Baraza la Wayahudi Linapinga Mamlaka ya Yesu

Viongozi (Baraza la Wayahudi) wanapinga rasmi mamlaka ya Yesu kama mwalimu aliyetambuliwa (rabi).

Katika ua wa hekalu. (Jumanne) Siku ya mabishano

Yesu anaweka msingi wa mamlaka yake ya kibinadamu kwa Yohana Mbatizaji, mtangulizi wake aliyembatiza, na anadai maoni ya Baraza la Wayahudi kuhusu ubatizo wa Yohana. Swali hili kali la kujibu swali linawafanya viongozi wa Wayahudi washindwe kujibu, na Yesu anasisitiza hoja yake kwa mifano mitatu: (a) mfano wa wana wawili; (b) mfano wa wapangaji waovu; (c) mfano wa karamu ya arusi ya mwana wa mfalme.

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 21:23–22:14

21:23 Yesu alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha na kusema, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka hayo?”

24 Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Kama mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.

25 Ubatizo wa Yohana, ulitoka wapi? Je, ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema ulitoka mbinguni atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’

26 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yohana kuwa ni nabii.”

27 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.”

Naye akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”

28 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’

29 “Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitakwenda.’ Baadaye akabadili mawazo yake akaenda.

30 “Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine akamwambia vilevile. Yeye akajibu, ‘Nitakwenda, bwana,’ lakini hakwenda.

31 “Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?”

Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.”

Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika Ufalme wa Mungu. 32 Kwa maana Yohana alikuja kwenu kuwaonyesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.

33 “Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo ndani yake na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri kwenda nchi nyingine.

34 Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake.

35 “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe.

36 Kisha akawatuma kwao watumishi wengine, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile.

37 Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’

38 “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’

39 Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.

40 “Kwa hiyo, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?”

41 Wakamjibu, “Kwa huzuni kuu atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.”

42 Yesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba:

“ ‘Jiwe walilolikataa waashi

limekuwa jiwe kuu la pembeni.

Bwana ndiye alitenda jambo hili,

nalo ni la ajabu machoni petu’?

43 “Kwa hiyo ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake.

44 Yeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”

45 Viongozi wa Makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano ya Yesu, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao.

46 Wakatafuta njia ya kumkamata, lakini wakaogopa umati wa watu, kwa kuwa watu walimwona Yesu kuwa ni nabii.

22:1 Yesu akasema nao tena kwa mifano, akawaambia, 2 “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. 3 Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja.

4 “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’

5 “Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake. 6 Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua. 7 Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto.

8 “Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja. 9 Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’ 10 Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni.

11 “Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi. 12 Mfalme akamuuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema.

13 “Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’

14 “Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.”

Marko 11:27–12:12

11:27 Wakafika tena Yerusalemu, na Yesu alipokuwa akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wa watu wakamjia.

28 Wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?”

29 Yesu akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.

30 Niambieni, je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

31 Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, “Kama tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’

32 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’…” (Waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yohana alikuwa nabii wa kweli.)

33 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatujui.”

Naye Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”

12:1 Yesu akaanza kusema nao kwa mifano, akawaambia: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akachimba shimo ndani yake kwa ajili ya shinikizo la kusindika divai, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha shamba hilo la mizabibu kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwenda nchi nyingine.

2 Wakati wa mavuno ulipofika, mwenye shamba akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili kuchukua sehemu yake ya mavuno ya shamba la mizabibu kutoka kwa hao wapangaji.

3 Lakini wale wakulima walimkamata yule mtumishi, wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu.

4 Kisha yule mwenye shamba akamtuma mtumishi mwingine kwao; nao wale wakulima wakampiga kichwani na kumfanyia mambo ya aibu.

5 Kisha akamtuma mtumishi mwingine, naye huyo wakamuua. Akawatuma wengine wengi; baadhi yao wakawapiga, na wengine wakawaua.

6 “Mwenye shamba alikuwa bado na mmoja wa kumtuma, mwanawe aliyempenda. Hatimaye akamtuma akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’

7 “Lakini wale wapangaji wakasemezana pamoja, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, nao urithi utakuwa wetu.’

8 Hivyo wakamchukua na kumuua, wakamtupa nje ya lile shamba la mizabibu.

9 “Sasa basi yule mwenye shamba atafanya nini? Atakuja na kuwaua hao wapangaji, kisha atawapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.

10 Je, hamjasoma Andiko hili:

“ ‘Jiwe walilolikataa waashi

limekuwa jiwe kuu la pembeni;

11 Bwana ndiye alitenda jambo hili,

nalo ni ajabu machoni petu’?”

12 Walipotambua kuwa amesema mfano huo kwa ajili yao, wakataka kumkamata, lakini wakaogopa ule umati wa watu. Wakamwacha, wakaondoka, wakaenda zao.

Luka 20:1–19

20:1 Siku moja, Yesu alipokuwa akifundisha watu Hekaluni na kuhubiri habari njema, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, pamoja na wazee wa watu wakamjia.

2 Wakamuuliza, “Tuambie, unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Ni nani aliyekupa mamlaka haya?”

3 Akawajibu, “Nami nitawauliza swali. 4 Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

5 Wakahojiana wao kwa wao wakisema, “Kama tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’

6 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ watu wote watatupiga mawe, kwa sababu wanaamini kwamba Yohana alikuwa nabii.”

7 Basi wakajibu, “Hatujui ulikotoka.”

8 Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”

9 Akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwa muda mrefu.

10 Wakati wa mavuno ulipofika, akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili wampe sehemu ya mavuno ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu.

11 Akamtuma mtumishi mwingine, huyo naye wakampiga, wakamfanyia mambo ya aibu na kumfukuza.

12 Bado akamtuma na mwingine wa tatu, huyu pia wakamjeruhi na kumtupa nje ya shamba.

13 “Basi yule mwenye shamba la mizabibu akasema, ‘Nifanye nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa, huenda yeye watamheshimu.’

14 “Lakini wale wapangaji walipomwona, wakasemezana wao kwa wao. Wakasema, ‘Huyu ndiye mrithi. Basi na tumuue ili urithi uwe wetu.’

15 Kwa hiyo wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.”

“Sasa basi yule mwenye shamba la mizabibu atawafanyia nini wapangaji hawa?

16 Atakuja na kuwaua hao wapangaji, na kuwapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.”

Watu waliposikia hayo wakasema, “Mungu apishie mbali jambo hili lisitokee!”

17 Lakini Yesu akawakazia macho, akasema, “Basi ni nini maana ya yale yaliyoandikwa:

“ ‘Jiwe walilolikataa waashi,

limekuwa jiwe kuu la pembeni’?

18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”

19 Walimu wa sheria na viongozi wa makuhani wakatafuta njia ya kumkamata mara moja, kwa sababu walifahamu kwamba amesema mfano huo kwa ajili yao. Lakini waliwaogopa watu.