Hekalu la Yerusalemu Linateketezwa (continued)

588 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Zaburi 74

Utenzi wa Asafu.

1 Ee Mungu, mbona umetukataa milele?

Mbona hasira yako inatoka moshi

juu ya kondoo wa malisho yako?

2 Kumbuka watu uliowanunua zamani,

kabila la urithi wako, ambao uliwakomboa:

Mlima Sayuni, ambamo uliishi.

3 Geuza hatua zako kuelekea magofu haya ya kudumu,

uharibifu wote huu ambao adui ameuleta pale patakatifu.

4 Adui zako wamenguruma pale ulipokutana nasi,

wanaweka bendera zao kama alama.

5 Walifanya kama watu wanaotumia mashoka

kukata kichaka cha miti.

6 Walivunjavunja milango yote iliyonakshiwa

kwa mashoka na vishoka vyao.

7 Waliteketeza kabisa mahali pako patakatifu,

wakayanajisi makao ya Jina lako.

8 Walisema mioyoni mwao,

“Tutawaponda kabisa!”

Walichoma kila mahali ambapo Mungu

aliabudiwa katika nchi.

9 Hatukupewa ishara za miujiza;

hakuna manabii waliobaki,

hakuna yeyote kati yetu ajuaye

hali hii itachukua muda gani.

10 Ee Mungu, mtesi atakudhihaki mpaka lini?

Je, adui watalitukana jina lako milele?

11 Kwa nini unazuia mkono wako,

mkono wako wa kuume?

Uutoe kutoka makunjo ya vazi lako

na uwaangamize!

12 Lakini wewe, Ee Mungu, ni mfalme wangu tangu zamani,

unaleta wokovu duniani.

13 Ni wewe uliyeigawanya bahari kwa uweza wako;

ulivunja vichwa vya wanyama wakubwa wa kutisha katika maji.

14 Ni wewe uliyeponda vichwa vya Lewiathani

nawe ukamtoa kama chakula

kwa viumbe vya jangwani.

15 Ni wewe uliyefungua chemchemi na vijito,

ulikausha mito ambayo ilikuwa ikitiririka daima.

16 Mchana ni wako, nao usiku ni wako pia,

uliziweka jua na mwezi.

17 Ni wewe uliyeiweka mipaka yote ya dunia,

ulifanya kiangazi na masika.

18 Ee Bwana, kumbuka jinsi mtesi alivyokudhihaki,

jinsi watu wapumbavu walivyolitukana jina lako.

19 Usiukabidhi uhai wa njiwa wako kwa wanyama wakali wa mwitu;

usisahau kabisa uhai wa watu wako wanaoteseka milele.

20 Likumbuke agano lako,

maana mara kwa mara mambo ya jeuri

yamejaa katika sehemu za giza nchini.

21 Usiruhusu walioonewa warudi nyuma kwa aibu;

maskini na wahitaji hebu walisifu jina lako.

22 Inuka, Ee Mungu, ujitetee;

kumbuka jinsi wapumbavu

wanavyokudhihaki mchana kutwa.

23 Usipuuze makelele ya watesi wako,

ghasia za adui zako, zinazoinuka mfululizo.

Zaburi 83

Wimbo. Zaburi ya Asafu.

1 Ee Mungu, usinyamaze kimya,

usinyamaze, Ee Mungu, usitulie.

2 Tazama watesi wako wanafanya fujo,

jinsi adui zako wanavyoinua vichwa vyao.

3 Kwa hila, wanafanya shauri dhidi ya watu wako,

wanafanya shauri baya dhidi ya wale unaowapenda.

4 Wanasema, “Njooni, tuwaangamize kama taifa,

ili jina la Israeli lisikumbukwe tena.”

5 Kwa nia moja wanapanga mashauri mabaya pamoja,

wanafanya muungano dhidi yako,

6 mahema ya Edomu na Waishmaeli,

ya Wamoabu na Wahagari,

7 Gebali, Amoni na Amaleki,

Ufilisti, pamoja na watu wa Tiro.

8 Hata Ashuru wameungana nao

kuwapa nguvu wazao wa Loti.

9 Uwatendee kama vile ulivyowatendea Midiani,

na kama vile ulivyowatendea Sisera na Yabini

hapo kijito cha Kishoni,

10 ambao waliangamia huko Endori

na wakawa kama takataka juu ya nchi.

11 Wafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu,

watawala wao kama Zeba na Salmuna,

12 ambao walisema, “Na tumiliki nchi

ya malisho ya Mungu.”

13 Ee Mungu wangu, wapeperushe kama mavumbi ya kisulisuli,

kama makapi yapeperushwayo na upepo.

14 Kama vile moto uteketezavyo msitu

au mwali wa moto unavyounguza milima,

15 wafuatilie kwa tufani yako

na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako.

16 Funika nyuso zao kwa aibu

ili watu walitafute jina lako, Ee Bwana.

17 Wao na waaibishwe na kufadhaishwa milele,

na waangamie kwa aibu.

18 Hebu wajue kwamba wewe, ambaye jina lako ni Bwana,

kwamba wewe peke yako ndiwe Uliye Juu Sana ya dunia yote.