Ibada ya Sanamu Yakemewa

710 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Isaya 48

1 “Sikilizeni hili, ee nyumba ya Yakobo,

ninyi mnaoitwa kwa jina la Israeli,

na mnaotoka katika ukoo wa Yuda,

ninyi mnaoapa kwa jina la Bwana,

mnaomwomba Mungu wa Israeli,

lakini si katika kweli au kwa haki;

2 ninyi mnaojiita raiya wa mji mtakatifu,

na kumtegemea Mungu wa Israeli,

Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake:

3 Nilitoa unabii mambo ya kwanza tangu zamani,

kinywa changu kiliyatangaza na kuyafanya yajulikane;

kisha ghafula nikayatenda, nayo yakatokea.

4 Kwa kuwa nalijua jinsi ulivyokuwa mkaidi;

mishipa ya shingo yako ilikuwa chuma,

kipaji chako cha uso kilikuwa shaba.

5 Kwa hiyo nilikuambia mambo haya tangu zamani,

kabla hayajatokea nilikutangazia

ili usije ukasema,

‘Sanamu zangu zilifanya hayo;

kinyago changu cha mti na mungu wangu wa chuma aliyaamuru.’

6 Umesikia mambo haya; yaangalie hayo yote.

Je, hutayakubali?

“Kuanzia sasa na kuendelea nitakueleza mambo mapya,

juu ya mambo yaliyofichika usiyoyajua.

7 Yameumbwa sasa, wala si tangu zamani;

hukupata kuyasikia kabla ya siku ya leo.

Hivyo huwezi kusema,

‘Naam, niliyajua hayo.’

8 Hujayasikia wala kuyaelewa,

tangu zamani sikio lako halikufunguka.

Ninafahamu vyema jinsi ulivyo mdanganyifu,

uliitwa mwasi tangu kuzaliwa kwako.

9 Kwa ajili ya Jina langu mwenyewe

ninaichelewesha ghadhabu yangu,

kwa ajili ya sifa zangu nimeizuia isikupate,

ili nisije nikakukatilia mbali.

10 Tazama, nimekusafisha, ingawa si kama fedha,

nimekujaribu katika tanuru ya mateso.

11 Kwa ajili yangu mwenyewe,

kwa ajili yangu mwenyewe, nafanya hili.

Jinsi gani niliache Jina langu lichafuliwe?

Sitautoa utukufu wangu kwa mwingine.

12 “Ee Yakobo, nisikilize mimi,

Israeli, ambaye nimekuita:

Mimi ndiye;

mimi ndimi mwanzo na mwisho.

13 Mkono wangu mwenyewe uliweka misingi ya dunia,

nao mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu;

niziitapo, zote husimama pamoja.

14 “Kusanyikeni, ninyi nyote, msikilize:

Ni ipi miongoni mwa hizo sanamu

ambayo imetabiri vitu hivi?

Watu wa Bwana waliochaguliwa na kuungana

watatimiza kusudi lake dhidi ya Babeli;

mkono wa Mungu utakuwa dhidi ya Wakaldayo.

15 Mimi, naam, Mimi, nimenena;

naam, nimemwita yeye.

Nitamleta,

naye atafanikiwa katika lile nililomtuma.

16 “Nikaribieni na msikilize hili:

“Tangu tangazo la kwanza sikusema kwa siri;

wakati litokeapo, nitakuwako hapo.”

Sasa Bwana Mwenyezi amenituma,

kwa Roho wake.

17 Hili ndilo asemalo Bwana,

Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:

“Mimi ni Bwana, Mungu wako,

nikufundishaye ili upate faida,

nikuongozaye katika njia ikupasayo kuiendea.

18 Laiti ungesikiliza kwa makini maagizo yangu,

amani yako ingekuwa kama mto,

haki yako kama mawimbi ya bahari.

19 Wazao wako wangekuwa kama mchanga,

watoto wako kama chembe zake zisizohesabika;

kamwe jina lao lisingefutiliwa mbali,

wala kuangamizwa kutoka mbele zangu.”

20 Tokeni huko Babeli,

kimbieni kutoka kwa Wakaldayo!

Tangazeni hili kwa kelele za shangwe

na kulihubiri.

Lipelekeni mpaka miisho ya dunia;

semeni, “Bwana amemkomboa

mtumishi wake Yakobo.”

21 Hawakuona kiu alipowaongoza kupita jangwani;

alifanya maji yatiririke kutoka kwenye mwamba kwa ajili yao;

akapasua mwamba

na maji yakatoka kwa nguvu.

22 “Hakuna amani kwa waovu,” asema Bwana.

Masiya Anasema na Watu Wake

Isaya 49

1 Nisikilizeni, enyi visiwa, sikieni hili,

ninyi mataifa mlio mbali:

Kabla sijazaliwa, Bwana aliniita,

tangu kuzaliwa kwangu, amelitaja jina langu.

2 Akafanya kinywa changu kuwa kama upanga ulionolewa,

katika uvuli wa mkono wake akanificha;

akanifanya kuwa mshale uliosuguliwa,

na kunificha katika podo lake.

3 Akaniambia, “Wewe u mtumishi wangu,

Israeli, ambaye katika yeye

nitaonyesha utukufu wangu.”

