Gideoni anaihukumu Israeli

1245 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Waamuzi 6:7–7:25

7 Waisraeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Wamidiani, 8 Bwana akawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa. 9 Nikawanyakua kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu nami nikawapa ninyi nchi yao. 10 Nikawaambia, ‘Mimi ndimi Bwana Mungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambayo mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.”

11 Malaika wa Bwana akaja akaketi chini ya mti wa mwaloni huko Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi, Mwabiezeri, ambako Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione. 12 Malaika wa Bwana alipomtokea Gideoni, akamwambia, “Bwana yu pamoja nawe, Ewe shujaa mwenye nguvu.”

13 Gideoni akajibu, “Ee Bwana wangu, kama Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi basi yale matendo yake makuu baba zetu waliyotusimulia juu yake waliposema, ‘Je, Bwana hakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasa Bwana ametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.”

14 Bwana akamgeukia na kusema “Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?”

15 Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.”

16 Bwana akamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.”

17 Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonyesha kweli kwamba ni wewe unayesema nami. 18 Tafadhali ninakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea sadaka yangu na kuiweka mbele yako.”

Naye Bwana akamwambia, “Nitangoja mpaka utakaporudi.”

19 Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mti wa mwaloni na kumpa.

20 Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo. 21 Malaika wa Bwana akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa Bwana akatoweka kutoka machoni pake. 22 Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa Bwana, akapiga kelele kwa mshangao, akasema, “Ole wangu, Bwana Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Bwana uso kwa uso!”

23 Lakini Bwana akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”

24 Hivyo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu mahali pale na kupaita, Yehova-Shalom. Mpaka leo ingalipo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.

25 Usiku ule ule Bwana akamwambia, “Mchukue ngʼombe dume wa baba yako, yaani, yule wa pili mwenye miaka saba, na ubomoe madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate Ashera iliyo karibu nayo. 26 Kisha mjengee Bwana Mungu wako, madhabahu halisi, kwa taratibu zake, juu ya huu mwamba. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.”

27 Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kama Bwana alivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana.

28 Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa na yule ngʼombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu yaliyojengwa upya!

29 Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?”

Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye alitenda hivi.”

30 Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”

31 Lakini Yoashi akauambia ule umati uliokuwa umezunguka ukiwa kinyume naye, “Je, ninyi mtamtetea Baali? Mnajaribu kumwokoa? Yeyote mwenye kumpigania atauawa kufikia kesho asubuhi! Kama Baali ni mungu kweli, anaweza kujitetea mwenyewe wakati mtu anapobomoa madhabahu yake.” 32 Basi siku ile wakamwita Gideoni “Yerub-Baali,” yaani, “Baali na ashindane naye,” kwa sababu alibomoa madhabahu yake.

33 Basi Wamidiani wote, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki wakaunganisha majeshi yao, wakavuka ngʼambo ya Yordani na kupiga kambi katika Bonde la Yezreeli. 34 Ndipo Roho wa Bwana akamjia Gideoni, akapiga tarumbeta, akiwaita Waabiezeri ili wamfuate. 35 Akatuma wajumbe waende katika Manase yote, akiwataka wachukue silaha na pia katika Asheri, Zabuloni na Naftali, nao wakakwea ili kukutana nao.

36 Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi: 37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo kwenye kiwanja cha kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya ngozi tu, nayo ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.” 38 Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akaikamua ile ngozi, umande ukatoka, maji ya kujaa bakuli.

39 Kisha Gideoni akamwambia Bwana, “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa ngozi hii. Wakati huu uifanye ngozi hii kavu na ardhi yote ifunikwe na umande.” 40 Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Ngozi ile ilikuwa kavu, nayo ardhi yote ikafunikwa na umande.

7:1 Ndipo Yerub-Baali (yaani Gideoni) na lile jeshi lililokuwa pamoja naye, wakaondoka asubuhi na mapema na kupiga kambi kando ya chemchemi ya Harodi. Kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini yao katika bonde karibu na kilima cha More. 2 Bwana akamwambia Gideoni, “Jeshi lililo pamoja nawe ni kubwa sana kwa mimi kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Ili kwamba Israeli asije akajisifu juu yangu akisema, ‘Mkono wangu ndio ulioniokoa, 3 kwa hiyo sasa tangaza jeshi lote likiwa linasikia, kwamba: Yeyote anayeogopa na kutetemeka, yeye na arudi nyumbani, aondoke katika Mlima Gileadi.’ ” Hivyo watu 22,000 walirudi, wakabaki 10,000.

