Yesu Anawatokea Wanafunzi Saba Kando ya Bahari ya Galilaya
Yesu anawatokea wanafunzi saba kando ya Bahari ya Galilaya. Kuvuliwa kwa samaki kwa muujiza.
30 au 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Yohana 21:1–25
21:1 Baada ya haya Yesu akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia. Yeye alijionyesha kwao hivi: 2 Simoni Petro, Tomaso aitwaye Didimasi, yaani Pacha, Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja. 3 Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi naenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutakwenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata chochote.
4 Mara baada ya kupambazuka, Yesu akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Yesu.
5 Yesu akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wowote?”
Wakamjibu, “La.”
6 Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu na tazama wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.
7 Yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia haya, akajifunga nguo yake kwa kuwa alikuwa uchi, naye akajitosa baharini. 8 Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliyojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa 200 9 Walipofika ufuoni, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake na mikate.
10 Yesu akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”
11 Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu pwani. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa 153. Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika. 12 Yesu akawaambia, “Njooni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wa wanafunzi aliyethubutu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Kwa sababu walijua ya kuwa ni Bwana. 13 Yesu akaja, akachukua ule mkate, akawapa na vivyo hivyo akawagawia pia wale samaki. 14 Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada yake kufufuliwa kutoka kwa wafu.
15 Walipokwisha kula, Yesu akamuuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?”
Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”
Yesu akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”
16 Yesu akamwambia tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?”
Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”
Yesu akamwambia, “Chunga kondoo zangu.”
17 Kwa mara ya tatu Yesu akamuuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akahuzunika sana kwa kuwa Yesu alimuuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.”
Yesu akamwambia, “Lisha kondoo wangu. 18 Amin, amin nakuambia, ulipokuwa kijana ulivaa na kwenda unakotaka, lakini utakapokuwa mzee utanyoosha mikono yako na mtu mwingine atakuvika na kukupeleka usipotaka kwenda.” 19 Yesu alisema haya ili kuashiria ni kifo cha aina gani Petro atakachomtukuza nacho Mungu. Kisha Yesu akamwambia Petro, “Nifuate!”
20 Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Yesu walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”) 21 Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamuuliza Yesu, “Bwana na huyu je?”
22 Yesu akamjibu, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!” 23 Kwa sababu ya maneno haya ya Yesu, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi mpaka nitakaporudi, inakuhusu nini?”
24 Huyu ndiye yule mwanafunzi anayeshuhudia mambo haya na ndiye ambaye ameandika habari hizi. Nasi tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.
25 Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Yesu alifanya. Kama yote yangeliandikwa, nadhani hata ulimwengu wote usingekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu vyote ambavyo vingeandikwa. Amen.
Yesu Anawatokea Zaidi ya Watu Mia Tano huko Galilaya
Yesu anawatokea zaidi ya watu mia tano kwenye mlima ulioteuliwa huko Galilaya, na kutoa agizo la utume.
Mathayo 28:16–20
28:16 Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza. 17 Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
Marko 16:15–18
16:15 Akawaambia, “Enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 Yeyote aaminiye na kubatizwa ataokoka. Lakini yeyote asiyeamini atahukumiwa. 17 Nazo ishara hizi zitafuatana na wanaoamini: Kwa Jina langu watatoa pepo wachafu; watasema kwa lugha mpya; 18 watashika nyoka kwa mikono yao; na hata wakinywa kitu chochote cha kuua, hakitawadhuru kamwe; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona.”
Yesu Anawapa Wanafunzi Agizo Jingine la Utume
Yesu anawatokea wanafunzi na kuwapa agizo jingine la utume.
Yerusalemu
Luka 24:44–49
24:44 Akawaambia, “Haya ndiyo yale niliyowaambia nilipokuwa bado niko pamoja nanyi, kwamba yote yaliyoandikwa kunihusu mimi katika Sheria ya Mose, Manabii na Zaburi hayana budi kutimizwa.”
45 Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko. 46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. 48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
49 “Tazama nitawatumia ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini hadi mtakapovikwa uwezo utokao juu.”
Kujitokeza kwa Mwisho na Kupaa
Kwenye Mlima wa Mizeituni, kati ya Yerusalemu na Bethania
Marko 16:19–20
16:19 Baada ya Bwana Yesu kusema nao, alichukuliwa juu mbinguni na kuketi mkono wa kuume wa Mungu. 20 Kisha wanafunzi wake wakatoka, wakahubiri kila mahali, naye Bwana akatenda kazi pamoja nao na kulithibitisha neno lake kwa ishara zilizofuatana nalo.]
Luka 24:50–53
24:50 Akiisha kuwaongoza mpaka kwenye viunga vya Bethania, akainua mikono yake juu na kuwabariki.
51 Alipokuwa anawabariki, akawaacha, akachukuliwa mbinguni. 52 Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu. 53 Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu. Amen.