Yesu Mbele ya Pilato kwa Mara ya Pili
Ijumaa karibu na macheo (Yohana 19:14)
Pilato anakubali polepole, kwa shingo upande na kwa hofu, dai la Baraza la Wayahudi la kutaka Kristo asulubiwe.
30 au 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 27:15–26
27:15 Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu.
16 Wakati huo alikuwepo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba.
17 Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu yeye aitwaye Kristo?”
18 Kwa kuwa alitambua Yesu alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu.
19 Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”
20 Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakaushawishi ule umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Yesu auawe.
21 Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?”
Wakajibu, “Baraba.”
22 Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?”
Wakajibu wote, “Msulubishe!”
23 Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”
Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”
24 Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Sina hatia juu ya damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”
25 Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”
26 Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
Marko 15:6–15
15:6 Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka.
7 Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi. 8 Ule umati wa watu ukamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake.
9 Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu Mfalme wa Wayahudi?”
10 Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Yesu mikononi mwake kwa ajili ya wivu.
11 Lakini viongozi wa makuhani wakauchochea ule umati wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake.
12 Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”
13 Wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe!”
14 Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”
Lakini wao wakapiga kelele kwa nguvu zaidi, wakisema, “Msulubishe!”
15 Pilato, akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
Luka 23:13–25
23:13 Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu, 14 akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami nimeona hakuna msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake. 15 Wala Herode hakumwona na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo.
16 Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachia.” [ 17 Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.]
18 Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyo! Tufungulie Baraba!” 19 (Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji.)
20 Pilato, akitaka kumwachia Yesu, akasema nao tena. 21 Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”
22 Kwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.”
23 Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu zaidi, wakidai kwamba Yesu asulubiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda.
24 Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe.
25 Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Yesu mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.
Yohana 18:39–19:16
18:39 Lakini ninyi mna desturi yenu kwamba wakati wa Pasaka nimwachie huru mfungwa mmoja mnayemtaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?”
40 Wao wakapiga kelele wakisema, “Si huyu mtu, bali tufungulie Baraba!” Yule Baraba alikuwa mnyangʼanyi.
19:1 Ndipo Pilato akamtoa Yesu akaamuru apigwe mijeledi. 2 Askari wakasokota taji ya miiba, wakamvika Yesu kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau. 3 Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu! Mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni.
4 Pilato akatoka tena nje akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Yesu kwenu kuwajulisha kwamba mimi sikumwona ana hatia.” 5 Kwa hiyo Yesu akatoka nje akiwa amevaa ile taji ya miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, huyu hapa huyo mtu!”
6 Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”
Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulubishe, mimi sioni hatia juu yake.”
7 Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu.”
8 Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi. 9 Akaingia tena ndani ya jumba la kifalme, akamuuliza Yesu, “Wewe umetoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu. 10 Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?”
11 Ndipo Yesu akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”
12 Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Yesu, lakini Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.”
13 Pilato aliposikia maneno haya akamtoa Yesu nje tena akaketi katika kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe, kwa Kiebrania paliitwa Gabatha 14 Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi.
Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”
15 Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!”
Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?”
Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.”
16 Ndipo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili wamsulubishe.
Kwa hiyo askari wakamchukua Yesu.