4 Lakini Bwana akamwambia Gideoni, “Idadi ya jeshi bado ni kubwa. Wapeleke chini katika maji nami nitawajaribu huko kwa ajili yako. Kama nikikuambia, ‘Huyu atakwenda pamoja nawe,’ yeye atakwenda; lakini kama nikisema, ‘Huyu hatakwenda pamoja nawe,’ yeye hatakwenda.”

5 Hivyo Gideoni akalileta lile jeshi chini kwenye maji naye Bwana akamwambia Gideoni, “Watenge upande mmoja wale wote wanywao maji kwa ulimi, kama vile mbwa anywavyo, wale wote wapigao magoti ili kunywa wakipeleka mikono yao vinywani mwao, waweke upande mwingine.” 6 Idadi ya wale waliokunywa kwa kuramba ramba walikuwa 300, lakini wengine wote katika jeshi walipiga magoti ili kunywa.

7 Bwana akamwambia Gideoni, “Kwa hao watu 300 walioramba maji nitawaokoa ninyi, nami nitawatia Wamidiani mkononi mwako. Waache hao watu wengine wote warudi kila mmoja nyumbani mwake.” 8 Hivyo Gideoni akawaacha wale Waisraeli wengine kila mmoja aende kwenye hema yake. Akabakia na wale 300, ambao walichukua vyakula na tarumbeta za wale wenzao.

Basi kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake bondeni. 9 Usiku ule ule Bwana akamwambia Gideoni, “Ondoka, ushuke kambini, kwa kuwa nimeitia mkononi mwako. 10 Lakini kama unaogopa kushambulia, shuka kambini pamoja na mtumishi wako Pura, 11 nawe sikiliza wanayosema. Hatimaye, utatiwa moyo kushambulia kambi.” Basi yeye na Pura mtumishi wake wakashuka na kufikia walinzi wa mbele wenye silaha waliokuwa mle kambini. 12 Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine yote ya mashariki walikaa bondeni, nao walikuwa mfano wa nzige kwa wingi wao. Ngamia zao hazikuhesabika, wingi wao ulikuwa kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.

13 Gideoni alifika wakati huo huo kukiwa na mtu mmoja aliyekuwa anamweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Niliota ndoto: Tazama mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi moja ya Wamidiani, ukaipiga na ikaanguka nao ukaipindua juu chini na hema ikaporomoka chini.”

14 Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine zaidi ya upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.”

15 Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akamwabudu Mungu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! Bwana amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.” 16 Akawagawa wale watu 300 katika makundi matatu, akawakabidhi tarumbeta mikononi mwao wote na mitungi isiyokuwa na maji yenye mienge ndani yake.

17 Akawaambia, “Nitazameni, fanyeni kama nitakavyofanya, nitakapofika mwisho wa kambi mfanye kama nitakavyofanya. 18 Wakati mimi na wale walio pamoja nami wote, tutakapopiga tarumbeta zetu, ninyi nanyi pigeni tarumbeta pande zote za kambi na mpige kelele, mseme, ‘Upanga wa Bwana na wa Gideoni.’ ”

19 Gideoni na wale watu 100 waliokuwa pamoja naye wakafika mwisho wa kambi usiku mwanzoni mwa zamu ya kati, mara tu walipokuwa wamebadili zamu. Wakapiga zile tarumbeta zao na kuvunja ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. 20 Yale makundi matatu yakapiga tarumbeta na kuvunja mitungi. Wakashika mienge kwa mikono yao ya kushoto na katika mikono yao ya kuume tarumbeta ili kuzipiga, wakapaza sauti zao, “Upanga wa Bwana na wa Gideoni!” 21 Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote, Wamidiani wote wakakimbia, huku wakipiga kelele.

22 Walipozipiga zile tarumbeta 300, Bwana akafanya watu katika kambi yote kugeuziana upanga kila mmoja na mwenziwe. Jeshi likakimbia mpaka Beth-Shita kuelekea Serera hadi mpakani mwa Abel-Mehola karibu na Tabathi. 23 Watu wa Israeli wakaitwa kutoka Naftali, Asheri na Manase, wakawafuatia Wamidiani. 24 Gideoni akatuma wajumbe katika nchi yote ya vilima vya Efraimu akisema, “Teremkeni dhidi ya Wamidiani na mkazuie vivuko vya maji mbele yao hadi Beth-Bara na pia Yordani.”

Hivyo watu wote wa Efraimu wakakutanika pamoja na kuzingira mto wa Yordani hadi Beth-Bara. 25 Wakawakamata wakuu wawili wa Midiani, Orebu na Zeebu. Wakamuulia Orebu pale penye mwamba wa Orebu, na Zeebu wakamuulia penye shinikizo la kukamulia divai la Zeebu. Wakawafuatia Wamidiani na kuleta vichwa vya Orebu na Zeebu kwa Gideoni, huko ngʼambo ya Yordani.