Kukataliwa kwa Kristo Kwatabiriwa

Unabii kuhusu kukataliwa kwa Kristo na kuinuliwa kwa kanisa lake hatimaye.

710 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Isaya 50:1–52:12

1 Hili ndilo asemalo Bwana:

“Iko wapi hati ya talaka ya mama yako

ambayo kwayo niliachana naye?

Au nimewauza ninyi kwa nani

miongoni mwa watu wanaonidai?

Kwa ajili ya dhambi zenu mliuzwa,

kwa sababu ya makosa, mama yenu aliachwa.

2 Nilipokuja, kwa nini hakuwepo hata mmoja?

Nilipoita, kwa nini hakuwepo hata mmoja wa kujibu?

Je, mkono wangu ni mfupi mno hata nisiweze kuwakomboa?

Je, mimi sina nguvu za kukuokoa?

Kwa kukemea tu naikausha bahari,

naigeuza mito ya maji kuwa jangwa;

samaki wake wanaoza kwa kukosa maji

na kufa kwa ajili ya kiu.

3 Ninalivika anga weusi na kufanya nguo ya gunia

kuwa kifuniko chake.”

4 Bwana Mwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa,

ili kujua neno limtegemezalo aliyechoka.

Huniamsha asubuhi kwa asubuhi,

huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye.

5 Bwana Mwenyezi amezibua masikio yangu,

nami sikuwa mwasi,

wala sikurudi nyuma.

6 Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao,

mashavu yangu wale wangʼoao ndevu zangu;

sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha

na kutemewa mate.

7 Kwa sababu Bwana Mwenyezi ananisaidia,

sitatahayarika.

Kwa hiyo nimekaza uso wangu kama jiwe la gumegume,

nami ninajua sitaaibika.

8 Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu.

Ni nani basi atakayeleta mashtaka dhidi yangu?

Tukabiliane uso kwa uso!

Mshtaki wangu ni nani?

Ni nani aliye mshtaki wangu?

9 Ni Bwana Mwenyezi anisaidiaye mimi.

Ni nani huyo atakayenihukumu?

Wote watachakaa kama vazi,

nondo watawala wawamalize.

10 Ni nani miongoni mwenu amchaye Bwana,

na kulitii neno la mtumishi wake?

Yeye atembeaye gizani,

yeye asiye na nuru,

na alitumainie jina la Bwana,

na amtegemee Mungu wake.

11 Lakini sasa, ninyi nyote mnaowasha mioto,

na kupeana mienge iwakayo ninyi kwa ninyi,

nendeni, tembeeni katika nuru ya moto wenu

na ya mienge mliyoiwasha.

Hili ndilo mtakalolipokea kutoka mkononi mwangu:

Mtalala chini kwa mateso makali.

51:1 “Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki

na mnaomtafuta Bwana:

Tazameni mwamba ambako mlichongwa,

na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa;

2 mwangalieni Abrahamu, baba yenu,

na Sara, ambaye aliwazaa.

Wakati nilipomwita alikuwa mmoja tu,

nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi.

3 Hakika Bwana ataifariji Sayuni,

naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote;

atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni,

nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya Bwana.

Shangwe na furaha zitakuwako ndani yake,

shukrani na sauti za kuimba.

4 “Nisikilizeni, watu wangu;

nisikieni, taifa langu:

Sheria itatoka kwangu;

haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa.

5 Haki yangu inakaribia mbio,

wokovu wangu unakuja,

nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa.

Visiwa vitanitegemea

na kungojea mkono wangu kwa matumaini.

6 Inueni macho yenu mbinguni,

mkaitazame dunia chini;

mbingu zitatoweka kama moshi,

dunia itachakaa kama vazi,

na wakazi wake kufa kama mainzi.

Bali wokovu wangu utadumu milele,

haki yangu haitakoma kamwe.

7 “Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa,

ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu:

Msiogope mashutumu ya wanadamu

wala msitiwe hofu na matukano yao.

8 Kwa maana nondo atawala kama vazi,

nao funza atawatafuna kama sufu.

Lakini haki yangu itadumu milele,

wokovu wangu kwa vizazi vyote.”

9 Amka, Amka! Jivike nguvu,

ewe mkono wa Bwana,

Amka, kama siku zilizopita,

kama vile vizazi vya zamani.

Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande,

uliyemchoma yule joka?

10 Si ni wewe uliyekausha bahari,

maji ya kilindi kikuu,

uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari

ili waliokombolewa wapate kuvuka?

11 Wale waliolipiwa fidia na Bwana watarudi.

Wataingia Sayuni wakiimba;

furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao.

