Majuto na Kujiua kwa Yuda Msaliti

Hekaluni na mahali nje ya kuta za Yerusalemu. Ijumaa asubuhi

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 27:3–10

27:3 Yuda, ambaye alikuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 4 Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”

Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”

5 Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.

6 Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” 7 Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. 8 Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. 9 Ndipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli, 10 wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.”

Yesu Mbele ya Pilato kwa Mara ya Kwanza

Yerusalemu. Ijumaa, asubuhi na mapema

Mathayo 27:2, 11–14

27:2 Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala wa Kirumi.

11 Wakati huo Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.”

12 Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno.

13 Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?”

14 Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.

Marko 15:2–5

15:2 Pilato akamuuliza, “Je, wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu, “Wewe umesema.”

3 Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi.

4 Pilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.”

5 Lakini Yesu hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa.

Luka 23:1–5

23:1 Kisha umati wote wa watu ukainuka na kumpeleka Yesu kwa Pilato. 2 Nao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita kuwa yeye ni Kristo, mfalme.”

3 Basi Pilato akamuuliza Yesu, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akajibu, “Wewe wasema.”

4 Pilato akawaambia viongozi wa makuhani na watu wote waliokuwepo, “Sioni sababu ya kutosha kumshtaki mtu huyu!”

5 Lakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Uyahudi yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!”

Yohana 18:28–38

18:28 Ndipo Wayahudi wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala wa Kirumi. Wakati huo ilikuwa ni alfajiri, ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani kwa sababu ya sheria za Kiyahudi. Wangehesabiwa kuwa najisi kama wangeingia nyumbani mwa mtu asiye Myahudi na wasingeruhusiwa kushiriki katika Sikukuu ya Pasaka. 29 Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?”

30 Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu tusingemleta kwako.”

31 Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.”

Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu yeyote.” 32 Walisema hivyo ili yale maneno aliyosema Yesu kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia.

33 Kwa hiyo Pilato akaingia ndani ya jumba la kifalme, akamwita Yesu, akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

34 Yesu akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe, au uliambiwa na watu kunihusu mimi?”

35 Pilato akamjibu, “Mimi si Myahudi, ama sivyo? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?”

36 Yesu akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo, ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”

37 Pilato akamuuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Mtu yeyote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”

38 Pilato akamuuliza Yesu, “Kweli ni nini?” Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Yesu, “Sioni kosa lolote alilotenda mtu huyu.

Yesu Mbele ya Herode Antipa, Mtawala wa Robo ya Nchi

Yerusalemu. Ijumaa, asubuhi na mapema

Luka 23:6–12

23:6 Pilato aliposikia hayo akauliza, “Huyu mtu ni Mgalilaya?” 7 Alipofahamu kwamba Yesu alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu.

8 Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu yeye. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha. 9 Herode akamuuliza maswali mengi, lakini Yesu hakumjibu lolote. 10 Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwepo wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana. 11 Herode na askari wake wakamdhihaki Yesu na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato. 12 Siku hiyo, Herode na Pilato wakawa marafiki; kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao.