Sehemu ya 11: Utawala wa Yothamu
Ufalme wa Yuda
758 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
32 Katika mwaka wa pili wa utawala wa Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli, Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala.
1 Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki. 2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya, lakini tofauti na yeye, hakuingilia huduma za hekaluni mwa Bwana. Lakini hata hivyo, watu wakaendelea na desturi zao mbaya.
35 Hata hivyo, mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu la Bwana.
1 Neno la Bwana lilimjia Mika, Mmoreshethi, wakati wa utawala wa Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda; ufunuo aliouona kuhusu Samaria na Yerusalemu.
2 Sikieni, enyi mataifa, enyi nyote,
sikilizeni, ee dunia na wote mliomo ndani yake,
ili Bwana Mwenyezi ashuhudie dhidi yenu,
Bwana kutoka Hekalu lake takatifu.
3 Tazama! Bwana anakuja kutoka mahali pake;
anashuka na kukanyaga
mahali palipoinuka juu pa dunia.
4 Milima inayeyuka chini yake
na mabonde yanagawanyika
kama nta mbele ya moto,
kama maji yatiririkayo kasi
kwenye mteremko.
5 Yote haya ni kwa sababu ya kosa la Yakobo,
ni kwa sababu ya dhambi za nyumba ya Israeli.
Kosa la Yakobo ni lipi?
Je, sio Samaria?
Je, mahali pa juu pa Yuda pa kuabudia miungu ni nini?
Je, sio Yerusalemu?
6 “Kwa hiyo nitaufanya Samaria kuwa lundo la kokoto,
mahali pa kuotesha mizabibu.
Nitayamwaga mawe yake katika bonde
na kuacha wazi misingi yake.
7 Sanamu zake zote
zitavunjwa vipande vipande;
zawadi zake zote za Hekalu
zitachomwa kwa moto;
nitaharibu vinyago vyake vyote.
Kwa kuwa alikusanya zawadi zake
kutokana na ujira wa kahaba,
nazo zitatumika tena
kulipa mishahara ya kahaba.”
8 Kwa ajili ya hili nitalia na kuomboleza;
nitatembea bila viatu na tena uchi.
Nitabweka kama mbweha
na kuomboleza kama bundi.
9 Kwa sababu jeraha lake halitibiki;
limekuja Yuda.
Limefika hasa kwenye lango la watu wangu,
hata Yerusalemu kwenyewe.
10 Usiliseme hili huko Gathi;
usilie hata kidogo.
Huko Beth-le-Afra
gaagaa mavumbini.
11 Piteni mkiwa uchi na wenye aibu,
ninyi mkaao Shafiri.
Wale waishio Saanani
hawatatoka nje.
Beth-Eseli iko katika maombolezo;
kinga yake imeondolewa kwako.
12 Wale waishio Marothi wanagaagaa kwa maumivu
wakingoja msaada,
kwa sababu maangamizi yamekuja
kutoka kwa Bwana,
hata katika lango la Yerusalemu.
13 Enyi mkaao Lakishi,
fungeni farasi kwenye magari ya vita.
Mlikuwa chanzo cha dhambi
kwa Binti Sayuni,
kwa kuwa makosa ya Israeli
yalikutwa kwako.
14 Kwa hiyo utaipa Moresheth-Gathi
zawadi za kuagana.
Mji wa Akzibu utaonyesha wazi udanganyifu
kwa wafalme wa Israeli.
15 Nitawaleteeni atakayewashinda
ninyi mnaoishi Maresha.
Yeye aliye utukufu wa Israeli
atakuja Adulamu.
16 Nyoeni nywele zenu katika kuomboleza
kwa ajili ya watoto wenu mnaowafurahia;
jifanyieni upara kama tai,
kwa kuwa watawaacha
na kwenda uhamishoni.
2:1 Ole kwa wale wapangao uovu,
kwa wale wafanyao shauri la hila vitandani mwao!
Kunapopambazuka wanalitimiza
kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza.
2 Wanatamani mashamba na kuyakamata,
pia nyumba na kuzichukua.
Wanamlaghai mwanaume nyumba yake,
mwanadamu mwenzake urithi wake.
