Midiani Inawafanya Waisraeli Watumwa
Waisraeli wa mashariki na kaskazini wanafanywa watumwa na Midiani, na Gideoni anakuwa mwamuzi.
1252 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele za Bwana, naye kwa miaka saba Bwana akawatia mikononi mwa Wamidiani. 2 Mkono wa Midiani ukawa na nguvu dhidi ya Israeli na kwa ajili ya Wamidiani, Waisraeli wakajitengenezea mahali pa kujificha milimani, kwenye mapango na ngome. 3 Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao. 4 Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe chochote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ngʼombe au punda. 5 Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia zao; wakavamia nchi ili kuiharibu. 6 Waisraeli wakafanywa kuwa maskini sana na Wamidiani, hata Israeli wakamlilia Bwana kuomba msaada.
Simulizi la Ruthu 1245 KK
1 Wakati Waamuzi walipotawala Israeli, kulikuwa na njaa katika nchi. Mtu mmoja kutoka nchi ya Bethlehemu ya Yuda, pamoja na mke wake na wanawe wawili, akaenda kuishi katika nchi ya Moabu. 2 Mtu huyu aliitwa Elimeleki, mkewe aliitwa Naomi, na hao wanawe wawili waliitwa Maloni na Kilioni. Walikuwa Waefrathi kutoka Bethlehemu ya Yuda. Wakaenda katika nchi ya Moabu, wakaishi huko.
3 Elimeleki mumewe Naomi akafa, hivyo Naomi akabaki na wanawe wawili. 4 Nao wakaoa wanawake Wamoabu, jina la mmoja aliitwa Orpa, na wa pili aliitwa Ruthu. Baada ya kama miaka kumi, 5 Maloni na Kilioni pia wakafa. Basi Naomi akabaki hana mume wala wanawe wawili.
6 Aliposikia akiwa huko Moabu kwamba Bwana amewasaidia watu wake kwa kuwapa chakula, Naomi na wakweze wakajiandaa kurudi nyumbani. 7 Yeye na wakweze wawili wakaondoka pale walipokuwa wakiishi na kushika njia kurudi nchi ya Yuda.
8 Ndipo Naomi akawaambia wale wakwe zake wawili, “Rudini, kila mmoja wenu nyumbani kwa mama yake. Bwana na awatendee fadhili kama mlivyowatendea hao waliofariki, na pia mimi. 9 Bwana na amjalie kila mmoja wenu maisha mema nyumbani kwa mume mwingine.”
Kisha akawabusu, nao wakalia kwa sauti kubwa, 10 wakamwambia, “Tutarudi pamoja na wewe nyumbani kwa watu wako.”
11 Lakini Naomi akasema, “Rudini nyumbani, binti zangu. Kwa nini mnifuate? Je, mimi nitaweza tena kuwa na wana wengine ambao wataweza kuwaoa ninyi? 12 Rudini nyumbani, binti zangu; mimi ni mzee kiasi kwamba siwezi kumpata mume mwingine. Hata kama ningefikiria kuwa bado kuna tumaini kwangu, hata kama ningekuwa na mume usiku huu na kuwazaa wana, 13 je, mngesubiri mpaka wakue? Mngebakia bila kuolewa mkiwasubiri? La, hasha, binti zangu. Nimepata uchungu kuliko ninyi, kwa sababu mkono wa Bwana umekuwa kinyume nami!”
14 Kisha wakalia tena kwa sauti. Orpa akambusu mama mkwe wake, akaenda zake, lakini Ruthu akaambatana naye.
15 Naomi akamwambia, “Tazama, mwenzako anarejea kwa watu wake na kwa miungu yake. Rudi pamoja naye.”
16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. 17 Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Bwana na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.” 18 Naomi alipotambua kwamba Ruthu amenuia kufuatana naye, hakuendelea kumsihi tena.
19 Kwa hiyo hao wanawake wawili wakaondoka, wakafika Bethlehemu. Walipofika Bethlehemu, mji mzima ulitaharuki, wanawake wakashangaa, wakasema, “Huyu aweza kuwa ni Naomi?”
20 Akawaambia, “Msiniite tena Naomi, niiteni Mara, kwa sababu Mwenyezi amenitendea mambo machungu sana. 21 Mimi niliondoka hali nimejaa, lakini Bwana amenirudisha mtupu. Kwa nini kuniita Naomi? Bwana amenitendea mambo machungu; Mwenyezi ameniletea msiba.”
