Saa Tatu za Giza

Saa tatu za giza, kuanzia adhuhuri hadi saa tisa alasiri.

(Kauli nyingine nne mwishoni mwa giza, na kifo cha Kristo.)

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 27:45–50

27:45 Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote.

46 Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)

47 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Eliya.”

48 Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe.

49 Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.”

50 Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.

Marko 15:33–37

15:33 Ilipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa.

34 Mnamo saa tisa, Yesu akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)

35 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hayo, wakasema, “Msikieni, anamwita Eliya.”

36 Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe, akisema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.”

37 Kisha Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho.

Luka 23:44–46

23:44 Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa,

45 kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili.

46 Yesu akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho.

Yohana 19:28–30

19:28 Baada ya haya, Yesu hali akijua kuwa mambo yote yamemalizika, alisema ili kutimiza Maandiko, “Naona kiu.”

29 Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni. 30 Baada ya kuionja hiyo siki, Yesu akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.

Matukio Yanayoambatana na Kifo cha Kristo

Mathayo 27:51–56

27:51 Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. 52 Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. 53 Wakatoka makaburini, na baada ya Yesu kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.

54 Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa, wakasema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

55 Walikuwako wanawake huko wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake.

56 Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo na Yosefu, na mama yao wana wa Zebedayo.

Marko 15:38–41

15:38 Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini.

39 Basi yule jemadari aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Yesu aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

40 Walikuwepo pia wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali. Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome.

41 Hawa walifuatana na Yesu na kushughulikia mahitaji yake alipokuwa Galilaya. Pia walikuwepo wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye Yerusalemu.

Luka 23:47–49

23:47 Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.”

48 Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao.

49 Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya.