kuwa nabii.
9 Mimi, Yohana, ndugu yenu ninayeshiriki pamoja nanyi mateso katika Yesu na katika ufalme na uvumilivu katika saburi, nilikuwa katika kisiwa cha Patmo kwa ajili ya neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu. 10 Katika siku ya Bwana, nilikuwa katika Roho na nikasikia sauti kubwa kama ya baragumu nyuma yangu 11 ikisema, “Andika kwenye kitabu haya yote unayoyaona, kisha uyapeleke kwa makanisa saba, yaani: Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”
12 Ndipo nikageuka ili nione ni sauti ya nani iliyokuwa ikisema nami. Nami nilipogeuka, nikaona vinara saba vya taa vya dhahabu, 13 na katikati ya vile vinara vya taa, alikuwamo mtu kama Mwana wa Adamu, akiwa amevaa joho refu, na mkanda wa dhahabu ukiwa umefungwa kifuani mwake. 14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. 15 Nyayo zake zilikuwa kama shaba inayongʼaa, katika tanuru ya moto, nayo sauti yake ilikuwa kama mugurumo ya maji mengi. 16 Katika mkono wake wa kuume alishika nyota saba, na kinywani mwake ulitoka upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa kama jua likingʼaa kwa nguvu zake zote.
17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.
19 “Basi andika mambo uliyoyaona, yaliyopo na yale yatakayotukia baada ya haya. 20 Kuhusu siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume na vile vinara saba vya taa vya dhahabu ni hii: Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, navyo vile vinara saba ni hayo makanisa saba.
Kwa Efeso na Makanisa Yote Yanayoiacha Imani
Ujumbe kwa kanisa la Efeso, na kwa makanisa yote yanayoanza kuiacha imani.
1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika:
“Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea kati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu. 2 Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo. 3 Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.
4 “Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza. 5 Kumbuka basi ni wapi ulikoangukia! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake. 6 Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami pia nayachukia.
7 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa haki ya kula matunda toka kwa mti wa uzima, ambao uko katika paradiso ya Mungu.
Kwa Smirna na Makanisa Yote Yanayoteswa
Ujumbe kwa kanisa la Smirna, na kwa makanisa yote yaliyo katika mateso na dhiki.
8 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika:
“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa kisha akafufuka. 9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi la Shetani. 10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.
11 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatadhuriwa kamwe na mauti ya pili.
Kwa Pergamo na Makanisa Yanayoruhusu Upotovu Uingie
Ujumbe kwa kanisa la Pergamo, na kwa makanisa yote ambayo, kwa kulegeza nidhamu yao, yamewaruhusu walimu wa upotovu kuingia.
12 “Kwa malaika wa Kanisa lililoko Pergamo andika:
“Haya ndiyo maneno yake yeye aliye na upanga mkali wenye makali kuwili. 13 Ninajua unakoishi, ni kule ambako Shetani ana kiti chake cha enzi. Lakini umelishika Jina langu. Wala hukuikana imani yako kwangu hata katika siku za shahidi wangu mwaminifu Antipa, ambaye aliuawa katika mji mkuu wenu, ambako ndiko anakoishi Shetani.
14 “Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa kafara kwa sanamu na kufanya uasherati. 15 Vivyo hivyo unao wale wayashikayo mafundisho ya Wanikolai. 16 Basi tubu! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu.
17 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa. Nitampa pia jiwe jeupe ambalo juu yake limeandikwa jina jipya asilolijua mtu, isipokuwa yule anayelipokea.
Kwa Thiatira na Makanisa Yanayoruhusu Upotovu wa Maadili
Ujumbe kwa kanisa la Thiatira, na kwa makanisa yote yanayoendelea kuikiri imani ya kweli na kutenda matendo mengi mema kwa njia mbalimbali, lakini bado yanaruhusu upotovu wa maadili na ibada ya sanamu kuendelea miongoni mwao.
18 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika:
“Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa sana. 19 Nayajua matendo yako, upendo wako na imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza.
20 “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu. 21 Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki. 22 Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake. 23 Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia, na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake. 24 Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo yanayoitwa mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wowote juu yenu): 25 Lakini shikeni sana mlicho nacho, mpaka nitakapokuja.
26 “Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu mpaka mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa:
27 “ ‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma,
atawavunja vipande vipande
kama chombo cha udongo’:
kama vile mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu. 28 Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi. 29 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.