Yesu Anazikwa katika Kaburi la Yosefu wa Arimathaya

Baada ya kifo chake kuthibitishwa, mwili wa Yesu unazikwa katika kaburi la Yosefu wa Arimathaya.

Ijumaa alasiri kabla ya 6 p.m.

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 27:57–60

27:57 Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.

58 Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe.

59 Yosefu akauchukua mwili wa Yesu, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi,

60 na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake.

Marko 15:42–46

15:42 Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizi, yaani siku moja kabla ya Sabato,

43 Yosefu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na ambaye alikuwa anautarajia Ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Yesu.

44 Pilato alikuwa akijiuliza kama Yesu alikuwa amekwisha kufa. Hivyo akamwita yule jemadari, akamuuliza iwapo Yesu alikuwa amekwisha kufa. 45 Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yosefu ruhusa ya kuuchukua huo mwili.

46 Hivyo Yosefu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili kutoka msalabani, akaufunga katika kile kitambaa cha kitani, na kuuweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi.

Luka 23:50–54

23:50 Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yosefu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi, 51 lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa mwenyeji wa Arimathaya huko Uyahudi, naye alikuwa anaungojea Ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa.

52 Yosefu alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.

53 Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado.

54 Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza.

Yohana 19:31–42

19:31 Kwa kuwa ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, Wayahudi hawakutaka miili ibaki msalabani siku ya Sabato, hasa kwa kuwa hiyo Sabato ingekuwa Sikukuu. Wakamwomba Pilato aamuru miguu ya wale waliosulubiwa ivunjwe ili wafe haraka miili iondolewe kwenye misalaba. 32 Kwa hiyo askari wakaenda wakavunja miguu ya mtu wa kwanza aliyesulubiwa pamoja na Yesu na yule mwingine pia. 33 Lakini walipomkaribia Yesu, wakaona ya kuwa amekwisha kufa, hivyo hawakuvunja miguu yake. 34 Badala yake mmoja wa wale askari akamchoma mkuki ubavuni na mara pakatoka damu na maji. 35 Mtu aliyeona mambo hayo ndiye alitoa ushuhuda, nao ushuhuda wake ni kweli. Anajua kuwa anasema kweli, naye anashuhudia ili pia nanyi mpate kuamini. 36 Kwa maana mambo haya yalitukia ili Maandiko yapate kutimia, yale yasemayo, “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.” 37 Tena Andiko lingine lasema, “Watamtazama yeye waliyemchoma.”

38 Baada ya mambo haya, Yosefu wa Arimathaya, aliyekuwa mfuasi wa Yesu, ingawa kwa siri kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili kuuchukua mwili wa Yesu. Pilato alimruhusu, hivyo akaja, akauchukua.

39 Naye Nikodemo, yule ambaye kwanza alimwendea Yesu usiku, akaja, akaleta mchanganyiko wa manemane na manukato, yenye uzito wa zaidi ya kilo thelathini

40 Wakauchukua mwili wa Yesu, wakaufunga katika sanda ya kitani safi pamoja na yale manukato, kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi. 41 Basi palikuwa na bustani karibu na mahali pale aliposulubiwa, na pale ndani ya ile bustani palikuwa na kaburi jipya, ambalo halikuwa limezikiwa mtu bado.

42 Kwa hiyo, kwa kuwa ilikuwa siku ya Wayahudi ya Maandalio, nalo kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamzika Yesu humo.

Wanawake Wanakaa Macho Kando ya Kaburi la Yesu

Ijumaa alasiri hadi Jumamosi alasiri

Wanawake wanaendelea kukesha na kupumzika siku ya Sabato (inayoanza saa 6 P.M.), huku Mafarisayo wakiagiza kikosi cha askari Warumi kuulinda muhuri wa Warumi ulioko kwenye kaburi.

Mathayo 27:61–66

27:61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwepo mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.

62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato 63 na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu wakati alikuwa bado hai alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ 64 Kwa hiyo uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti mpaka baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuliwa kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”

65 Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadri mwezavyo.” 66 Kwa hiyo wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.

Marko 15:47

15:47 Maria Magdalene na Maria mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.

Luka 23:55–56

23:55 Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Yesu wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yosefu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Yesu ulivyolazwa. 56 Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.