Wanafunzi Wawili Wanarudi Kutoa Habari
Taarifa ya wanafunzi wawili, na habari za kumtokea Simoni Petro.
Yerusalemu. Jumapili jioni
30 au 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Luka 24:33–35
24:33 Wakaondoka mara, wakarudi Yerusalemu. Wakawakuta wale wanafunzi kumi na mmoja na wale waliokuwa pamoja nao, wamekusanyika 34 wakisema, “Ni kweli! Bwana amefufuka, naye amemtokea Simoni.” 35 Kisha wale wanafunzi wawili wakaeleza yaliyotukia njiani na jinsi walivyomtambua Yesu alipoumega mkate.
Yesu Anawatokea Wanafunzi Bila Tomaso Kuwepo
Yesu anawatokea wanafunzi walioshangaa (Tomaso hayupo) na kuwapa agizo la utume. Wanashindwa kumshawishi Tomaso.
Yerusalemu. Jumapili jioni
Marko 16:14
16:14 Baadaye Yesu akawatokea wale wanafunzi kumi na mmoja walipokuwa wakila chakula. Akawakemea kwa kutoamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao kwa kutosadiki wale waliomwona baada yake kufufuka.
Luka 24:36–43
24:36 Walipokuwa bado wanazungumza hayo, Yesu mwenyewe akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!”
37 Wakashtuka na kuogopa wakidhani kwamba wameona mzuka. 38 Lakini Yesu akawauliza, “Kwa nini mnaogopa? Kwa nini mna shaka mioyoni mwenu?
39 Tazameni mikono yangu na miguu yangu, mwone kuwa ni mimi hasa. Niguseni mwone; kwa maana mzuka hauna nyama na mifupa, kama mnionavyo kuwa navyo.”
40 Aliposema haya, akawaonyesha mikono na miguu yake. 41 Wakashindwa kuamini kwa ajili ya furaha na mshangao waliokuwa nao. Akawauliza, “Mna chakula chochote hapa?”
42 Wakampa kipande cha samaki aliyeokwa, 43 naye akakichukua na kukila mbele yao.
Yohana 20:19–25
20:19 Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi. Naye Yesu aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!”
20 Baada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana.
21 Yesu akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22 Naye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23 Mkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa, na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”
24 Lakini Tomaso, aliyeitwa Didimasi, yaani Pacha, mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Yesu alipokuja. 25 Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.”
Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake, na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”
Yesu Anatokea Tena na Tomaso Anasadiki
Yesu anawatokea wanafunzi usiku wa Jumapili inayofuata, na Tomaso anasadiki.
Yerusalemu
Yohana 20:26–31
20:26 Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomaso alikuwa pamoja nao. Ndipo Yesu akaja milango ikiwa imefungwa na kusimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.” 27 Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyoosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”
28 Tomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”
29 Yesu akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”
30 Yesu alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. 31 Lakini haya yameandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu, na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.