Sehemu ya 11: Huduma ya Mwisho ya Hadharani Huko Yerusalemu

Kuanzia Ijumaa iliyotangulia hadi Jumanne ya Wiki ya Mateso, wakati wa majira ya kuchipua mwaka wa 30 BK (au 29 BK). Muda mfupi kabla ya Pasaka

Yesu Anafika Bethania Karibu na Yerusalemu

Ijumaa alasiri

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yohana 11:55–12:1, 9–11

11:55 Basi Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walitoka vijijini wakaenda Yerusalemu kabla ya Pasaka ili wakajitakase. 56 Watu wakawa wanamtafuta Yesu, nao waliposimama kwenye eneo la Hekalu waliulizana, Je, mtu huyu hatakuja kamwe kwenye Sikukuu? 57 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kuwa yeyote atakayejua mahali Yesu aliko, lazima atoe taarifa ili wapate kumkamata.

12:1 Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alikwenda Bethania mahali ambako Lazaro aliyekuwa amefufuliwa na Yesu alikuwa anaishi.

9 Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Yesu alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Yesu, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua. 10 Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakafanya mpango wa kumuua Lazaro pia, 11 kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake Wayahudi wengi walikuwa wanamwendea Yesu na kumwamini.

Yesu Anaingia Yerusalemu kwa Ushindi kama Masiya

Hapa tuna safari na mafundisho ya Mwokozi siku za Jumapili, Jumatatu na Jumanne: mwisho wa huduma yake ya hadharani, isipokuwa yale machache aliyosema wakati wa kesi zake mbele ya Wayahudi na Warumi. Mafundisho yake yote baada ya haya yanatolewa kwa wanafunzi wake.

Kutoka Bethania kwenda Yerusalemu na kurudi (Jumapili). Siku ya kujidhihirisha kama Masihi

Mathayo 21:1–3, 6–7, 4–5, 8–11, 14–17

21:1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili,

2 akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu, nanyi mtamkuta punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee.

3 Kama mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara.”

6 Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza.

7 Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Yesu akaketi juu yake.

4 Haya yalitukia ili litimie lile lililonenwa na nabii, akisema:

5 “Mwambieni Binti Sayuni,

‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako,

ni mnyenyekevu, naye amepanda punda,

juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”

8 Umati mkubwa wa watu ukatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kutoka kwenye miti, wakayatandaza barabarani.

9 Ule umati wa watu uliomtangulia na ule uliomfuata ukapiga kelele ukisema,

“Hosana, Mwana wa Daudi!”

“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”

“Hosana juu mbinguni!”

10 Yesu alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?”

11 Ule umati wa watu ukajibu, “Huyu ni Yesu, yule nabii kutoka Nazareti katika Galilaya.”

14 Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya.

15 Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika.

16 Wakamuuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?”

Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma,

“ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao

umeamuru sifa’?”

17 Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.

Marko 11:1–11

11:1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni. Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake,

2 akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na hapo mtakapoingia kijijini, mtamkuta mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa.

3 Kama mtu yeyote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ”

4 Wakaenda, wakamkuta mwana-punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba.

5 Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Mna maana gani mnapomfungua huyo mwana-punda?”

6 Wakawajibu kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu.

7 Kisha wakamleta huyo mwana-punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda.

8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani. 9 Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema,

“Hosana!”

“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”

10 “Umebarikiwa Ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!”

“Hosana kwake yeye aliye juu!”

11 Yesu akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni. Akaangalia kila kitu kilichokuwamo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.

Luka 19:29–44

19:29 Naye alipokaribia Bethfage na Bethania kwenye mlima uitwao Mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia,

30 “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa.

31 Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’ ”

32 Wale waliotumwa wakaenda, wakakuta kila kitu kama vile Yesu alivyokuwa amewaambia.

33 Walipokuwa wanamfungua yule mwana-punda, wenyewe wakawauliza, “Mbona mnamfungua huyo mwana-punda?”

34 Wale wanafunzi wakajibu, “Bwana anamhitaji.”

35 Wakamleta kwa Yesu, nao baada ya kutandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, wakampandisha Yesu juu yake.

36 Alipokuwa akienda akiwa amempanda, watu wakatandaza mavazi yao barabarani.

37 Alipokaribia mahali yanapoanzia materemko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema:

38 “Amebarikiwa Mfalme ajaye kwa Jina la Bwana!”

“Amani mbinguni na utukufu huko juu sana.”

39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwamo miongoni mwa ule umati wa watu wakamwambia, “Mwalimu, waamuru wanafunzi wako wanyamaze.”

40 Yesu akawajibu, “Nawaambia ninyi, kama hawa wakinyamaza, mawe yatapiga kelele.”

41 Alipokaribia Yerusalemu na kuuona mji, aliulilia, 42 akisema, “Laiti ungalijua hata wewe leo yale ambayo yangeleta amani, lakini sasa yamefichika machoni pako. 43 Hakika siku zinakujia, ambazo adui zako watakuzingira, nao watakuzunguka pande zote na kukuzuilia ndani. 44 Watakuponda chini, wewe na watoto walioko ndani ya kuta zako. Nao hawataacha hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukutambua wakati wa kujiliwa kwako.”

Yohana 12:12–19

12:12 Siku iliyofuata umati mkubwa uliokuwa umekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Yesu angekuja Yerusalemu.

13 Basi wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema,

“Hosana!”

“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”

“Amebarikiwa Mfalme wa Israeli!”

14 Yesu akamkuta mwana-punda akampanda, kama ilivyoandikwa,

15 “Usiogope, Ewe binti Sayuni;

tazama, Mfalme wako anakuja,

amepanda mwana-punda!”

16 Wanafunzi wake Yesu mwanzoni hawakuelewa mambo haya, lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye.

17 Wale waliokuwepo wakati Yesu alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu, waliendelea kushuhudia.

18 Ni kwa sababu pia walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda muujiza huu ndiyo maana umati wa watu ukaenda kumlaki.

19 Hivyo Mafarisayo walipoona hayo wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lolote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”