Yerusalemu Inatekwa na Sedekia Anakamatwa; Yeremia Anaachiliwa Huru

588 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yeremia 52:5–6

5 Mji ulizungukwa na jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia.

6 Ilipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu.

Yeremia 39:3

3 Kisha maafisa wote wa mfalme wa Babeli wakaja na kuketi kwenye Lango la Kati, nao ni: Nergal-Shareza wa Samgari, Nebo-Sarsekimu afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa mwenye cheo cha juu, na maafisa wengine wote wa mfalme wa Babeli.

Yeremia 52:7–11

7 Kisha ukuta wa mji ukavunjwa na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba. 8 Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia Mfalme Sedekia na kumpata katika sehemu tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika, 9 naye akakamatwa.

Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mahali ambapo alimtangazia hukumu. 10 Huko Ribla mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Pia akawaua maafisa wote wa Yuda. 11 Kisha akayangʼoa macho ya Sedekia, akamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli, alipomweka gerezani mpaka siku ya kifo chake.

Yeremia 39:11–14

11 Basi, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuwa ametoa maagizo kuhusu Yeremia kupitia Nebuzaradani kiongozi wa walinzi wa mfalme akisema: 12 “Mchukue umtunze. Usimdhuru, lakini umfanyie chochote anachotaka.” 13 Basi Nebuzaradani kiongozi wa walinzi, Nebushazbani afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa wa cheo cha juu, na maafisa wengine wote wa mfalme wa Babeli 14 wakatuma watu kumwondoa Yeremia kutoka ua wa walinzi. Wakamkabidhi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ili amrudishe nyumbani kwake. Kwa hiyo akabaki miongoni mwa watu wake mwenyewe.

Yeremia 52:24–27

24 Yule jemadari wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu. 25 Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji, na washauri saba wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji. 26 Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla. 27 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe.

Hivyo Yuda wakaenda utumwani, mbali na nchi yao.

Hekalu la Yerusalemu Linateketezwa

Yeremia 52:12–14

12 Mnamo siku ya kumi ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi wa mfalme, aliyemtumikia mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu. 13 Alichoma moto Hekalu la Bwana, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu. 14 Jeshi lote la Wakaldayo chini ya jemadari wa askari walinzi wa mfalme walivunja kuta zote zilizoizunguka Yerusalemu.

Yeremia 52:17–23

17 Wakaldayo walivunja vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Bwana. Hivyo wakaichukua hiyo shaba yote na kuipeleka Babeli. 18 Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu. 19 Jemadari wa askari walinzi wa mfalme akachukua yale masinia, vile vyetezo, yale mabakuli ya kunyunyizia, zile sufuria, vile vinara vya taa, zile sahani na yale mabakuli yaliyotumika kwa sadaka za vinywaji, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.

20 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na wale mafahali kumi na mawili wa shaba waliokuwa chini yake, pamoja na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Mfalme Solomoni alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Bwana, ilikuwa na uzito usioweza kupimika. 21 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, kimo chake na mzunguko dhiraa kumi na mbili, na unene wa nyanda nne, na zote zilikuwa wazi ndani. 22 Sehemu ya shaba juu ya ile nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tano, na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na makomamanga yake ilifanana na hiyo ya kwanza. 23 Kulikuwa na makomamanga tisini na sita pembeni; jumla ya makomamanga juu ya wavu uliokuwa umezunguka yalikuwa mia moja.

Yeremia 52:15–16

15 Nebuzaradani, jemadari wa askari walinzi, akawapeleka uhamishoni baadhi ya watu maskini sana na wale waliobaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli. 16 Lakini Nebuzaradani akawaacha mabaki ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.

Yeremia 39:10

10 Lakini Nebuzaradani kiongozi wa walinzi aliwabakiza baadhi ya watu maskini katika nchi ya Yuda, ambao hawakuwa na kitu. Naye wakati huo akawapa mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.

Zaburi 79

Zaburi ya Asafu.

1 Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako,

wamelinajisi Hekalu lako takatifu,

wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.

2 Wametoa maiti za watumishi

kuwa chakula cha ndege wa angani

na nyama ya watakatifu wako

kwa wanyama wa nchi.

3 Wamemwaga damu kama maji

kuzunguka Yerusalemu yote,

wala hakuna yeyote wa kuwazika.

4 Tumekuwa kitu cha aibu kwa jirani zetu,

cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka.

5 Hata lini, Ee Bwana? Je, wewe utakasirika milele?

Wivu wako utawaka kama moto hadi lini?

6 Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali,

juu ya falme za hao wasioliitia jina lako,

7 kwa maana wamemrarua Yakobo

na kuharibu nchi ya makao yake.

8 Usituhesabie dhambi za baba zetu,

huruma yako na itujie hima,

kwa maana tu wahitaji mno.

9 Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie,

kwa ajili ya utukufu wa jina lako;

tuokoe na kutusamehe dhambi zetu

kwa ajili ya jina lako.

10 Kwa nini mataifa waseme,

“Yuko wapi Mungu wenu?”

Mbele ya macho yetu,

dhihirisha kati ya mataifa

kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa

ya watumishi wako.

11 Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako;

kwa nguvu za mkono wako

hifadhi wale waliohukumiwa kufa.

12 Walipize jirani zetu mara saba vifuani mwao

aibu walizovurumisha juu yako, Ee Bwana.

13 Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako,

tutakusifu milele;

toka kizazi hadi kizazi

tutasimulia sifa zako.