Simulizi la Ruthu (continued)
1245 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Kisha Naomi akamwambia mkwewe, “Binti yangu, je, nisingelikutafutia pumziko ambako utatunzika vyema? 2 Je, Boazi, ambaye umekuwa pamoja na watumishi wake wasichana, si jamaa yetu wa karibu? Usiku wa leo atakuwa anapepeta ngano kwenye sakafu ya kupuria. 3 Basi oga na ukajipake marashi, ujivalie nguo zako nzuri. Kisha uende kwenye sakafu ya kupuria, lakini angalia asijue kwamba upo pale mpaka atakapomaliza kula na kunywa. 4 Atakapokwenda kulala, angalia mahali atakapolala. Kisha uende ufunue miguu yake, ulale. Naye atakuambia utakalofanya.”
5 Ruthu akajibu, “Lolote usemalo nitatenda.” 6 Basi akashuka mpaka kwenye sakafu ya kupuria, akafanya kila kitu mama mkwe wake alichomwambia kufanya.
7 Wakati Boazi alipomaliza kula na kunywa, naye akawa amejawa na furaha, alikwenda kulala mwisho wa lundo la nafaka. Ruthu akanyemelea polepole, akafunua miguu yake, na akalala. 8 Usiku wa manane, kitu kilimshtua Boazi, akajigeuza, akagundua yupo mwanamke amelala miguuni pake.
9 Akauliza, “Wewe ni nani?”
Akajibu, “Ni mimi Ruthu, mjakazi wako. Uitande nguo yako juu yangu, kwa sababu wewe ndiwe jamaa wa karibu wa kutukomboa.”
10 Akamwambia, “Binti yangu, ubarikiwe na Bwana. Wema huu wa sasa ni mkuu kushinda hata ule ulioonyesha mwanzoni. Hukuwakimbilia vijana, wakiwa matajiri au maskini. 11 Sasa, binti yangu, usiogope. Nitakufanyia yote uliyoomba. Kwa maana mji wote wa watu wangu wanakujua ya kwamba wewe ni mwanamke mwenye tabia nzuri. 12 Ingawa ni kweli kwamba mimi ndiye jamaa aliye karibu, bado kuna mtu mwingine wa jamaa aliye karibu zaidi wa kukomboa kuliko mimi. 13 Wewe kaa hapa usiku huu, kisha asubuhi kama akikubali kukomboa, vyema na akomboe. La sivyo kama hayuko tayari, hakika kama Bwana aishivyo nitafanya hivyo. Lala hapa mpaka asubuhi.”
14 Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake mpaka asubuhi, akaondoka mapema pasipo mtu kuweza kumtambua mwenzake, maana Boazi alisema, “Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika kwenye sakafu ya kupuria.”
15 Pia akamwambia, “Leta shela yako uliyoivaa, uitandaze.” Naye alipoitandaza, akamimina vipimo sita vya shayiri, akamtwika. Kisha Ruthu akarudi zake mjini.
16 Basi Ruthu alipofika kwa mama mkwe wake Naomi, akamuuliza, “Je, binti yangu, ilikuwaje huko?”
Ndipo akamwelezea kila kitu Boazi alichomfanyia. 17 Akaendelea kusema, “Amenipa shayiri vipimo sita akisema, ‘Usiende kwa mama mkwe wako mikono mitupu.’ ”
18 Kisha Naomi akasema, “Subiri binti yangu, mpaka utakapojua kwamba hili jambo limekwendaje. Kwa sababu mtu huyu hatatulia mpaka akamilishe jambo hili leo.”
4:1 Boazi akakwea mpaka kwenye lango la mji, akaketi pale. Yule mtu wa jamaa aliyekuwa wa karibu wa kukomboa, ambaye Boazi alimtaja, akaja. Boazi akasema, “Njoo hapa, rafiki yangu. Karibu uketi.” Naye akakaribia, akaketi.