Furaha na shangwe zitawapata,

huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka.

12 “Mimi, naam mimi,

ndimi niwafarijie ninyi.

Ninyi ni nani hata kuwaogopa

wanadamu wanaokufa,

wanadamu ambao ni majani tu,

13 kwamba mnamsahau Bwana Muumba wenu,

aliyezitanda mbingu

na kuiweka misingi ya dunia,

kwamba mnaishi katika hofu siku zote

kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu,

ambaye nia yake ni kuangamiza?

Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu?

14 Wafungwa waliojikunyata kwa hofu

watawekwa huru karibuni;

hawatafia kwenye gereza lao,

wala hawatakosa chakula.

15 Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume:

Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.

16 Nimeweka maneno yangu kinywani mwako

na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu:

Mimi niliyeweka mbingu mahali pake,

niliyeweka misingi ya dunia,

niwaambiaye Sayuni,

‘Ninyi ni watu wangu.’ ”

17 Amka, amka!

Simama, ee Yerusalemu,

wewe uliyekunywa kutoka mkono wa Bwana

kikombe cha ghadhabu yake,

wewe uliyekunywa mpaka kufikia machujo yake,

kikombe kile cha kunywea

kiwafanyacho watu kuyumbayumba.

18 Kati ya wana wote aliowazaa

hakuwepo hata mmoja wa kumwongoza,

kati ya wana wote aliowalea

hakuwepo hata mmoja wa kumshika mkono.

19 Majanga haya mawili yamekuja juu yako:

ni nani awezaye kukufariji?

Maangamizi, uharibifu, njaa na upanga:

ni nani awezaye kukutuliza?

20 Wana wako wamezimia,

wamelala kwenye mwanzo wa kila barabara,

kama swala aliyenaswa kwenye wavu.

Wamejazwa na ghadhabu ya Bwana

na makaripio ya Mungu wako.

21 Kwa hiyo sikiliza hili, wewe uliyeteswa,

uliyelewa, lakini si kwa mvinyo.

22 Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi wako,

Mungu wako, yeye ambaye huwatetea watu wake:

“Tazama, nimeondoa mkononi mwako

kikombe kilichokufanya uyumbayumbe;

kutoka kikombe hicho,

kikombe cha kunywa cha ghadhabu yangu,

kamwe hutakunywa tena.

23 Nitakiweka mikononi mwa watesi wako,

wale waliokuambia,

‘Anguka kifudifudi

ili tuweze kutembea juu yako.’

Ukaufanya mgongo wako kama ardhi,

kama njia yao ya kupita.”

52:1 Amka, amka, ee Sayuni,

jivike nguvu.

Vaa mavazi yako ya fahari,

ee Yerusalemu, mji mtakatifu.

Asiyetahiriwa na aliye najisi

hataingia kwako tena.

2 Jikungʼute mavumbi yako,

inuka, uketi kwenye kiti cha enzi, ee Yerusalemu.

Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako,

ee Binti Sayuni uliye mateka.

3 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:

“Mliuzwa pasipo malipo,

nanyi mtakombolewa bila fedha.”

4 Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi,

hatimaye, Ashuru wakawaonea.

5 “Basi sasa nina nini hapa?” asema Bwana.

“Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo,

nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,”

asema Bwana.

“Mchana kutwa

jina langu limetukanwa bila kikomo.

6 Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu;

kwa hiyo katika siku ile watajua

kwamba ndimi niliyetangulia kulisema.

Naam, ni mimi.”

7 Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema

ilivyo mizuri juu ya milima,

wale wanaotangaza amani,

wanaoleta habari njema,

wanaotangaza wokovu,

wauambiao Sayuni,

“Mungu wako anatawala!”

8 Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao,

pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha.

Wakati Bwana atakaporejea Sayuni,

wataliona kwa macho yao wenyewe.

9 Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja,

enyi magofu ya Yerusalemu,

kwa maana Bwana amewafariji watu wake,

ameikomboa Yerusalemu.

10 Mkono mtakatifu wa Bwana umefunuliwa

machoni pa mataifa yote,

nayo miisho yote ya dunia itaona

wokovu wa Mungu wetu.

11 Ondokeni, ondokeni, tokeni huko!

Msiguse kitu chochote kilicho najisi!

Tokeni kati yake mwe safi,

ninyi mchukuao vyombo vya Bwana.

12 Lakini hamtaondoka kwa haraka,

wala hamtakwenda kwa kukimbia;

kwa maana Bwana atatangulia mbele yenu,

Mungu wa Israeli atakuwa mlinzi nyuma yenu.