Farisayo Mtaalamu wa Sheria Anamwuliza Yesu Swali
Mafarisayo wanafurahia kushindwa kwa Masadukayo, na mtaalamu wa sheria ambaye ni Farisayo anamwuliza Yesu swali kuhusu Sheria.
Katika ua wa hekalu. (Jumanne)
30 au 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 22:34–40
22:34 Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja. 35 Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema,
36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”
37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’
38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ 40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”
Marko 12:28–34
12:28 Mwalimu mmoja wa sheria akaja, akawasikia wakijadiliana. Akiona kwamba Yesu amewajibu vyema, naye akamuuliza, “Katika amri zote, ni ipi iliyo kuu?”
29 Yesu akajibu, “Amri iliyo kuu ndiyo hii: ‘Sikia ee Israeli. Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.
30 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.’
31 Ya pili ndiyo hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”
32 Yule mwalimu wa sheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, umejibu vyema kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye. 33 Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa akili zote na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama mtu anavyojipenda mwenyewe ni bora zaidi kuliko kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu zote.”
34 Yesu alipoona kwamba amejibu kwa busara, akamwambia, “Wewe hauko mbali na Ufalme wa Mungu.” Tangu wakati huo, hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumuuliza maswali tena.
Yesu Anawanyamazisha Adui Zake Kuhusu Mwana wa Daudi
Kwa furaha ya umati, Yesu anawanyamazisha adui zake kwa swali kali kuhusu jinsi Masiya alivyo mzao wa Daudi na bado ni Bwana wa Daudi.
Katika ua wa hekalu. (Jumanne)
Mathayo 22:41–46
22:41 Wakati Mafarisayo walikuwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza,
42 “Mnaonaje kuhusu Kristo? Yeye ni mwana wa nani?”
Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”
43 Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema,
44 “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’
45 Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?” 46 Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.
Marko 12:35–37
12:35 Yesu alipokuwa akifundisha Hekaluni, akauliza, “Imekuwaje walimu wa sheria wanasema kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi?
36 Kwa maana Daudi mwenyewe, akinena kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, alisema:
“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’
37 Kwa hiyo Daudi mwenyewe anamwita ‘Bwana.’ Awezaje basi yeye kuwa mwanawe?”
Ule umati wote wa watu wakamsikiliza kwa furaha.
Luka 20:41–44
20:41 Kisha Yesu akawaambia, “Imekuwaje basi wao husema Kristo ni Mwana wa Daudi?
42 Daudi mwenyewe anasema katika Kitabu cha Zaburi:
“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
43 hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’
44 Ikiwa Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ basi atakuwaje mwanawe?”