Saa Tatu za Kwanza Msalabani

Kuanzia saa tatu asubuhi hadi adhuhuri Ijumaa (kauli tatu za Yesu; askari wanapiga kura kwa ajili ya vazi la Yesu; maandishi juu ya msalaba; umati, Baraza la Wayahudi, askari, na hata wale wanyang'anyi wawili walioko kila upande wa Kristo wanamdhihaki Yesu)

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 27:35–44

27:35 Walipokwisha kumsulubisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie lile neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”]

36 Kisha wakaketi, wakamchunga.

37 Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.

38 Wanyangʼanyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto.

39 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao 40 na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka msalabani.”

41 Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wakamdhihaki wakisema, 42 “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni Mfalme wa Israeli! Ashuke sasa kutoka msalabani, nasi tutamwamini.

43 Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ”

44 Hata wale wanyangʼanyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.

Marko 15:24–32

15:24 Basi wakamsulubisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni gani kila mtu ataichukua.

25 Ilikuwa yapata saa tatu asubuhi walipomsulubisha. 26 Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya: “Mfalme wa Wayahudi.”

27 Pamoja naye walisulubiwa wanyangʼanyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. [ 28 Nayo maandiko yakatimizwa, yale yasemayo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.]”

29 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, 30 basi shuka kutoka msalabani na ujiokoe mwenyewe!”

31 Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa sheria wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe!

32 Basi huyu Kristo, huyu Mfalme wa Israeli, ashuke sasa kutoka msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulubiwa pamoja naye pia wakamtukana.

Luka 23:34, 38, 35–37, 39–43

23:34 Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.

38 Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.

Maandishi haya yalikuwa yameandikwa kwa lugha za Kiyunani, Kilatini na Kiebrania.

35 Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Kristo wa Mungu, Mteule wake.”

36 Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe,

37 na wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”

39 Mmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Kristo? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.”

40 Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu iyo hiyo? 41 Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.”

42 Kisha akasema, “Yesu, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.”

43 Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”

Yohana 19:18, 23–24, 19–22, 25–27

19:18 Hapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wengine wawili, mmoja kila upande wake, naye Yesu katikati.

23 Askari walipokwisha kumsulubisha Yesu, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono bali limefumwa tangu juu hadi chini. 24 Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.”

Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema,

“Wanagawana nguo zangu,

na vazi langu wanalipigia kura.”

Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.

19 Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Yesu, likasema: “Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi.” 20 Kwa kuwa mahali hapo Yesu aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini.

21 Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.”

22 Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!”

25 Wakati huo huo karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Maria mke wa Klopa, na Maria Magdalene. 26 Yesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,” 27 kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake.