Matendo hadi Ufunuo
Sehemu ya 1: Injili Inahubiriwa kwa Wayahudi Pekee
Tangu kupaa kwa Kristo hadi mwisho wa kipindi ambacho injili ilihubiriwa kwa waongofu wa haki na kwa Wayahudi pekee.
Mitume Wanarudi Yerusalemu
Baada ya kupaa kwa Kristo, mitume wanarudi Yerusalemu.
29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia, mpendwa Theofilo, kuhusu mambo yote Yesu aliyofanya na kufundisha tangu mwanzo, 2 hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maagizo kupitia kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. 3 Baada ya mateso yake, alijionyesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu Ufalme wa Mungu. 4 Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake. 5 Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
7 Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”
9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.
10 Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao, 11 wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”
12 Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato kutoka mjini. 13 Walipowasili mjini Yerusalemu, walikwenda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Wale waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Tomaso, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. 14 Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwepo wanawake kadha, na Maria mama yake Yesu, pamoja na ndugu zake Yesu.
Mathiya Anachaguliwa kwa Kura Kuchukua Nafasi ya Yuda
Mathiya anateuliwa kwa kura kuwa mtume badala ya Yuda.
15 Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao wote walikuwa watu wapatao 120), akasema, 16 “Ndugu zangu, ilibidi Andiko litimie ambalo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu. 17 Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”
18 (Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje. 19 Kila mtu Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu).
20 “Kama vile ilivyoandikwa katika kitabu cha Zaburi,
“ ‘Mahali pake na pawe ukiwa,
wala asiwepo yeyote atakayeishi humo,’
na,
“ ‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake ya uongozi.’
21 Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Yesu alipoingia na kutoka katikati yenu, 22 kuanzia ubatizo wa Yohana mpaka siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”
23 Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yosefu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya. 24 Kisha wakaomba, wakasema, “Bwana, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25 ili achukue nafasi ya huduma ya utume ambayo Yuda aliiacha ili aende mahali pake mwenyewe.” 26 Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.
Roho Mtakatifu Anakuja Siku ya Pentekoste
1 Siku ya Pentekoste ilipowadia, waamini wote walikuwa mahali pamoja. 2 Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali uliotoka mbinguni ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. 3 Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. 4 Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.
5 Basi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu. 6 Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. 7 Wakiwa wameshangaa na kustaajabu wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya? 8 Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa? 9 Wapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto na Asia, 10 Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene na wageni kutoka Rumi, 11 Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.” 12 Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”
13 Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa divai!”