2 Boazi akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, “Ketini hapa.” Nao wakaketi. 3 Kisha akamwambia yule jamaa wa karibu wa kukomboa, “Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi iliyokuwa mali ya ndugu yetu Elimeleki. 4 Nami niliwaza nikujulishe wewe na kukuambia uinunue mbele ya hawa waliopo hapa, na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya fanya hivyo. Lakini kama hutaikomboa, uniambie, ili nijue. Kwa kuwa hakuna mtu mwingine mwenye haki ya kuikomboa ila wewe na baada yako ni mimi.”
Naye akasema, “Nitaikomboa mimi.”
5 Ndipo Boazi akasema “Siku utakaponunua hiyo ardhi kutoka kwa Naomi na Ruthu, Mmoabu, itakubidi kumchukua pia huyo mjane, ili kudumisha jina la marehemu pamoja na mali yake.”
6 Aliposikia hili, yule jamaa wa karibu wa kukomboa akasema, “Basi mimi sitaweza kuikomboa, kwa sababu inaonekana nitauhatarisha urithi wangu. Wewe ikomboe mwenyewe. Mimi sitaweza.”
7 (Basi katika siku za kale huko Israeli, ili kukamilisha tendo la kukomboa na kukabidhiana mali, mmoja huvua kiatu chake na kumpatia mwingine. Hii ilikuwa ni njia ya kuhalalisha mabadilishano katika Israeli.)
8 Basi yule jamaa wa karibu wa kukomboa akamwambia Boazi, “Wewe inunue mwenyewe.” Naye huyo jamaa akavua kiatu chake.
9 Kisha Boazi akawatangazia wazee na watu wote waliokuwepo, “Leo ninyi ni mashahidi kwamba mimi nimenunua kutoka kwa Naomi yote yaliyokuwa mali ya Elimeleki, Kilioni na Maloni. 10 Nimemchukua pia Ruthu, Mmoabu, mjane wa Maloni, awe mke wangu, ili kuendeleza jina la marehemu pamoja na mali zake, ili jina lake marehemu lisitoweke miongoni mwa jamaa yake, wala katika kumbukumbu za mji wake. Leo hivi ninyi ni mashahidi!”
11 Kisha wazee pamoja na watu wote waliokuwa langoni wakasema, “Sisi ni mashahidi. Bwana na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wanawake wawili ambao pamoja waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrathi na uwe mashuhuri katika Bethlehemu. 12 Kupitia kwa watoto ambao Bwana atakupa kutokana na huyu mwanamwali, jamaa yako na ifanane na ya Peresi, ambaye Tamari alimzalia Yuda.”
13 Basi Boazi akamwoa Ruthu, naye akawa mke wake. Alipoingia kwake, Bwana akamjalia Ruthu, naye akapata mimba, akamzaa mtoto wa kiume. 14 Wanawake wakamwambia Naomi: “Ahimidiwe Bwana, asiyekuacha bila kuwa na jamaa wa karibu wa kukomboa. Na awe mashuhuri katika Israeli yote! 15 Atakurejeshea uhai wako na kukuangalia katika siku za uzee wako. Kwa maana mkweo ambaye anakupenda, na ambaye kwako ni bora zaidi ya watoto wa kiume saba, ndiye alimzaa.”
16 Basi Naomi akamchukua yule mtoto, akampakata na akawa mlezi wake. 17 Wanawake waliokuwa jirani zake wakasema, “Naomi ana mtoto wa kiume.” Wakamwita jina lake Obedi. Yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi.
18 Hivi ndivyo vizazi vya Peresi:
Peresi alimzaa Hesroni,
19 Hesroni akamzaa Ramu,
Ramu akamzaa Aminadabu,
20 Aminadabu akamzaa Nashoni,
Nashoni akamzaa Salmoni,
21 Salmoni akamzaa Boazi,
Boazi akamzaa Obedi,
22 Obedi akamzaa Yese,
na Yese akamzaa Daudi.