Wimbo wa Solomoni

1001 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Wimbo 1–2

1 Wimbo ulio bora wa Solomoni.

Mpendwa

2 Unibusu kwa busu la kinywa chako,

kwa maana upendo wako unafurahisha kuliko divai.

3 Manukato yako yananukia vizuri,

jina lako ni kama manukato yaliyomiminwa.

Ndiyo sababu wanawali wanakupenda!

4 Nichukue twende nawe, na tufanye haraka!

Mfalme na anilete ndani ya vyumba vyake.

Marafiki

Tunakushangilia na kukufurahia,

tutasifu upendo wako zaidi kuliko divai.

Mpendwa

Tazama jinsi ilivyo bora wakupende!

5 Mimi ni mweusi, lakini napendeza,

enyi binti za Yerusalemu,

mweusi kama mahema ya Kedari,

kama mapazia ya hema la Solomoni.

6 Usinikazie macho kwa sababu mimi ni mweusi,

kwa sababu nimefanywa mweusi na jua.

Wana wa mama yangu walinikasirikia

na kunifanya niwe mtunza mashamba ya mizabibu.

Shamba langu mwenyewe la mizabibu nimeliacha.

7 Niambie, wewe ambaye ninakupenda,

unalisha wapi kundi lako la kondoo

na ni wapi unapowapumzisha kondoo wako adhuhuri.

Kwa nini niwe kama mwanamke aliyefunikwa shela

karibu na makundi ya rafiki zako?

Marafiki

8 Kama hujui, ewe mwanamke mzuri kuliko wote,

fuata nyayo za kondoo,

na kulisha wana-mbuzi wako

karibu na hema za wachungaji.

Mpenzi

9 Mpenzi wangu, ninakufananisha na farasi jike

aliyefungwa katika mojawapo ya magari ya vita ya Farao.

10 Mashavu yako yanapendeza yakiwa na vipuli,

shingo yako ikiwa na mikufu ya vito.

11 Tutakufanyia vipuli vya dhahabu,

vyenye kupambwa kwa fedha.

Mpendwa

12 Wakati mfalme alipokuwa mezani pake,

manukato yangu yalisambaza harufu yake nzuri.

13 Mpenzi wangu kwangu mimi ni kifuko cha manemane

kati ya matiti yangu.

14 Mpenzi wangu kwangu mimi ni kama kishada cha maua ya mhina

kutoka mashamba ya mizabibu ya En-Gedi.

Mpenzi

15 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!

Tazama jinsi ulivyo mzuri!

Macho yako ni kama ya hua.

Mpendwa

16 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!

Ee, tazama jinsi unavyopendeza!

Na kitanda chetu ni cha majani mazuri.

Mpenzi

17 Nguzo za nyumba yetu ni mierezi,

na mapao yetu ni miberoshi.

Mpendwa

2:1 Mimi ni ua la Sharoni,

yungiyungi ya bondeni.

Mpenzi

2 Kama yungiyungi katikati ya miiba

ndivyo alivyo mpenzi wangu katikati ya wanawali.

Mpendwa

3 Kama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni

ndivyo alivyo mpenzi wangu

miongoni mwa wanaume vijana.

Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu,

na tunda lake ni tamu kwangu.

4 Amenichukua mpaka kwenye ukumbi wa karamu,

na bendera ya huyu mwanaume

juu yangu ni upendo.

5 Nitie nguvu kwa zabibu kavu,

niburudishe kwa matofaa,

kwa maana ninazimia kwa mapenzi.

6 Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,

na mkono wake wa kuume unanikumbatia.

7 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza

kwa paa na kwa ayala wa shambani:

Msichochee wala kuamsha mapenzi

hata yatakapotaka yenyewe.

Mpendwa

8 Sikiliza! Mpenzi wangu!

Tazama! Huyu hapa anakuja,

akirukaruka juu milimani

akizunguka juu ya vilima.

9 Mpenzi wangu ni kama paa au ayala kijana.

Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu,

akitazama kupitia madirishani,

akichungulia kimiani.

10 Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia,

“Inuka, mpenzi wangu,

mrembo wangu, tufuatane.

11 Tazama! Wakati wa masika umepita,

mvua imekwisha na ikapita.

12 Maua yanatokea juu ya nchi;

majira ya kuimba yamewadia,

sauti za njiwa zinasikika

katika nchi yetu.

13 Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni,

zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri.

Inuka, njoo mpenzi wangu.

Mrembo wangu, tufuatane.”

Mpenzi

14 Hua wangu penye nyufa za majabali,

mafichoni pembezoni mwa mlima,

nionyeshe uso wako,

na niisikie sauti yako,

kwa maana sauti yako ni tamu,

na uso wako unapendeza.

15 Tukamatie mbweha,

mbweha wale wadogo

wanaoharibu mashamba ya mizabibu,

mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua.

Mpendwa

16 Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake,

yeye hujilisha katikati ya yungiyungi.

17 Mpaka jua linapochomoza,

na vivuli vikimbie,

rudi, mpenzi wangu,

na uwe kama paa,

au kama ayala kijana

juu ya vilima vya Betheri.