Yesu Anamtokea Maria Magdalene

Yesu anamtokea Maria Magdalene na kumpa ujumbe kwa wanafunzi.

Inaelezwa kwamba alionekana mara tano siku ya ufufuo wake, na mara nyingine tano baadaye, katika kipindi cha siku arobaini. Siku hiyo alionekana mara tano kwa watu hawa: (1) Maria Magdalene (Yohana na Marko); (2) wale wanawake wengine (Mathayo); (3) wale wawili waliokuwa wakienda Emau; (4) Simoni Petro (Luka 24:34); (5) mitume kumi na watu wengine.

Yerusalemu. Siku ya kwanza ya juma (Jumapili)

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Marko 16:9–11

16:9 Yesu alipofufuka alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma alimtokea kwanza Maria Magdalene, yule ambaye alikuwa amemtoa pepo wachafu saba.

10 Maria akaenda, naye akawaambia wale waliokuwa wamefuatana na Yesu, waliokuwa wanaomboleza na kulia. 11 Lakini waliposikia kwamba Yesu yu hai na kwamba Maria alikuwa amemwona, hawakusadiki.

Yohana 20:11–18

20:11 Lakini Maria Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama, kuchungulia mle kaburini, 12 naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.

13 Wakamuuliza Maria, “Mwanamke, mbona unalia?”

Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu na sijui walikomweka.”

14 Baada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Yesu amesimama, lakini hakumtambua.

15 Yesu akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?”

Maria akidhani ya kuwa aliyekuwa anaongea naye ni mtunza bustani, kwa hiyo akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nionyeshe ulikomweka, nami nitamchukua.”

16 Yesu akamwita, “Maria!”

Ndipo Maria akamgeukia Yesu na kusema naye kwa Kiebrania, “Rabboni!” (maana yake Mwalimu).

17 Yesu akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”

18 Kwa hiyo Maria Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Yesu, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Yesu alikuwa amemweleza mambo hayo yote.

Yesu Anawatokea Wanawake Wengine

Yerusalemu. Jumapili, siku ya kwanza ya juma

Mathayo 28:9–10

28:9 Ghafula, Yesu akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. 10 Ndipo Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”

Baadhi ya Walinzi Wanawapa Habari Viongozi wa Wayahudi

Mathayo 28:11–15

28:11 Wakati wale wanawake walikuwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia. 12 Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kutunga hila, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha 13 wakiwaambia, “Inawapasa mseme, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’ 14 Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.” 15 Kwa hiyo wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi mpaka leo.

Yesu Anawatokea Wanafunzi Wawili Njiani Kwenda Emau

Yesu anawatokea wanafunzi wawili (Kleopa na mwingine) njiani kwenda Emau.

Jumapili alasiri

Marko 16:12–13

16:12 Baadaye Yesu akawatokea wawili miongoni mwa wanafunzi wake walipokuwa wakienda shambani akiwa katika sura nyingine. 13 Nao wakarudi na kuwaambia wenzao. Lakini hawakuwasadiki wao pia.

Luka 24:13–32

24:13 Ikawa siku iyo hiyo, wanafunzi wawili wa Yesu walikuwa njiani wakienda kijiji kilichoitwa Emau, yapata maili saba kutoka Yerusalemu. 14 Walikuwa wakizungumza wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotukia. 15 Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akaja akatembea pamoja nao, 16 lakini macho yao yakazuiliwa ili wasimtambue.

17 Akawauliza, “Ni mambo gani haya mnayozungumza wakati mnatembea?”

Wakasimama, nyuso zao zikionyesha huzuni. 18 Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa, akamuuliza, “Je, wewe ndiye peke yako mgeni huku Yerusalemu ambaye hufahamu mambo yaliyotukia humo siku hizi?”

19 Akawauliza, “Mambo gani?”

Wakamjibu, “Mambo ya Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii, mwenye uwezo mkuu katika maneno yake na matendo yake, mbele za Mungu na mbele ya wanadamu wote. 20 Viongozi wa makuhani na viongozi wetu walimtoa ahukumiwe kufa, nao wakamsulubisha. 21 Lakini tulikuwa tumetegemea kwamba yeye ndiye angelikomboa Israeli. Zaidi ya hayo, leo ni siku ya tatu tangu mambo haya yatokee. 22 Isitoshe, baadhi ya wanawake katika kundi letu wametushtusha. Walikwenda kaburini leo alfajiri, 23 lakini hawakuukuta mwili wake. Walirudi wakasema wameona maono ya malaika ambao waliwaambia kwamba Yesu yu hai. 24 Kisha baadhi ya wenzetu walikwenda kaburini wakalikuta kama vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini yeye hawakumwona.”

25 Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga kiasi gani, nanyi ni wazito mioyoni mwenu kuamini mambo yote yaliyonenwa na manabii! 26 Je, haikumpasa Kristo kuteswa kwa njia hiyo na kisha aingie katika utukufu wake?” 27 Naye akianzia na Sheria ya Mose na Manabii wote, akawafafanulia jinsi Maandiko yalivyosema kumhusu yeye.

28 Nao walipokaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, Yesu akawa kama anaendelea mbele. 29 Lakini wao wakamsihi sana akae nao, wakisema, “Kaa hapa nasi, kwa maana sasa ni jioni na usiku unaingia.” Basi akaingia ndani kukaa nao.

30 Alipokuwa mezani pamoja nao, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akaanza kuwagawia. 31 Ndipo macho yao yakafumbuliwa, nao wakamtambua, naye akatoweka machoni pao. Hawakumwona tena. 32 Wakaulizana wao kwa wao, “Je, mioyo yetu haikuwakawaka kwa furaha ndani yetu alipokuwa anazungumza nasi njiani na kutufafanulia Maandiko?”