Kipindi cha 7: Uhamisho wa Babeli

Sehemu ya 1: Matukio Yerusalemu Hadi Hekalu Linapoteketea

Matukio Yerusalemu, tangu mwanzo wa uhamisho hadi kuteketezwa kwa hekalu.

Hati ya Kukunjwa Inasomwa Mara ya Pili

Utawala wa Yehoyakimu unaendelea. Kusomwa kwa hati ya kukunjwa mara ya pili.

605 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yeremia 36:9–32

9 Katika mwezi wa tisa, mnamo mwaka wa tano wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati wa kufunga mbele za Bwana, ilitangazwa kwa watu wote walioko Yerusalemu, na wale wote waliokuwa wamekuja kutoka miji ya Yuda. 10 Kutoka chumba cha Gemaria mwana wa Shafani mwandishi, kilichokuwa katika ua wa juu kwenye ingilio la Lango Jipya la Hekalu, Baruku akawasomea watu wote waliokuwa katika Hekalu la Bwana maneno ya Yeremia kutoka kwenye kile kitabu.

11 Basi Mikaya mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya Bwana kutoka kwenye kile kitabu, 12 alishuka hadi kwenye chumba cha mwandishi kwenye jumba la kifalme, mahali walipokuwa wameketi maafisa wote: yaani Elishama mwandishi, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania, na maafisa wengine wote. 13 Baada ya Mikaya kuwaambia kila kitu ambacho alikuwa amesikia Baruku akiwasomea watu kutoka kwenye kile kitabu, 14 maafisa wote wakamtuma Yehudi mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, kumwambia Baruku, “Leta hicho kitabu ambacho umewasomea watu, nawe mwenyewe uje.” Ndipo Baruku mwana wa Neria akawaendea akiwa na hicho kitabu mkononi mwake. 15 Wakamwambia, “Tafadhali, keti na utusomee hicho kitabu.”

Ndipo Baruku akawasomea kile kitabu. 16 Walipoyasikia maneno hayo yote, wakatazamana wao kwa wao kwa woga na kumwambia Baruku, “Lazima tutoe taarifa ya maneno haya yote kwa mfalme.” 17 Kisha wakamuuliza Baruku, “Tuambie, uliandikaje haya yote? Je, yalitoka kinywani mwa Yeremia?”

18 Baruku akajibu, “Ndiyo, maneno haya yote yalitoka kinywani mwa Yeremia, nami nikayaandika kwa wino katika hiki kitabu.”

19 Ndipo wale maafisa wakamwambia Baruku, “Wewe na Yeremia nendeni mkajifiche. Mtu yeyote asijue mahali mlipo.”

20 Baada ya kuhifadhi kile kitabu ndani ya chumba cha Elishama mwandishi, wakamwendea mfalme katika ua wa nje na kumwarifu kila kitu. 21 Mfalme akamtuma Yehudi akachukue kile kitabu. Yehudi akakileta hicho kitabu kutoka kwenye chumba cha Elishama mwandishi, na akakisoma mbele ya mfalme na maafisa wakiwa wamesimama kando ya mfalme. 22 Ulikuwa mwezi wa tisa, na mfalme alikuwa ameketi chumba cha wakati wa baridi akiota moto. 23 Hata ikawa kila wakati Yehudi alipomaliza kusoma kurasa tatu au nne za hicho kitabu, mfalme alizikata kwa kisu cha mwandishi na kuzitupia motoni, hadi kitabu chote kikateketea. 24 Mfalme na watumishi wake wote waliosikia yote yaliyosomwa hawakuonyesha hofu yoyote, wala hawakuyararua mavazi yao. 25 Hata ingawa Elnathani, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asikichome kile kitabu, yeye hakuwasikiliza. 26 Badala yake, mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, Seraya mwana wa Azrieli, na Shelemia mwana wa Abdeeli kuwakamata mwandishi Baruku na nabii Yeremia. Lakini Bwana alikuwa amewaficha.

27 Baada ya mfalme kuchoma kile kitabu kilichokuwa na yale maneno Baruku aliyokuwa ameyaandika kutoka kinywani mwa Yeremia, neno la Bwana lilimjia Yeremia likisema: 28 “Chukua kitabu kingine na uandike juu yake maneno yote yaliyokuwa katika kile kitabu cha kwanza, ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda amekiteketeza kwa moto. 29 Mwambie pia Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Ulikiteketeza kile kitabu ukasema, “Kwa nini uliandika kwenye kitabu kwamba kwa hakika mfalme wa Babeli angekuja na kuangamiza nchi hii, na kuwakatilia mbali watu na wanyama kutoka humo?” 30 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana kuhusu Yehoyakimu mfalme wa Yuda: Hatakuwa na mtu yeyote atakayekalia kiti cha enzi cha Daudi; maiti yake itatupwa nje kwenye joto wakati wa mchana na kupigwa na baridi wakati wa usiku. 31 Nitamwadhibu yeye, watoto wake na watumishi wake kwa ajili ya uovu wao. Nitaleta juu yao na wote waishio Yerusalemu na watu wa Yuda kila maafa niliyoyasema dhidi yao, kwa sababu hawajasikiliza.’ ”

32 Kisha Yeremia akachukua kitabu kingine na kumpa mwandishi Baruku mwana wa Neria, naye kama Yeremia alivyosema, Baruku akaandika juu yake maneno yote ya kile kitabu ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda alikuwa amekichoma moto, na maneno mengine mengi yaliyofanana na hayo yaliyoongezewa humo.

Yehoyakimu Anaasi na Kufa 603 KK

2 Wafalme 24:2

2 Bwana akatuma wavamiaji wa Wakaldayo, Waaramu, Wamoabu na Waamoni ili kumshambulia. Aliwatuma kuiangamiza Yuda sawasawa na neno la Bwana lililosemwa na watumishi wake manabii.

2 Nyakati 36:5

5 Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na mmoja. Akafanya maovu machoni pa Bwana Mungu wake.

2 Wafalme 24:5

5 Matukio mengine ya utawala wa Yehoyakimu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?

2 Nyakati 36:8

8 Matukio mengine ya utawala wa Yehoyakimu, machukizo aliyoyafanya na yote yaliyoonekana dhidi yake, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda. Naye Yehoyakini mwanawe akawa mfalme baada yake.