Sehemu ya 4: Majengo Mengine ya Solomoni na Fahari Yake

Mungu Anamtokea Solomoni

Kujengwa kwa Nyumba ya Msitu wa Lebanoni. Mungu anamtokea Solomoni.

1004 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wafalme 7:1–12

1 Ilimchukua Solomoni miaka kumi na mitatu kukamilisha ujenzi wa Jumba lake la kifalme. 2 Alijenga Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni, urefu wake ulikuwa dhiraa 100, upana wake dhiraa hamsini na kimo chake dhiraa thelathini, likiwa na safu nne za nguzo za mierezi zikishikilia boriti za mierezi zilizorembwa. 3 Ilipauliwa kwa mierezi juu ya boriti zile zilizolala juu ya nguzo arobaini na tano, kumi na tano kwa kila safu. 4 Madirisha yake yaliwekwa juu kwa safu tatu, yakielekeana. 5 Milango yote ilikuwa na miimo ya mstatili, ilikuwa upande wa mbele katika safu tatu, ikielekeana.

6 Akajenga ukumbi wa nguzo, ambao urefu wake ulikuwa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa thelathini. Mbele ya jengo hilo kulikuwepo baraza. Mbele ya baraza kulikuwepo na nguzo na paa lililoningʼinia.

7 Akajenga ukumbi wa kiti cha enzi, Ukumbi wa Hukumu, mahali ambapo angelitolea hukumu, akaufunika kwa mierezi kutoka sakafuni hadi darini. 8 Kwenye jumba la kifalme ambamo angeliishi, aliiweka nyuma zaidi, ikiwa na mjengo wa aina moja na hiyo nyingine. Pia Solomoni akajenga jumba la kifalme linalofanana na huo ukumbi mkubwa kwa ajili ya binti Farao, aliyekuwa amemwoa.

9 Ujenzi huu wote, kuanzia nje mpaka kwenye ua mkuu na kuanzia kwenye msingi hadi upenuni, ulifanywa kwa mawe ya ubora wa hali ya juu yaliyokuwa yamechongwa kwa vipimo na kusawazishwa kwa msumeno nyuso zake za ndani na za nje. 10 Misingi iliwekwa kwa mawe makubwa yaliyo bora, yenye urefu wa dhiraa kumi na mengine yenye urefu wa dhiraa nane 11 Sehemu za juu kulikuwepo na mawe yenye ubora wa hali ya juu, yaliyokatwa kwa vipimo na boriti za mierezi. 12 Ule ua mkuu ulizungukwa na ukuta wa safu tatu za mawe yaliyochongwa na safu moja ya boriti za mierezi zilizorembwa, kama ulivyokuwa ua wa ndani wa Hekalu la Bwana na baraza yake.

2 Nyakati 7:11–22

11 Solomoni alipomaliza kujenga Hekalu la Bwana na jumba la kifalme, naye akiwa amefanikiwa kutenda yale yote aliyokuwa nayo moyoni mwake kufanya katika Hekalu la Bwana na katika jumba lake mwenyewe la kifalme, 12 Bwana akamtokea Solomoni usiku na kumwambia:

“Nimesikia maombi yako nami nimechagua mahali hapa kwa ajili yangu mwenyewe kuwa Hekalu kwa ajili ya dhabihu.

13 “Wakati nitakapofunga mbingu ili isiwepo mvua, au nikiamuru nzige kula mazao ya nchi au nikituma tauni miongoni mwa watu wangu, 14 kama watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na nitaiponya nchi yao. 15 Sasa macho yangu yatafumbuka na masikio yangu yatasikiliza kwa makini maombi yaombwayo mahali hapa. 16 Kwa maana sasa nimechagua na kutakasa Hekalu hili ili kwamba Jina langu lipate kuwa huko milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwepo huko daima.

17 “Kwa habari yako wewe, kama ukienenda mbele zangu kama Daudi baba yako alivyoenenda na kufanya yote nikuamuruyo, nawe ukizishika amri zangu na sheria zangu, 18 Nitakiimarisha kiti chako cha enzi kama nilivyoagana na Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe mtu wa kutawala juu ya Israeli.’

