Wimbo wa Solomoni (continued)

1001 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Wimbo 3–5

1 Usiku kucha kwenye kitanda changu

nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye;

nilimtafuta, lakini sikumpata.

2 Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini,

katika barabara zake na viwanja;

nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye.

Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata.

3 Walinzi walinikuta

walipokuwa wakizunguka mji.

Nikawauliza, “Je, mmemwona

yule moyo wangu umpendaye?”

4 Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita

nilimpata yule moyo wangu umpendaye.

Nilimshika na sikumwachia aende

mpaka nilipomleta katika nyumba ya mama yangu,

katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.

5 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza

kwa paa na kwa ayala wa shambani:

Msichochee wala kuamsha mapenzi

hata yatakapotaka yenyewe.

Mpenzi

6 Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani

kama nguzo ya moshi,

anayenukia manemane na uvumba

iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote

vya mfanyabiashara?

7 Tazama! Ni gari la Solomoni

lisindikizwalo na mashujaa sitini,

walio wakuu sana wa Israeli,

8 wote wamevaa panga,

wote wazoefu katika vita,

kila mmoja na upanga wake pajani,

wamejiandaa kwa ajili ya hofu za usiku.

9 Mfalme Solomoni alijitengenezea gari;

alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.

10 Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha,

kitako chake kwa dhahabu.

Kiti chake kilipambwa kwa zambarau,

gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo

na binti za Yerusalemu.

11 Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni,

mkamtazame Mfalme Solomoni akiwa amevaa taji,

taji ambalo mama yake alimvika

siku ya arusi yake,

siku ambayo moyo wake ulishangilia.

Mpenzi

4:1 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!

Ee, jinsi ulivyo mzuri!

Macho yako nyuma ya shela yako

ni kama ya hua.

Nywele zako ni kama kundi la mbuzi

zikishuka kutoka Mlima Gileadi.

2 Meno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya sasa hivi,

watokao kuogeshwa.

Kila mmoja ana pacha lake,

hakuna hata mmoja aliye peke yake.

3 Midomo yako ni kama uzi mwekundu,

kinywa chako kinapendeza.

Mashavu yako nyuma ya shela yako

ni kama vipande viwili vya komamanga.

4 Shingo yako ni kama mnara wa Daudi,

uliojengwa kwa madaha,

juu yake zimetundikwa ngao elfu,

zote ni ngao za mashujaa.

5 Matiti yako mawili ni kama wana-paa wawili,

kama wana-paa mapacha

wajilishao katikati ya yungiyungi.

6 Hata kupambazuke na vivuli vikimbie,

nitakwenda kwenye mlima wa manemane

na kwenye kilima cha uvumba.

7 Wewe ni mzuri kote, mpenzi wangu,

hakuna hitilafu ndani yako.

8 Enda nami kutoka Lebanoni, bibi arusi wangu,

enda nami kutoka Lebanoni.

Shuka kutoka ncha ya Amana,

kutoka juu ya Seniri, kilele cha Hermoni,

kutoka mapango ya simba

na kutoka mlima wapendapo kukaa chui.

9 Umeiba moyo wangu, dada yangu, bibi arusi wangu;

umeiba moyo wangu

kwa mtazamo mmoja wa macho yako,

kwa kito kimoja cha mkufu wako.

10 Tazama jinsi pendo lako linavyofurahisha,

dada yangu, bibi arusi wangu!

Pendo lako linafurahisha aje zaidi ya divai,

na harufu ya manukato yako zaidi ya kikolezo chochote!

11 Midomo yako inadondosha utamu kama sega la asali,

bibi arusi wangu;

maziwa na asali viko chini ya ulimi wako.

Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni.

12 Wewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu,

bibi arusi wangu;

wewe ni chanzo cha maji kilichozungushiwa kabisa,

chemchemi yangu peke yangu.

13 Mimea yako ni bustani ya mikomamanga

yenye matunda mazuri sana,

yenye hina na nardo,

14 nardo na zafarani,

mchai na mdalasini,

pamoja na kila aina ya mti wa uvumba,

manemane na udi,

na aina zote za vikolezo bora kuliko vyote.

15 Wewe ni chemchemi ya bustani,

kisima cha maji yatiririkayo,

yakitiririka kutoka Lebanoni.

Mpendwa

16 Amka, upepo wa kaskazini,

na uje, upepo wa kusini!

Vuma juu ya bustani yangu,

ili harufu yake nzuri iweze kuenea mpaka ngʼambo.

Mpendwa wangu na aje bustanini mwake

na kuonja matunda mazuri sana.

Mpenzi

5:1 Nimekuja kwenye bustani yangu, dada yangu,

bibi arusi wangu;

nimekusanya manemane yangu pamoja

na kikolezo changu.

Nimekula sega langu la asali na asali yangu;

nimekunywa divai yangu na maziwa yangu.

Marafiki

Kuleni, enyi marafiki, mnywe;

kunyweni ya kutosha, ee wapenzi.

Mpendwa

2 Nililala lakini moyo wangu ulikuwa macho.

Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha:

“Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu,

hua wangu, asiye na hitilafu.

Kichwa changu kimeloa umande,

na nywele zangu manyunyu ya usiku.”

3 Nimevua joho langu:

je, ni lazima nivae tena?

Nimenawa miguu yangu:

je, ni lazima niichafue tena?

4 Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo;

moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake.

5 Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu,

mikono yangu ikidondosha manemane,

vidole vyangu vikitiririka manemane,

penye vipini vya komeo.

6 Nilimfungulia mpenzi wangu,

lakini mpenzi wangu alishaondoka;

alikuwa amekwenda zake.

Moyo wangu ulishuka kwa kuondoka kwake.

Nilimtafuta lakini sikumpata.

Nilimwita lakini hakunijibu.

7 Walinzi walinikuta

walipokuwa wakifanya zamu za ulinzi mjini.

Walinipiga, wakanijeruhi,

wakaninyangʼanya joho langu,

hao walinzi wa kuta!

8 Enyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza:

kama mkimpata mpenzi wangu,

mtamwambia nini?

Mwambieni ninazimia kwa mapenzi.

Marafiki

9 Je, mpendwa wako ni bora kuliko wengine namna gani,

wewe uliye mzuri kupita wanawake wote?

Je, mpendwa wako ni mzuri kuliko wengine, namna gani,

hata unatuagiza hivyo?

Mpendwa

10 Mpenzi wangu anangʼaa, tena ni mwekundu,

wa kuvutia miongoni mwa wanaume kumi elfu.

11 Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote,

nywele zake ni za mawimbi

na ni nyeusi kama kunguru.

12 Macho yake ni kama ya hua

kandokando ya vijito vya maji,

aliyeogeshwa kwenye maziwa,

yaliyopangwa kama vito vya thamani.

13 Mashavu yake ni kama matuta ya vikolezo

yakitoa manukato.

Midomo yake ni kama yungiyungi

inayodondosha manemane.

14 Mikono yake ni fimbo za dhahabu

iliyopambwa kwa krisolitho.

Mwili wake ni kama pembe ya ndovu iliyongʼarishwa

iliyopambwa na yakuti samawi.

15 Miguu yake ni nguzo za marmar

zilizosimikwa katika vitako vya dhahabu safi.

Sura yake ni kama Lebanoni,

bora kama miti yake ya mierezi.

16 Kinywa chake chenyewe ni utamu,

kwa ujumla yeye ni wa kupendeza.

Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu,

ee binti za Yerusalemu.