Mafarisayo na Maherode Wanajaribu Kumnasa Yesu Kuhusu Kodi

Mafarisayo na Maherode wanajaribu kumnasa Yesu kuhusu kulipa kodi kwa Kaisari.

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 22:15–22

22:15 Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Yesu katika maneno yake.

16 Wakatuma wanafunzi wao kwake pamoja na Maherode. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonyesha upendeleo. 17 Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?”

18 Lakini Yesu, akijua makusudi yao mabaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega?

19 Nionyesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari.

20 Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”

21 Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”

Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”

22 Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao.

Marko 12:13–17

12:13 Baadaye wakawatuma baadhi ya Mafarisayo na Maherode ili kwenda kumtega Yesu katika yale anayosema.

14 Wakamjia, wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu. Wewe huyumbishwi na wanadamu, kwa kuwa huna upendeleo. Lakini wewe huifundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?

15 Je, tulipe kodi au tusilipe?”

Lakini Yesu alijua unafiki wao. Akawauliza “Mbona mnajaribu kunitega? Nileteeni hiyo dinari niione.”

16 Wakamletea hiyo sarafu. Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”

Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”

17 Ndipo Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”

Nao wakamstaajabia sana.

Luka 20:20–26

20:20 Kwa hiyo wakawa wanamchunguza na kutuma wapelelezi waliojifanya kuwa wenye haki ili wapate kumtega kwa maneno asemayo, ili wamtie katika uwezo na mamlaka ya mtawala.

21 Hivyo wale wapelelezi wakamuuliza, “Mwalimu, tunajua unasema na kufundisha yaliyo kweli wala humpendelei mtu, bali wafundisha njia ya Mungu katika kweli.

22 Je, ni halali sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au la?”

23 Lakini Yesu akatambua hila yao, kwa hiyo akawaambia,

24 “Nionyesheni dinari. Je, sura hii na maandishi haya yaliyoko juu yake ni vya nani?”

25 Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”

Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”

26 Wakashindwa kumkamata kwa yale aliyokuwa amesema hadharani. Nao wakashangazwa mno na majibu yake, wakanyamaza kimya.

Kitendawili cha Masadukayo Kuhusu Ufufuo

Masadukayo wanamwuliza Yesu swali la kutatanisha kuhusu ufufuo.

Katika ua wa hekalu. (Jumanne)

Mathayo 22:23–33

22:23 Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza swali, wakisema,

24 “Mwalimu, Mose alisema, ‘Kama mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’

25 Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane.

26 Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba.

27 Hatimaye, yule mwanamke naye akafa.

28 Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?”

29 Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu.

30 Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni.

31 Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba, 32 ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”

33 Ule umati wa watu uliposikia hayo, ulishangaa sana kwa mafundisho yake.

Marko 12:18–27

12:18 Kisha Masadukayo, wale wasemao kuwa hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu,

19 wakasema, “Mwalimu, Mose alituandikia kuwa kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto.

20 Basi palikuwepo ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa pasipo kuwa na mtoto yeyote.

21 Wa pili akamwoa yule mjane, lakini naye akafa bila kuacha mtoto yeyote. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa tatu. 22 Hakuna hata mmojawapo wa hao ndugu wote saba aliyeacha mtoto. Hatimaye yule mwanamke naye akafa.

23 Kwa hiyo wakati wa ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?”

24 Yesu akawajibu, “Je, hampotoki kwa sababu hamfahamu Maandiko wala uweza wa Mungu?

25 Wafu watakapofufuka, hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni.

26 Basi kuhusu wafu kufufuliwa, je hamjasoma katika Kitabu cha Mose jinsi Mungu alivyosema na Mose kutoka kile kichaka akisema, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo?’

27 Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai. Kwa hiyo mmekosea kabisa.”

Luka 20:27–40

20:27 Baadhi ya Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza,

28 “Mwalimu, Mose alituandikia kwamba kama ndugu wa mtu akifa na kumwacha mkewe bila mtoto, basi huyo mtu inampasa amwoe huyo mjane ili amzalie ndugu yake watoto.

29 Basi palikuwepo ndugu saba. Yule wa kwanza akaoa, akafa bila kuzaa mtoto.

30 Kisha yule wa pili akamwoa huyo mjane, naye akafa bila mtoto, 31 naye wa tatu pia akamwoa. Vivyo hivyo ndugu wote saba wakawa wamemwoa huyo mwanamke, na wote wakafa pasipo yeyote kupata mtoto.

32 Mwishowe, yule mwanamke naye akafa.

33 Sasa basi, siku ya ufufuo huyo mwanamke atakuwa mke wa nani, maana aliolewa na ndugu wote saba?”

34 Yesu akawajibu, “Katika maisha haya watu huoa na kuolewa. 35 Lakini wale ambao wamehesabiwa kwamba wanastahili kupata nafasi katika ulimwengu ule na katika ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaolewi.

36 Hawa hawawezi kufa tena, kwa maana wao ni kama malaika. Wao ni watoto wa Mungu, kwa sababu ni watoto wa ufufuo.

37 Hata Mose alidhihirisha kuwa wafu wanafufuka, kwa habari ya kile kichaka kilichokuwa kikiwaka moto bila kuteketea, alipomwita Bwana, ‘Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo.’

38 Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai, kwa kuwa kwake wote ni hai.”

39 Baadhi ya walimu wa sheria wakasema, “Mwalimu, umesema sawasawa kabisa!”

40 Baada ya hayo hakuna mtu aliyethubutu kumuuliza maswali tena.