Askari Warumi Wanamdhihaki Yesu

Ijumaa, kati ya saa 6 na saa 9 asubuhi kwa saa za Kizungu

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 27:27–30

27:27 Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitorio na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka.

28 Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha

29 wakasokota taji ya miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” 30 Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena.

Marko 15:16–19

15:16 Askari wakampeleka Yesu hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio, wakakusanya kikosi kizima cha askari.

17 Wakamvalisha Yesu joho la zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani.

18 Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” 19 Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki.

Yesu Njiani Kuelekea Msalabani

Yesu njiani kuelekea msalabani (Via Dolorosa) huko Golgotha.

Kabla ya saa 9 asubuhi kwa saa za Kizungu, siku ya Ijumaa

Mathayo 27:31–34

27:31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe.

32 Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.

33 Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).

34 Hapo wakampa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa.

Marko 15:20–23

15:20 Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.

21 Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Aleksanda na Rufo, alikuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shamba, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.

22 Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).

23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa.

Luka 23:26–33

23:26 Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni mwenyeji wa Kirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Yesu. 27 Idadi kubwa ya watu wakamfuata Yesu, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea. 28 Yesu akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. 29 Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’ 30 Ndipo

“ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!”

na vilima, “Tufunikeni!” ’

31 Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?”

32 Watu wengine wawili wahalifu, walipelekwa pamoja na Yesu ili wakasulubiwe.

33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto.

Yohana 19:17

19:17 Yesu, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha).