Kudhalilishwa na Kuinuliwa kwa Kristo Kunatabiriwa

Unabii kuhusu kudhalilishwa, mateso na kuinuliwa kwa Kristo.

710 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Isaya 52:13–53:12

13 Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima;

atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana.

14 Kama walivyokuwa wengi

walioshangazwa naye,

kwani uso wake ulikuwa umeharibiwa sana

zaidi ya mtu yeyote

na umbo lake kuharibiwa

zaidi ya mfano wa mwanadamu:

15 hivyo atayashangaza mataifa mengi,

nao wafalme watafunga vinywa vyao kwa sababu yake.

Kwa kuwa yale ambayo hawakuambiwa, watayaona,

nayo yale wasiyoyasikia, watayafahamu.

53:1 Ni nani aliyeamini ujumbe wetu,

na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?

2 Alikua mbele yake kama mche mwororo

na kama mzizi katika nchi kavu.

Hakuwa na uzuri wala utukufu wa kutuvutia kwake,

hakuwa na chochote katika sura yake cha kutufanya tumtamani.

3 Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,

mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.

Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

4 Hakika alichukua udhaifu wetu

na akajitwika huzuni zetu,

hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,

akapigwa sana naye, na kuteswa.

5 Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,

alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;

adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,

na kwa majeraha yake sisi tumepona.

6 Sisi sote, kama kondoo, tumepotea,

kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,

naye Bwana aliweka juu yake

maovu yetu sisi sote.

7 Alionewa na kuteswa,

hata hivyo hakufungua kinywa chake;

aliongozwa kama mwana-kondoo

apelekwaye machinjoni,

kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya,

hivyo hakufungua kinywa chake.

8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa.

Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake?

Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai,

alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu.

9 Wakamfanyia kaburi pamoja na waovu,

pamoja na matajiri katika kifo chake,

ingawa hakutenda jeuri,

wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

10 Lakini yalikuwa ni mapenzi ya Bwana

kumchubua na kumsababisha ateseke.

Ingawa Bwana amefanya maisha yake

kuwa sadaka ya hatia,

ataona uzao wake na kuishi siku nyingi,

nayo mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake.

11 Baada ya maumivu ya nafsi yake,

ataona nuru ya uzima na kuridhika;

kwa maarifa yake, mtumishi wangu mwenye haki

atawafanya wengi kuwa wenye haki,

naye atayachukua maovu yao.

12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu miongoni mwa wakuu,

naye atagawana nyara pamoja na wenye nguvu,

kwa sababu aliyamimina maisha yake hadi mauti,

naye alihesabiwa pamoja na wakosaji.

Kwa kuwa alichukua dhambi za wengi,

na kuwaombea wakosaji.

Ukuaji na Ushindi wa Kanisa Vyatabiriwa

Isaya 54

1 “Imba, ewe mwanamke tasa,

wewe ambaye kamwe hukuzaa mtoto;

paza sauti kwa kuimba, piga kelele kwa furaha,

wewe ambaye kamwe hukupata utungu;

kwa sababu watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi

kuliko wa mwanamke mwenye mume,”

asema Bwana.

2 “Panua mahali pa hema lako,

tandaza mapazia ya hema lako uyaeneze mbali,

wala usiyazuie;

ongeza urefu wa kamba zako,

imarisha vigingi vyako.

3 Kwa maana utaenea upande wa kuume

na upande wa kushoto;

wazao wako watayamiliki mataifa

na kukaa katika miji yao iliyoachwa ukiwa.

4 “Usiogope, wewe hutaaibika.

Usiogope aibu, wewe hutaaibishwa.

Wewe utasahau aibu ya ujana wako,

wala hutakumbuka tena mashutumu ya ujane wako.

5 Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako,

Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako,

yeye anaitwa Mungu wa dunia yote.

6 Bwana atakuita urudi

kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni;

kama mke aliyeolewa bado angali kijana

na kukataliwa,” asema Mungu wako.

7 “Kwa kitambo kidogo nilikuacha,

lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha.

8 Katika ukali wa hasira

nilikuficha uso wangu kwa kitambo,

lakini kwa fadhili za milele

nitakuwa na huruma juu yako,”

asema Bwana Mkombozi wako.

9 “Kwangu mimi jambo hili ni kama siku za Noa,

nilipoapa kuwa maji ya Noa kamwe hayatafunika tena dunia.

Hivyo sasa nimeapa sitawakasirikia ninyi,

kamwe sitawakemea tena.

