Mtini Unalaaniwa na Hekalu Linatakaswa Tena

Mtini usiozaa unalaaniwa, na hekalu linatakaswa kwa mara ya pili.

Bethania na Yerusalemu (Jumatatu). Siku ya nguvu za kimasihi

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 21:18–19, 12–13

21:18 Asubuhi na mapema, Yesu alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa.

19 Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka.

12 Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa.

13 Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.”

Marko 11:12–18

11:12 Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa.

13 Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini. 14 Akauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo.

15 Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, 16 wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu.

17 Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa:

“ ‘Nyumba yangu itaitwa

nyumba ya sala kwa mataifa yote’?

Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ”

18 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote ulikuwa unashangazwa na mafundisho yake.

Luka 19:45–48

19:45 Ndipo akaingia eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza vitu humo.

46 Naye akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ”

47 Kila siku alikuwa akifundisha Hekaluni. Lakini viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na viongozi wa watu walikuwa wakitafuta njia ili kumuua. 48 Lakini hawakupata nafasi kwa sababu watu wote walimfuata wakiyasikiliza maneno yake kwa usikivu mwingi.

Wayunani Fulani Wanatamani Kumwona Yesu

Hamu ya Wayunani fulani ya kumwona Yesu inawachanganya wanafunzi. Inamwongoza Yesu, akiwa na fadhaa rohoni, kufafanua maisha na kifo kama dhabihu, na kuonyesha jinsi atakavyowavuta watu wote kwake kwa “kuinuliwa.”

Yerusalemu (Jumatatu)

Yohana 12:20–50

12:20 Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wamekwenda kuabudu wakati wa Sikukuu. 21 Hawa wakamjia Filipo, ambaye alikuwa mwenyeji wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Yesu.” 22 Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Yesu.

23 Yesu akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa. 24 Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa huzaa mbegu nyingi. 25 Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele. 26 Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.

27 “Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii.’ Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu. 28 Baba, litukuze jina lako.”

Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.” 29 Ule umati wa watu uliokuwa mahali pale uliisikia nao ukasema, “Hiyo ni sauti ya radi,” wengine wakasema, “Malaika ameongea naye.”

30 Yesu akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu. 31 Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. 32 Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.” 33 Yesu aliyasema haya akionyesha ni kifo gani atakachokufa.

34 Ule umati wa watu ukapiga kelele ukasema, “Tumesikia kutoka Sheria kwamba ‘Kristo adumu milele,’ wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?”

35 Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingalipo pamoja nanyi. Enendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakokwenda. 36 Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone.

37 Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini. 38 Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema:

“Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu,

na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?”

39 Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine:

40 “Amewafanya vipofu,

na kuifanya mioyo yao kuwa migumu,

ili wasiweze kuona kwa macho yao,

wala kuelewa kwa mioyo yao,

wasije wakageuka nami nikawaponya.”

41 Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Yesu na kunena habari zake.

42 Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi. 43 Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu.

44 Yesu akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali yeye aliyenituma. 45 Yeyote anionaye mimi, amemwona yeye aliyenituma. 46 Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kwamba kila mtu aniaminiye asibaki gizani.

47 “Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. 48 Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. 49 Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. 50 Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”

Mtini Usiozaa Unakutwa Umenyauka

Njiani kutoka Bethania kwenda Yerusalemu. (Jumanne)

Mathayo 21:20–22

21:20 Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?”

21 Yesu akawajibu, “Amin, nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ngʼoka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. 22 Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”

Marko 11:19–26

11:19 Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji.

20 Asubuhi yake walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake.

21 Petro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Rabi, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!”

22 Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. 23 Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu. 25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [ 26 Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]”

Luka 21:37–38

21:37 Kila siku Yesu alikuwa akifundisha Hekaluni, na jioni ilipofika, alikwenda zake kwenye Mlima wa Mizeituni na kukaa huko usiku kucha.

38 Nao watu wote walikuja asubuhi na mapema Hekaluni ili kumsikiliza.