Sehemu ya 14: Ufufuo na Kupaa kwa Kristo
Ufufuo, kujitokeza, na kupaa kwa Kristo.
Katika kipindi cha siku arobaini, kuanzia Jumapili baada ya kifo cha Kristo. Majira ya kuchipua ya mwaka wa 30 BK (au 29). Uyahudi na Galilaya
Wanawake Wanatembelea Kaburi la Yesu
Golgotha na Bethania. Mwishoni mwa alasiri na mwanzoni mwa jioni ya Jumamosi kwa hesabu yetu
Wanalitazama kaburi mwishoni mwa Sabato (alasiri ya Jumamosi kwa hesabu yetu), na kununua manukato baada ya Sabato (baada ya 6 P.M. Jumamosi), siku ya kwanza ya juma.
30 au 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 28:1
28:1 Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi.
Marko 16:1
16:1 Sabato ilipomalizika, Maria Magdalene, Maria mama yake Yakobo, na Salome walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu.
Malaika Analiviringisha Jiwe na Kuliondoa
Kuna tetemeko la ardhi, malaika analiviringisha jiwe na kuliondoa, na walinzi Warumi wanaogopa sana.
Jumapili kabla ya jua kuchomoza
Mathayo 28:2–4
28:2 Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaenda penye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. 3 Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4 Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.
Malaika Wanawaambia Wanawake kuhusu Kaburi Tupu
Wanawake wanatembelea kaburi la Yesu karibu na wakati wa kuchomoza kwa jua Jumapili asubuhi, na malaika wanawapa ujumbe kuhusu kaburi tupu.
Golgotha. Jumapili asubuhi na mapema
Mathayo 28:5–8
28:5 Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. 6 Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa.
7 Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ”
8 Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, bali wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo.
Marko 16:2–8
16:2 Asubuhi na mapema, siku ya kwanza ya juma, mara tu baada ya kuchomoza jua, walikwenda kaburini. 3 Njiani wakawa wanaulizana wao kwa wao, “Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe kutoka kwenye ingilio la kaburi?”
4 Lakini walipotazama, wakaona lile jiwe, ambalo lilikuwa kubwa sana, limekwisha kuvingirishwa kutoka pale penye ingilio la kaburi.
5 Walipokuwa wakiingia mle kaburini, wakamwona kijana mmoja aliyevaa joho jeupe akiwa ameketi upande wa kuume, nao wakastaajabu.
6 Yule malaika akawaambia, “Msistaajabu. Mnamtafuta Yesu, Mnazareti, aliyesulubiwa. Amefufuka! Hayuko hapa. Tazameni mahali walipomlaza.
7 Lakini nendeni mkawaambie wanafunzi wake pamoja na Petro, kwamba, ‘Anawatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona, kama alivyowaambia.’ ”
8 Hivyo wakatoka, wakakimbia kutoka mle kaburini wakiwa na hofu kuu na mshangao. Nao hawakumwambia mtu yeyote neno lolote, kwa sababu waliogopa.
Luka 24:1–8
24:1 Mnamo siku ya kwanza ya juma, alfajiri na mapema, wale wanawake walichukua yale manukato waliyokuwa wameyaandaa, wakaenda kaburini.
2 Wakakuta lile jiwe limevingirishwa kutoka kwenye kaburi, 3 lakini walipoingia ndani, hawakuuona mwili wa Bwana Yesu. 4 Walipokuwa wanashangaa juu ya jambo hili, ghafula watu wawili waliokuwa wamevaa mavazi yanayongʼaa kama umeme wakasimama karibu nao.
5 Wale wanawake, wakiwa na hofu, wakainamisha nyuso zao mpaka chini. Lakini wale watu wakawaambia, “Kwa nini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu?
6 Hayuko hapa; amefufuka! Kumbukeni alivyowaambia alipokuwa bado yuko pamoja nanyi huko Galilaya kwamba: 7 ‘Ilikuwa lazima Mwana wa Adamu atiwe mikononi mwa watu wenye dhambi na waovu ili asulubiwe, na siku ya tatu afufuke.’ ” 8 Ndipo wakayakumbuka maneno ya Yesu.
Yohana 20:1
20:1 Alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa kungali giza bado, Maria Magdalene alikwenda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio.
Petro na Yohana Wanatembelea Kaburi Tupu
Maria Magdalene na wanawake wengine wanawapa mitume habari, na Petro na Yohana wanatembelea kaburi tupu.
Luka 24:9–12
24:9 Waliporudi kutoka huko kaburini, wakawaeleza wale wanafunzi kumi na mmoja pamoja na wengine wote mambo haya yote. 10 Basi Maria Magdalene, Yoana, na Maria mama yake Yakobo, pamoja na wanawake wengine waliofuatana nao ndio waliwaelezea mitume habari hizi.
11 Lakini hawakuwasadiki hao wanawake, kwa sababu maneno yao yalionekana kama upuzi.
12 Hata hivyo, Petro akainuka na kukimbia kwenda kule kaburini. Alipoinama kuchungulia, akaona vile vitambaa vya kitani, ila hakuona kitu kingine. Naye akaenda zake akijiuliza nini kilichotokea.
Yohana 20:2–10
20:2 Hivyo akaja akikimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na hatujui walikomweka!”
3 Petro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara kuelekea kaburini.
4 Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 5 Alipofika, akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani mle ndani, lakini hakuingia. 6 Ndipo Simoni Petro akaja, akimfuata nyuma akaenda moja kwa moja hadi ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini 7 na kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Yesu. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa mahali pa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda. 8 Kisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini naye akaingia ndani, akaona, akaamini, 9 (kwa kuwa mpaka wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Yesu afufuke kutoka kwa wafu).
10 Kisha hao wanafunzi wakaondoka wakarudi nyumbani kwao.