10 Ijapotikisika milima, na vilima viondolewe,

hata hivyo upendo wangu usiokoma kwenu hautatikisika,

wala agano langu la amani halitaondolewa,”

asema Bwana, mwenye huruma juu yenu.

11 “Ewe mji uliyeteswa, uliyepigwa kwa dhoruba na usiyetulizwa,

nitakujenga kwa almasi, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi.

12 Nitafanya minara yako ya akiki,

malango yako kwa vito vingʼaavyo,

nazo kuta zako zote za vito vya thamani.

13 Watoto wako wote watafundishwa na Bwana,

nayo amani ya watoto wako itakuwa kuu.

14 Kwa haki utathibitika:

Kuonewa kutakuwa mbali nawe;

hutaogopa chochote.

Hofu itakuwa mbali nawe;

haitakukaribia wewe.

15 Kama mtu yeyote akikushambulia,

haitakuwa kwa ruhusa yangu;

yeyote akushambuliaye

atajisalimisha kwako.

16 “Tazama, ni mimi niliyemuumba mhunzi,

yeye afukutaye makaa kuwa moto,

na kutengeneza silaha inayofaa kwa kazi yake.

Tena ni mimi niliyemwambia mharabu

kufanya uharibifu mwingi.

17 Hakuna silaha itakayofanyizwa dhidi yako

itakayofanikiwa,

nawe utauthibitisha kuwa mwongo

kila ulimi utakaokushtaki.

Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana

na hii ndiyo haki yao itokayo kwangu,”

asema Bwana.

Baraka Nyingi za Injili

Utimilifu na ubora wa baraka za injili.

Isaya 55:1–56:8

1 “Njooni, ninyi nyote wenye kiu,

njooni kwenye maji;

nanyi ambao hamna fedha,

njooni, nunueni na mle!

Njooni, nunueni divai na maziwa

bila fedha na bila gharama.

2 Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula,

na kutaabikia kitu kisichoshibisha?

Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri,

nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono.

3 Tegeni sikio mje kwangu,

nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi.

Nitafanya agano la milele nanyi,

pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi.

4 Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa,

kiongozi na jemadari wa mataifa.

5 Hakika utaita mataifa usiyoyajua,

nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia,

kwa sababu ya Bwana Mungu wako,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli,

kwa maana amekutukuza.”

6 Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana;

mwiteni maadamu yu karibu.

7 Mtu mwovu na aiache njia yake,

na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.

Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu,

arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.

8 “Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,

wala njia zenu si njia zangu,”

asema Bwana.

9 “Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,

ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu

na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

10 Kama vile mvua na theluji

ishukavyo kutoka mbinguni,

nayo hairudi tena huko

bila kunywesha dunia

na kuichipusha na kuistawisha,

hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi

na mkate kwa mlaji,

11 ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu:

Halitanirudia tupu,

bali litatimiliza lile nililokusudia

na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.

12 Mtatoka nje kwa furaha

na kuongozwa kwa amani;

milima na vilima

vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu,

nayo miti yote ya shambani

itapiga makofi.

13 Badala ya kichaka cha miiba

itaota miti ya misunobari,

na badala ya michongoma

utaota mhadasi.

Hili litakuwa jambo la kumpatia Bwana jina,

kwa ajili ya ishara ya milele,

ambayo haitaharibiwa.”

56:1 Hili ndilo asemalo Bwana:

“Dumisheni haki

na mkatende lile lililo sawa,

kwa maana wokovu wangu u karibu

na haki yangu itafunuliwa upesi.

2 Amebarikiwa mtu yule atendaye hili,

mtu yule alishikaye kwa uthabiti,

yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi,

auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.”

3 Usimwache mgeni aambatanaye na Bwana aseme,

“Hakika Bwana atanitenga na watu wake.”

Usimwache towashi yeyote alalamike akisema,

“Mimi ni mti mkavu tu.”

4 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:

“Kwa matowashi washikao Sabato zangu,

ambao huchagua kile kinachonipendeza

na kulishika sana agano langu:

5 hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake

kumbukumbu na jina bora

kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike:

nitawapa jina lidumulo milele,

ambalo halitakatiliwa mbali.

6 Wageni wanaoambatana na Bwana

ili kumtumikia,

kulipenda jina la Bwana,

na kumwabudu yeye,

wote washikao Sabato bila kuinajisi

na ambao hushika sana agano langu:

7 hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu

na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala.

Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao

zitakubalika juu ya madhabahu yangu;

kwa maana nyumba yangu itaitwa

nyumba ya sala kwa mataifa yote.”

8 Bwana Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye

Waisraeli waliohamishwa:

“Bado nitawakusanya wengine kwao

zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.”