Baruku Asoma Gombo kwa Mara ya Kwanza
606 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia nabii Yeremia kutoka kwa Bwana, kusema: 2 “Chukua kitabu uandike ndani yake maneno yote niliyonena nawe kuhusu Israeli, Yuda na mataifa mengine yote, tangu nilipoanza kunena nawe wakati wa utawala wa Yosia hadi sasa. 3 Labda watu wa Yuda watakaposikia juu ya kila maafa ninayokusudia kuwapiga nayo, kila mmoja wao atageuka kutoka njia zake mbaya, kisha nitasamehe uovu wao na dhambi yao.”
4 Hivyo Yeremia akamwita Baruku mwana wa Neria, naye Yeremia alipokuwa akiyakariri maneno yote aliyoyasema Bwana, Baruku akayaandika katika kitabu. 5 Kisha Yeremia akamwambia Baruku, “Nimezuiliwa, mimi siwezi kuingia katika Hekalu la Bwana. 6 Basi wewe nenda katika nyumba ya Bwana siku ya kufunga, uwasomee watu maneno ya Bwana kutoka kitabu hiki yale uliyoyaandika kutoka kinywani mwangu. Wasomee watu wote wa Yuda waliofika kutoka miji yao. 7 Labda wataomba na kusihi mbele za Bwana na kila mmoja akageuka kutoka njia zake mbaya, kwa sababu hasira na ghadhabu zilizotamkwa dhidi ya watu hawa na Bwana ni kubwa.”
8 Baruku mwana wa Neria akafanya kila kitu nabii Yeremia alichomwambia kufanya. Alisoma maneno ya Bwana katika Hekalu la Bwana kutoka kile kitabu.
Baruku Afarijiwa Baada ya Kusoma Gombo
1 Hili ndilo nabii Yeremia alilomwambia Baruku mwana wa Neria katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, baada ya Baruku kuandika katika kitabu maneno ambayo yalitoka kinywani mwa Yeremia wakati ule: 2 “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, akuambialo wewe Baruku: 3 Ulisema, ‘Ole wangu! Bwana ameongeza huzuni juu ya maumivu yangu, nimechoka kwa kulia kwa uchungu wala sipati pumziko.’ ”
4 Bwana akasema, “Mwambie hivi: ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Nitakibomoa kile nilichokijenga, na kungʼoa kile nilichokipanda katika nchi yote. 5 Je, utajitafutia mambo makubwa kwa ajili yako mwenyewe? Usiyatafute hayo. Kwa kuwa nitaleta maangamizi juu ya watu wote, asema Bwana, lakini popote utakapokwenda, nitayaokoa maisha yako.’ ”
Utumwa Waanza
1 Wakati wa utawala wa Yehoyakimu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliishambulia nchi, naye Yehoyakimu akawa mtumwa wake kwa miaka mitatu. Lakini hatimaye akabadili mawazo yake na kuasi dhidi ya Nebukadneza.
6 Nebukadneza mfalme wa Babeli akamshambulia na kumfunga kwa pingu za shaba akampeleka Babeli. 7 Nebukadneza akachukua pia vyombo kutoka Hekalu la Bwana na kuviweka katika hekalu lake huko Babeli.
1 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu kwa jeshi. 2 Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza, pamoja na baadhi ya vyombo kutoka Hekalu la Mungu. Hivi akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari, naye akaviweka nyumbani ya hazina ya mungu wake.
3 Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa mfalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya mfalme na kutoka jamaa kuu, 4 vijana wanaume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonyesha kipaji katika kila aina ya elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo. 5 Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, na hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.
6 Baadhi ya hawa vijana walitoka Yuda: nao ni Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. 7 Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya: Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki, na Azaria akamwita Abednego.
3 Hakika mambo haya yalitokea Yuda kulingana na agizo la Bwana, ili kuwaondoa kutoka machoni pake kwa sababu ya dhambi za Manase na yote aliyoyafanya, 4 ikiwa ni pamoja na kumwaga damu isiyo na hatia. Kwa kuwa aliijaza Yerusalemu kwa damu isiyo na hatia, naye Bwana hakuwa radhi kusamehe.