Hekalu la Yerusalemu Linateketezwa (continued)

588 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Zaburi 94

1 Ee Bwana, ulipizaye kisasi,

Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa.

2 Ee Mhukumu wa dunia, inuka,

uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili.

3 Hata lini, waovu, Ee Bwana,

hata lini waovu watashangilia?

4 Wanamimina maneno ya kiburi,

watenda mabaya wote wamejaa majivuno.

5 Ee Bwana, wanawaponda watu wako,

wanawaonea urithi wako.

6 Wanamchinja mjane na mgeni,

na kuwaua yatima.

7 Nao husema, “Bwana haoni,

Mungu wa Yakobo hafahamu.”

8 Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu;

enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?

9 Je, aliyeweka sikio asisikie?

Aliyeumba jicho asione?

10 Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu?

Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?

11 Bwana anajua mawazo ya mwanadamu;

anajua kwamba ni ubatili.

12 Ee Bwana, heri mtu anayeadhibishwa na wewe,

mtu unayemfundisha kwa sheria yako,

13 unampa utulivu siku za shida,

mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa

kwa ajili ya mwovu.

14 Kwa kuwa Bwana hatawakataa watu wake,

hatauacha urithi wake.

15 Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki,

wote walio na mioyo minyofu wataifuata.

16 Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu?

Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu?

17 Kama Bwana asingelinisaidia upesi,

ningelikuwa ninaishi katika ukimya wa kifo.

18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”

Ee Bwana, upendo wako ulinishikilia.

19 Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,

faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.

20 Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe,

ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?

21 Huungana kuwashambulia wenye haki,

kuwahukumu kufa wasio na hatia.

22 Lakini Bwana amekuwa ngome yangu,

na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia.

23 Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao

na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao;

Bwana Mungu wetu atawaangamiza.

2 Wafalme 24:17–20

17 Akamfanya Matania, ndugu wa baba yake Yehoyakini, kuwa mfalme mahali pake, na akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia.

18 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, kutoka Libna. 19 Alifanya maovu machoni pa Bwana, kama alivyofanya Yehoyakimu. 20 Ilikuwa ni kwa sababu ya hasira ya Bwana haya yote yalitokea Yerusalemu na Yuda, naye mwishoni akawaondoa mbele zake.

Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.

Yeremia 52:4

4 Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Wakapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka mji pande zote.

Yeremia 39:2

2 Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne wa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia, ukuta wa mji ulibomolewa.

Yeremia 39:4–9

4 Mfalme Sedekia wa Yuda na askari wote walipowaona, wakakimbia na kuondoka mjini usiku kwa njia ya bustani ya mfalme, kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili, wakaelekea Araba.

5 Lakini jeshi la Wakaldayo likawafuatia na kumpata Sedekia katika sehemu tambarare za Yeriko. Wakamkamata na kumpeleka kwa Nebukadneza mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mahali ambapo alimtangazia hukumu. 6 Huko Ribla, mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake, na pia akawaua wakuu wote wa Yuda. 7 Kisha akayangʼoa macho ya Sedekia na kumfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.

8 Jeshi la Wakaldayo likachoma moto jumba la kifalme na nyumba za watu, na kuzibomoa kuta za Yerusalemu. 9 Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme akawachukua na kuwapeleka uhamishoni Babeli watu waliokuwa wamebaki ndani ya mji, pamoja na wale waliokuwa wamejisalimisha kwake, na watu wengine wote.

2 Wafalme 25:3–21

3 Ilipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu. 4 Kisha ukuta wa mji ukavunjwa, na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba. 5 Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia mfalme na kumpata katika sehemu tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika, 6 naye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, mahali ambapo hukumu yake ilitangazwa. 7 Wakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Kisha wakayangʼoa macho yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.

8 Mnamo siku ya saba ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi wa mfalme, afisa wa mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu. 9 Alichoma moto Hekalu la Bwana, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu. 10 Jeshi lote la Wakaldayo, chini ya jemadari wa askari walinzi wa mfalme, walivunja kuta zilizoizunguka Yerusalemu. 11 Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi akawapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli. 12 Lakini yule jemadari wa askari walinzi akawaacha baadhi ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.

13 Wakaldayo walivunja vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Bwana. Hivyo wakaichukua hiyo shaba na kuipeleka Babeli. 14 Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu. 15 Jemadari wa askari walinzi wa mfalme akachukua vile vyetezo na yale mabakuli ya kunyunyizia, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.

16 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Solomoni alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Bwana, ilikuwa na uzito usioweza kupimika. 17 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane. Sehemu ya shaba juu ya nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tatu na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na wavu wake ilifanana na hiyo ya kwanza.

18 Yule jemadari wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu. 19 Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji, na washauri watano wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji. 20 Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla. 21 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe.

Hivyo Yuda wakaenda utumwani, mbali na nchi yao.