4 Lakini nilisema, “Nimetumika bure,

nimetumia nguvu zangu bure bila faida.

Hata hivyo linalonistahili liko mkononi mwa Bwana,

nao ujira wangu uko kwa Mungu wangu.”

5 Sasa Bwana asema:

yeye aliyeniumba tumboni kuwa mtumishi wake,

kumrudisha tena Yakobo kwake

na kumkusanyia Israeli,

kwa maana nimepata heshima machoni pa Bwana,

naye Mungu wangu amekuwa nguvu yangu;

6 yeye asema:

“Je, ni jambo dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu

ili kurejeza makabila ya Yakobo,

na kuwarudisha wale Waisraeli niliowahifadhi?

Pia nitakufanya uwe nuru kwa ajili ya watu wa Mataifa,

ili upate kuleta wokovu wangu hata miisho ya dunia.”

7 Hili ndilo asemalo Bwana,

yeye Mkombozi na Aliye Mtakatifu wa Israeli,

kwake yeye aliyedharauliwa na kuchukiwa na taifa,

kwa mtumishi wa watawala:

“Wafalme watakuona na kusimama,

wakuu wataona na kuanguka kifudifudi,

kwa sababu ya Bwana, aliye mwaminifu,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, aliyekuchagua wewe.”

8 Hili ndilo asemalo Bwana:

“Wakati wangu uliokubalika nitakujibu,

nami katika siku ya wokovu nitakusaidia;

nitakuhifadhi, nami nitakufanya

kuwa agano kwa ajili ya watu,

ili kurudisha nchi

na kugawanyia urithi tena wale waliokuwa ukiwa,

9 kuwaambia mateka, ‘Tokeni nje,’

nao wale walio gizani, ‘Kuweni huru!’

“Watajilisha kando ya barabara

na kupata malisho yao juu ya kila kilima kilicho kitupu.

10 Hawataona njaa wala kuona kiu,

wala hari ya jangwani au jua halitawapiga.

Yeye mwenye huruma juu yao atawaonyesha njia,

na kuwaongoza kando ya chemchemi za maji.

11 Nitaifanya milima yangu yote kuwa barabara,

na njia kuu zangu zitainuliwa.

12 Tazama, watakuja kutoka mbali:

wengine kutoka kaskazini, wengine kutoka magharibi,

wengine kutoka nchi ya Sinimu.”

13 Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu;

furahi, ee dunia;

pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima!

Kwa maana Bwana anawafariji watu wake,

naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa.

14 Lakini Sayuni alisema, “Bwana ameniacha,

Bwana amenisahau.”

15 “Je, mama aweza kumsahau mtoto

aliyeko matitini mwake akinyonya,

wala asiwe na huruma

juu ya mtoto aliyemzaa?

Ingawa anaweza kusahau,

mimi sitakusahau wewe!

16 Tazama, nimekuchora kama muhuri

katika vitanga vya mikono yangu,

kuta zako zi mbele yangu daima.

17 Wana wako wanaharakisha kurudi,

nao wale waliokuteka wanaondoka kwako.

18 Inua macho yako ukatazame pande zote:

wana wako wote wanakusanyika na kukujia.

Kwa hakika kama vile niishivyo,

utawavaa wote kama mapambo,

na kujifunga nao kama bibi arusi,”

asema Bwana.

19 “Ingawa uliangamizwa na kufanywa ukiwa,

na nchi yako ikaharibiwa,

sasa nafasi itakuwa finyu kwa ajili ya watu wako,

nao wale waliokuangamiza watakuwa mbali sana.

20 Watoto waliozaliwa wakati wa msiba wako

bado watakuambia,

‘Mahali hapa ni finyu sana kwetu,

tupe eneo kubwa zaidi la kuishi.’

21 Ndipo utasema moyoni mwako,

‘Ni nani aliyenizalia hawa?

Nilikuwa nimefiwa, tena tasa;

nilikuwa nimehamishwa na kukataliwa.

Ni nani aliyewalea hawa?

Niliachwa peke yangu,

lakini hawa wametoka wapi?’ ”

22 Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“Tazama, nitawaashiria watu wa Mataifa,

nitainua bendera yangu kwa mataifa;

watawaleta wana wako mikononi yao,

na kuwabeba binti zenu juu ya mabega yao.

23 Wafalme watakuwa baba zenu wa kuwalea,

na malkia wao watakuwa mama zenu wa kuwalea.

Watasujudu mbele yako nyuso zao zikigusa ardhi;

wataramba mavumbi yaliyo miguuni mwako.

Ndipo utajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana;

wale wanaonitumaini mimi hawataaibika.”

24 Je, nyara zaweza kuchukuliwa kutoka kwa mashujaa wa vita,

au mateka kuokolewa kutoka kwa watu wakali?

25 Lakini hili ndilo asemalo Bwana:

“Naam, mateka watachukuliwa kutoka kwa mashujaa,

na nyara zitapokonywa kutoka kwa watu wakali.

Nitashindana na wale wanaoshindana nawe,

nami nitawaokoa watoto wako.

26 Nitawafanya wale wanaokuonea kula nyama yao wenyewe,

watalewa kwa damu yao wenyewe,

kama vile kwa mvinyo.

Ndipo wanadamu wote watajua

ya kuwa Mimi, Bwana, ni Mwokozi wako,

Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.”