19 “Lakini kama ukigeuka na kuyaacha maagizo na amri nilizowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, 20 ndipo nitakapoingʼoa Israeli kutoka nchi yangu niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Nitalifanya kitu cha kudharauliwa na kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote. 21 Ingawa Hekalu hili linavutia sana sasa, wote watakaolipita watashangaa na kusema, ‘Kwa nini Bwana amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’ 22 Watu watajibu, ‘Ni kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewatoa Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”

1 Wafalme 9:1–9

1 Solomoni alipomaliza kujenga Hekalu la Bwana na jumba la kifalme, alipokwisha kufanya yote aliyotaka kufanya, 2 Bwana akamtokea mara ya pili, kama alivyokuwa amemtokea huko Gibeoni. 3 Bwana akamwambia:

“Nimesikia dua na maombi uliyofanya mbele zangu, nimeliweka wakfu Hekalu hili ambalo umelijenga, kwa kuweka Jina langu humo milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwa humo siku zote.

4 “Kukuhusu wewe, kama ukienenda kwa unyofu wa moyo na uadilifu, kama baba yako Daudi alivyofanya na kutenda yote ninayoyaagiza kwa kutunza maagizo yangu na sheria, 5 nitakiimarisha kiti chako cha enzi juu ya Israeli milele kama nilivyomwahidi Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe kuwa na mtu kwenye kiti cha enzi cha Israeli.’

6 “Lakini kama ninyi au wana wenu mkigeukia mbali nami na kuziacha amri na maagizo yangu niliyowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, 7 basi nitakatilia mbali Israeli kutoka nchi niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Ndipo Israeli itakuwa kitu cha kudharauliwa na watu na kuwa kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote. 8 Ingawa hekalu hili linavutia sasa, wote watakaolipita watashangaa na kudhihaki wakisema, ‘Kwa nini Bwana amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’ 9 Watu watajibu, ‘Kwa sababu wamemwacha Bwana Mungu wao, aliyewatoa baba zao Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu Bwana ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”

Maeneo Aliyoyateka Solomoni na Matendo Yake Mengine 1001 KK

1 Wafalme 9:10–14

10 Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Solomoni alijenga majengo haya mawili, yaani Hekalu la Bwana na jumba la kifalme, 11 Mfalme Solomoni akampa Hiramu mfalme wa Tiro miji ishirini katika Galilaya, kwa sababu Hiramu alikuwa amempatia mierezi yote, misunobari na dhahabu yote aliyohitaji. 12 Lakini Hiramu alipotoka Tiro kwenda kuiona ile miji ambayo Solomoni alikuwa amempa, hakupendezwa nayo. 13 Hiramu akauliza, “Hii ni miji ya namna gani uliyonipa, ndugu yangu?”

Naye akaiita nchi ya Kabul, jina lililoko hadi leo. 14 Basi Hiramu alikuwa amempelekea mfalme talanta 120 za dhahabu.

2 Nyakati 8:1–11

1 Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Solomoni alilijenga Hekalu la Bwana na jumba lake mwenyewe la kifalme, 2 Solomoni akajenga tena vijiji vile ambavyo Hiramu alikuwa amempa, naye akawapa Waisraeli waishi humo. 3 Kisha Solomoni akaenda Hamath-Soba na kuuteka. 4 Pia akajenga mji wa Tadmori katika jangwa na miji yote ya kuhifadhia vitu katika Hamathi. 5 Akajenga tena Beth-Horoni ya Juu na Beth-Horoni ya Chini, miji yenye ngome, kuta, malango na makomeo. 6 Solomoni pia akajenga Baalathi na miji yake yote ya kuhifadhia vitu, na miji kwa ajili ya magari yake na kwa ajili ya farasi wake, chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, katika Lebanoni na katika nchi yote aliyotawala.

7 Watu wote waliosalia kutoka kwa Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi (haya mataifa hayakuwa Waisraeli), 8 yaani, wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawakuwa wamewaangamiza: hawa Solomoni akawalazimisha kuwa watumwa katika shokoa, kama ilivyo hadi leo. 9 Lakini Solomoni hakuwafanya Waisraeli watumwa kwa ajili ya kazi yake, bali walikuwa wapiganaji, majemadari, maafisa wake, majemadari wa magari yake ya vita na waendesha magari ya vita. 10 Pia walikuwa maafisa wakuu wa Mfalme Solomoni, yaani, maafisa wakaguzi 250 waliosimamia watu.

11 Solomoni akampandisha mke wake binti Farao kutoka Mji wa Daudi na kumleta jumba la kifalme alilokuwa amemjengea, kwa kuwa alisema, “Mke wangu hataishi katika jumba la kifalme la Daudi mfalme wa Israeli, kwa sababu mahali ambapo Sanduku la Bwana limefika ni patakatifu.”

1 Wafalme 9:24

24 Baada ya binti Farao kuja kutoka Mji wa Daudi na kuingia jumba la kifalme ambalo Solomoni alikuwa amemjengea, akajenga Milo.