Utawala wa Yehoyakini na Uhamisho wa Ezekieli

603 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 24:6–9

6 Yehoyakimu akalala pamoja na baba zake. Naye Yehoyakini mwanawe akawa mfalme baada yake.

7 Mfalme wa Misri hakutoka tena katika nchi yake, kwa sababu mfalme wa Babeli alikuwa ameitwaa himaya yake yote, kuanzia Kijito cha Misri hadi Mto Frati.

8 Yehoyakini alikuwa na miaka kumi na minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu. Jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani kutoka Yerusalemu. 9 Akafanya maovu machoni pa Bwana, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.

Yeremia 22:24–23:40

24 “Hakika kama niishivyo,” asema Bwana, “hata kama wewe, Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya muhuri katika mkono wangu wa kuume, bado ningekungʼoa hapo. 25 Nitakutia mikononi mwa wale wanaotafuta uhai wako, wale unaowaogopa, yaani Nebukadneza mfalme wa Babeli na kwa Wakaldayo. 26 Nitakutupa mbali wewe na mama aliyekuzaa mwende katika nchi nyingine, ambayo hakuna hata mmoja wenu aliyezaliwa huko, nanyi mtafia huko. 27 Kamwe hamtarudi katika nchi mliyotamani kuirudia.”

28 Je, huyu mtu Yekonia ni chungu kilichodharauliwa,

chungu kilichovunjika,

chombo kisichotakiwa na mtu yeyote?

Kwa nini yeye na watoto wake watupwe nje kwa nguvu,

na kutupwa kwenye nchi wasioijua?

29 Ee nchi, nchi, nchi,

sikia neno la Bwana!

30 Hili ndilo Bwana asemalo:

“Mwandike huyu mtu kama asiye na mtoto,

mtu ambaye hatafanikiwa maisha yake yote,

kwa maana hakuna mtoto wake atakayefanikiwa,

wala kukaa kwenye kiti cha enzi cha Daudi

wala kuendelea kutawala katika Yuda.”

23:1 “Ole wao wachungaji wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yangu!” asema Bwana. 2 Kwa hiyo hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, analowaambia wachungaji wanaowachunga watu wangu: “Kwa sababu mmelitawanya kundi langu na kuwafukuzia mbali, wala hamkuwatunza, basi mimi nitawaadhibu kwa ajili ya uovu mliofanya,” asema Bwana. 3 “Mimi mwenyewe nitayakusanya mabaki ya kundi langu kutoka nchi zote ambazo nimewafukuzia, nami nitawarudisha katika malisho yao, mahali ambapo watazaa na kuongezeka idadi yao. 4 Nitaweka wachungaji juu yao ambao watawachunga, nao hawataogopa tena au kutishwa, wala hatapotea hata mmoja,” asema Bwana.

5 Bwana asema, “Siku zinakuja,

nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki,

Mfalme atakayetawala kwa hekima,

na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.

6 Katika siku zake, Yuda ataokolewa

na Israeli ataishi salama.

Hili ndilo jina atakaloitwa:

Bwana Haki Yetu.

7 “Hivyo basi, siku zinakuja, wakati ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’ 8 bali watasema, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewatoa wazao wa Israeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia,’ asema Bwana. Ndipo wataishi katika nchi yao wenyewe.”

9 Kuhusu manabii:

Moyo wangu umevunjika ndani yangu;

mifupa yangu yote inatetemeka.

Nimekuwa kama mtu aliyelewa,

kama mtu aliyelemewa na divai,

kwa sababu ya Bwana

na maneno yake matakatifu.

10 Nchi imejaa wazinzi;

kwa sababu ya laana, nchi imekauka

na malisho yaliyoko nyikani yamekauka.

Mwenendo wa manabii ni mbaya

na mamlaka yao si ya haki.

11 “Nabii na kuhani wote si wacha Mungu;

hata hekaluni mwangu ninaona uovu wao,”

asema Bwana.

12 “Kwa hiyo mapito yao yatakuwa utelezi,

watafukuziwa mbali gizani

na huko wataanguka.

Nitaleta maafa juu yao

katika mwaka wa kuadhibiwa kwao,”

asema Bwana.

13 “Miongoni mwa manabii wa Samaria

nililiona jambo la kuchukiza:

Walitabiri kwa Baali

na kuwapotosha Israeli watu wangu.

14 Nako miongoni mwa manabii wa Yerusalemu

nimeona jambo baya sana:

Wanafanya uzinzi

na kuenenda katika uongo.

Wanatia nguvu mikono ya watenda mabaya,

kwa ajili hiyo hakuna yeyote

anayeachana na uovu wake.

Wote wako kama Sodoma kwangu;

watu na Yerusalemu wako kama Gomora.”

15 Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo kuhusu manabii:

“Nitawafanya wale chakula kichungu

na kunywa maji yaliyotiwa sumu,

kwa sababu kutokana na manabii wa Yerusalemu

kutokumcha Mungu kumeenea katika nchi yote.”

16 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo:

“Msisikilize wanachowatabiria manabii,

wanawajaza matumaini ya uongo.

Wanasema maono kutoka akili zao wenyewe,

hayatoki katika kinywa cha Bwana.

17 Huendelea kuwaambia wale wanaonidharau mimi,

‘Bwana asema: Mtakuwa na amani.’

Kwa wale wote wafuatao ugumu wa mioyo yao,

wao husema, ‘Hakuna dhara litakalowapata.’

18 Lakini ni yupi miongoni mwao aliyesimama katika baraza la Bwana

ili kuona au kusikia neno lake?