3 Kwa hiyo, Bwana asema:
“Ninapanga maangamizi dhidi ya watu hawa,
ambayo hamwezi kujiokoa wenyewe.
Hamtatembea tena kwa majivuno,
kwa kuwa utakuwa ni wakati wa maafa.
4 Siku hiyo watu watawadhihaki,
watawafanyia mzaha
kwa wimbo huu wa maombolezo:
‘Tumeangamizwa kabisa;
mali ya watu wangu imegawanywa.
Ameninyangʼanya!
Ametoa mashamba yetu kwa wasaliti.’ ”
5 Kwa hiyo hutakuwa na yeyote katika kusanyiko la Bwana
wa kugawanya mashamba kwa kura.
6 Manabii wao husema, “Usitabiri.
Usitabiri kuhusu vitu hivi;
aibu haitatupata.”
7 Je, ingesemwa, ee nyumba ya Yakobo:
“Je, Roho wa Bwana amekasirika?
Je, yeye hufanya vitu kama hivyo?”
“Je, maneno yangu hayamfanyii mema
yeye ambaye njia zake ni nyofu?
8 Siku hizi watu wangu wameinuka
kama adui.
Unawavua joho la kitajiri wale wanaopita
pasipo kujali,
kama watu warudio kutoka vitani.
9 Unawahamisha wanawake wa watu wangu
kutoka kwenye nyumba zao za kupendeza.
Unaondoa baraka yangu
kwa watoto wao milele.
10 Inuka, nenda zako!
Kwa maana hapa sio mahali pako pa kupumzikia,
kwa sababu pametiwa unajisi,
pameharibiwa, wala hapatengenezeki tena.
11 Ikiwa mwongo na mdanganyifu atakuja na kusema,
‘Nitawatabiria divai na pombe kwa wingi,’
angekuwa ndiye nabii
anayekubalika na watu hawa!
12 “Hakika nitawakusanya ninyi nyote, ee Yakobo,
Hakika nitawaleta pamoja mabaki ya Israeli.
Nitawaleta pamoja kama kondoo ndani ya zizi,
kama kundi kwenye malisho yake,
mahali hapa patakuwa na msongamano wa watu.
13 Yeye afunguaye njia atawatangulia;
watapita kwenye lango na kutoka nje.
Mfalme wao atawatangulia,
Bwana atakuwa kiongozi.”
3 Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu la Bwana na kufanya kazi kubwa kwenye ukuta katika kilima cha Ofeli. 4 Akajenga miji katika vilima vya Yuda pamoja na ngome na minara mwituni.
5 Yothamu akafanya vita na mfalme wa Waamoni na kumshinda. Mwaka ule Waamoni wakamlipa talanta 100 za fedha, kori 10,000 za ngano na kori 10,000 za shayiri. Waamoni wakamletea kiasi hicho hicho mwaka wa pili na wa tatu.
6 Yothamu akaendelea kuwa na nguvu kwa sababu alienenda kwa ukamilifu mbele za Bwana Mungu wake.
7 Matukio mengine ya utawala wa Yothamu, pamoja na vita vyake vyote na vitu vingine alivyofanya, vimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda. 8 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. 9 Yothamu akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Ahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.
37 (Katika siku hizo, Bwana akaanza kuwatuma Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia dhidi ya Yuda.)
33 Alikuwa na miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki. 34 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya.
36 Matukio mengine ya utawala wa Yothamu na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda?
38 Yothamu akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi, mji wa baba zake. Naye Ahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.
Ufalme wa Israeli
Utawala wa Peka
27 Katika mwaka wa hamsini na mbili wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Peka mwana wa Remalia akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, naye alitawala miaka ishirini. 28 Akafanya maovu machoni pa Bwana. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
29 Wakati wa utawala wa Peka mfalme wa Israeli, Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru alikuja na kuteka Iyoni, Abel-Beth-Maaka, Yanoa, Kedeshi na Hazori. Akateka miji ya Gileadi na Galilaya, pamoja na nchi yote ya Naftali, na kuwahamishia watu wote Ashuru.