22 Kwa hiyo Naomi alirudi pamoja na Ruthu Mmoabu mkwe wake, nao wakafika Bethlehemu mwanzoni mwa kuvuna shayiri.
2:1 Basi Naomi alikuwa na jamaa wa upande wa mume wake, kutoka ukoo wa Elimeleki, mtu maarufu ambaye aliitwa Boazi.
2 Ruthu, Mmoabu, akamwambia Naomi, “Nitakwenda mashambani nikaokote mabaki ya nafaka nyuma ya yule nitakayepata kibali machoni pake.”
Naomi akamwambia, “Nenda, binti yangu.” 3 Basi akaenda, akaokota mabaki ya nafaka mashambani nyuma ya wavunaji. Ikatokea kwamba alijikuta anafanya kazi kwenye shamba lililokuwa mali ya Boazi, ambaye alitoka kwenye ukoo wa Elimeleki.
4 Papo hapo Boazi akarudi kutoka Bethlehemu, akawasalimu wavunaji, akasema, “Bwana awe nanyi!”
Nao wakamjibu, “Bwana akubariki.”
5 Boazi akamuuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule mwanamwali ni wa nani?”
6 Msimamizi akamjibu, “Ni yule Mmoabu aliyerudi kutoka nchi ya Moabu pamoja na Naomi. 7 Yeye aliomba, ‘Tafadhali niruhusu niokote na kukusanya miongoni mwa miganda nyuma ya wavunaji.’ Naye ameshinda shambani tangu asubuhi pasipo kupumzika, isipokuwa kwa muda mfupi kivulini.”
8 Kisha Boazi akamwambia Ruthu, “Binti yangu, nisikilize. Usiende kuokota mabaki ya mavuno katika shamba lingine, na usiondoke hapa. Kaa hapa na hawa watumishi wangu wa kike. 9 Angalia shamba wanaume wanamovuna, ufuate nyuma yao. Nimewaamuru wanaume hawa wasikuguse. Wakati wowote ukiona kiu, nenda kwenye mitungi ukanywe maji waliyoyateka wanaume hawa.”
10 Kwa ajili ya hili, akasujudu mpaka nchi, akamwambia, “Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanijali mimi mgeni?”
11 Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wako alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu awali. 12 Bwana na akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi na Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mabawani mwake.”
13 Kisha Ruthu akasema, “Naomba niendelee kupata kibali machoni pako, bwana wangu. Kwa maana umenifariji na umezungumza kwa ukarimu na mjakazi wako, hata ingawa mimi si bora kama mmoja wa watumishi wako wa kike.”
14 Wakati wa chakula, Boazi akamwambia Ruthu, “Karibia hapa. Kula mkate na uchovye ndani ya siki.”
Alipoketi pamoja na wavunaji, akampa nafaka zilizookwa. Akala kiasi alichotaka na kusaza. 15 Alipoinuka ili kuokota mabaki ya nafaka, Boazi akawaagiza watu wake, “Hata kama atakusanya kati ya miganda, msimzuie. 16 Badala yake, toeni masuke katika miganda, mwachieni ayaokote, na msimkemee.”
17 Basi Ruthu akaokota masazo shambani hata jioni. Akatwanga ile shayiri aliyokusanya, ikajaa efa moja. 18 Akaibeba na kuelekea mjini, naye mama mkwe wake akaona jinsi alivyoweza kuokota nafaka nyingi. Pia Ruthu akachukua kile alichobakiza baada ya kula na kushiba, akampa.
19 Basi mkwewe akamuuliza, “Je, umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Abarikiwe mtu yule aliyekujali.”
Ndipo Ruthu akamwambia mama mkwe wake juu ya yule ambaye yeye alikuwa amefanyia kazi katika shamba lake. Akasema, “Yule mtu niliyefanyia kazi kwake leo, anaitwa Boazi.”
20 Naye Naomi akamwambia mkwewe, “Bwana ambariki! Hakuacha kuonyesha fadhili zake kwa walio hai na kwa waliokufa.” Pia akamwambia, “Huyo mtu ni mmoja wa jamaa yetu wa karibu anayestahili kutukomboa.”
21 Kisha Ruthu, Mmoabu, akasema, “Hata aliniambia, ‘Kaa pamoja na watumishi wangu mpaka watakapomaliza kuvuna nafaka yangu yote.’ ”
22 Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, “Binti yangu, itakuwa vyema wewe ufuatane na wasichana wake, kwa sababu katika shamba la mtu mwingine wanaweza kukudhuru.”
23 Kwa hivyo Ruthu akafuatana na watumishi wa kike wa Boazi, akaokota mpaka mwisho wa mavuno ya shayiri na ya ngano. Naye aliishi na mama mkwe wake.