Ni nani aliyesikiliza

na kusikia neno lake?

19 Tazama, dhoruba ya Bwana

itapasuka kwa ghadhabu,

kisulisuli kitazunguka na kuanguka

vichwani vya waovu.

20 Hasira ya Bwana haitageuka mpaka amelitimiza kusudi la moyo wake.

Siku zijazo mtalifahamu kwa wazi.

21 Mimi sikuwatuma manabii hawa,

lakini bado wamekimbia wakitangaza ujumbe wao.

Mimi sikusema nao,

lakini wametabiri.

22 Lakini kama wangesimama barazani mwangu,

wangetangaza maneno yangu kwa watu wangu,

nao wangewageuza kutoka njia zao mbaya

na kutoka matendo yao maovu.”

23 “Je, mimi ni Mungu aliyeko hapa karibu tu,”

Bwana asema,

“wala si Mungu aliyeko pia mbali?

24 Je, mtu yeyote aweza kujificha

mahali pa siri ili nisiweze kumwona?”

Bwana asema.

“Je, mimi sikuijaza mbingu na nchi?”

Bwana asema.

25 “Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’ 26 Mambo haya yataendelea mpaka lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe? 27 Wanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau jina langu, kama baba zao walivyolisahau jina langu kwa kumwabudu Baali. 28 Mwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asema Bwana. 29 “Je, neno langu si kama moto,” asema Bwana, “na kama nyundo ivunjayo mwamba vipande vipande?

30 “Kwa hiyo, niko kinyume na manabii wanaoibiana maneno kana kwamba ni yangu,” asema Bwana. 31 “Naam, mimi niko kinyume na manabii wanaotikisa ndimi zao wenyewe na kusema, ‘Bwana asema.’ 32 Kweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asema Bwana. “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaamuru. Hawawafaidi watu hawa hata kidogo,” asema Bwana.

33 “Wakati watu hawa, au nabii, au kuhani watakapokuuliza, ‘Mzigo wa Bwana ni nini?’ wewe utawaambia, ‘Ninyi ndio mzigo. Nami nitawavua kama vazi, asema Bwana.’ 34 Nabii, kuhani, au mtu yeyote akisema, ‘Huu ndio mzigo wa Bwana,’ nitamwadhibu huyo na nyumba yake. 35 Hivyo mnaambiana kila mmoja na mwenzake, au kwa mtu wa nyumba yao: ‘Bwana amejibu nini?’ au ‘Bwana amesema nini?’ 36 Lakini kamwe msiseme tena, ‘Nina mzigo wa Bwana,’ kwa sababu kila neno la mtu binafsi linakuwa mzigo wake mwenyewe, na hivyo kupotosha maneno ya Mungu aliye hai, Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wetu. 37 Hivi ndivyo utakavyoendelea kumuuliza nabii: ‘Bwana amekujibu nini?’ au ‘Je, Bwana amesema nini?’ 38 Ingawa unadai, ‘Huu ndio mzigo wa Bwana,’ hili ndilo Bwana asemalo: Ulitumia maneno, ‘Huu ndio mzigo wa Bwana,’ hata ingawa nilikuambia kuwa kamwe usiseme, ‘Huu ni mzigo wa Bwana.’ 39 Kwa hiyo, hakika nitakusahau na kukutupa mbali na uso wangu pamoja na mji niliowapa ninyi na baba zenu. 40 Nitaleta juu yako fedheha ya kudumu: yaani aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”

2 Wafalme 24:10–16

10 Wakati huo, maafisa wa Nebukadneza mfalme wa Babeli walikuja ili kuishambulia Yerusalemu, nao wakaizunguka kwa jeshi. 11 Nebukadneza mwenyewe akaupandia mji wakati maafisa wake walipokuwa wameuzunguka kwa jeshi. 12 Yehoyakini mfalme wa Yuda, mama yake, wahudumu wake, wakuu na maafisa wake wote wakajisalimisha kwa Nebukadneza.

Katika mwaka wa nane wa utawala wa mfalme wa Babeli, akamchukua Yehoyakini kuwa mfungwa. 13 Kama vile Bwana alivyokuwa amesema, Nebukadneza akaondoa hazina yote kutoka Hekalu la Bwana na kutoka jumba la mfalme, akavichukua vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Solomoni mfalme wa Israeli alikuwa amevitengeneza kwa ajili ya Hekalu la Bwana. 14 Akawachukua watu wa Yerusalemu wote kwenda uhamishoni: yaani maafisa wote na mashujaa, watu wenye ustadi na ufundi, jumla yao watu elfu kumi. Watu maskini sana ndio tu waliobaki katika nchi.

15 Nebukadneza akamchukua mateka Yehoyakini hadi Babeli. Pia akawachukua utumwani kutoka Yerusalemu hadi Babeli mama yake mfalme, wake zake, maafisa wake, na viongozi wote wa nchi. 16 Mfalme wa Babeli pia akawahamishia Babeli mashujaa elfu saba, wenye nguvu na wanaofaa kupigana vita, na watu wenye ustadi na mafundi elfu moja.

2 Nyakati 36:9–10

9 Yehoyakini alikuwa na miaka kumi na minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu na siku kumi. Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana. 10 Mnamo majira ya vuli, Mfalme Nebukadneza akatuma watu, nao wakamleta Babeli, pamoja na vyombo vya thamani kutoka Hekalu la Bwana. Naye akamfanya Sedekia, ndugu yake Yehoyakimu kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu.