Sehemu ya 12: Utawala wa Ahazi

Ufalme wa Yuda

Tabia ya Ahazi

742 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 16:1–4

1 Katika mwaka wa kumi na saba wa utawala wa Peka mwana wa Remalia, Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala. 2 Ahazi alikuwa na miaka ishirini alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na sita. Tofauti na Daudi baba yake, hakufanya yaliyo mema machoni pa Bwana, Mungu wake. 3 Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, na hata akamtoa mwanawe kafara katika moto, akifuata njia za machukizo za mataifa ambayo Bwana alikuwa ameyafukuza mbele ya Waisraeli. 4 Akatoa kafara na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu, juu ya vilima, na chini ya kila mti uliotanda.

Resini na Peka Wanaivamia Yuda

2 Wafalme 16:5

5 Kisha Resini mfalme wa Aramu na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli wakaondoka kwenda kupigana dhidi ya Yerusalemu na kumzunguka Ahazi kwa jeshi, lakini hawakuweza kumshinda.

Isaya 7–8

1 Wakati Ahazi mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, Mfalme Resini wa Aramu, na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walipanda kupigana dhidi ya Yerusalemu, lakini hawakuweza kuushinda.

2 Wakati huu nyumba ya Daudi iliambiwa, “Aramu wameungana na Efraimu.” Kwa hiyo mioyo ya Ahazi na watu wake ilitikiswa, kama miti ya msituni inavyotikiswa na upepo.

3 Ndipo Bwana akamwambia Isaya, “Toka uende, wewe na mwanao Shear-Yashubu, mkutane na Ahazi huko mwisho wa mfereji wa Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo Shamba la Dobi. 4 Mwambie, ‘Uwe mwangalifu, utulie na usiogope. Usife moyo kwa ajili ya watu hawa wawili walio kama visiki vya kuni vifukavyo moshi, kwa ajili ya hasira kali ya Resini na Aramu na ya mwana wa Remalia. 5 Aramu, Efraimu na mwana wa Remalia wamepanga shauri baya ili wakuangamize, wakisema, 6 “Tuishambulie Yuda, naam, tuirarue vipande vipande na kuigawa miongoni mwetu, na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme juu yake.” 7 Lakini Bwana Mwenyezi asema hivi:

“ ‘Jambo hili halitatendeka,

halitatokea,

8 kwa kuwa kichwa cha Aramu ni Dameski,

na kichwa cha Dameski ni Resini peke yake.

Katika muda wa miaka sitini na mitano,

Efraimu atakuwa ameharibiwa

kiasi kwamba hataweza tena kuwa taifa.

9 Kichwa cha Efraimu ni Samaria,

na kichwa cha Samaria

ni mwana wa Remalia peke yake.

Kama hamtasimama thabiti katika imani yenu,

hamtaimarika kamwe.’ ”

10 Bwana akasema na Ahazi tena, 11 “Mwombe Bwana Mungu wako ishara, iwe kwenye vina virefu sana, au kwenye vimo virefu sana.”

12 Lakini Ahazi akasema, “Sitaomba; sitamjaribu Bwana.”

13 Ndipo Isaya akasema, “Sikia sasa, ewe nyumba ya Daudi! Je, haitoshi kujaribu uvumilivu wa wanadamu? Je, mtaujaribu uvumilivu wa Mungu wangu pia? 14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli. 15 Atakula jibini na asali atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua mema. 16 Lakini kabla mtoto hajajua kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa. 17 Bwana ataleta juu yako, juu ya watu wako, na juu ya nyumba ya baba yako wakati ambao haujawahi kuwako tangu Efraimu alipojitenga na Yuda: yeye atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”

18 Katika siku ile Bwana atawapigia filimbi mainzi kutoka vijito vya mbali vya Misri, na nyuki kutoka nchi ya Ashuru. 19 Wote watakuja na kukaa kwenye mabonde yenye miteremko, na kwenye nyufa za miamba, kwenye vichaka vyote vyenye miiba, na kwenye mashimo yote ya maji. 20 Katika siku ile Bwana atatumia wembe ulioajiriwa kutoka ngʼambo ya Mto, yaani mfalme wa Ashuru, kunyoa nywele za kichwa chako na malaika ya miguu yako, na kuziondoa ndevu zako pia. 21 Katika siku ile, mtu atahifadhi hai ndama mmoja na kondoo wawili. 22 Kwa ajili ya wingi wa maziwa watakayotoa, atapata jibini ya kula. Wote watakaobakia katika nchi watakula jibini na asali. 23 Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli 1,000 za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu. 24 Watu watakwenda huko wakiwa na upinde na mshale, kwa maana nchi itafunikwa na michongoma na miiba. 25 Kuhusu vilima vyote vilivyokuwa vikilimwa kwa jembe, hamtakwenda huko tena kwa ajili ya hofu ya michongoma na miiba. Patakuwa mahali ambapo ngʼombe wataachiwa huru, na kondoo kukimbia kimbia.

8:1 Bwana akaniambia, “Chukua gombo kubwa, uandike juu yake kwa kalamu ya kawaida jina: Maher-Shalal-Hash-Bazi. 2 Nami nitawaita kuhani Uria, na Zekaria mwana wa Yeberekia kama mashahidi wangu waaminifu.”

3 Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mwana. Kisha Bwana akaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi. 4 Kabla mtoto hajaweza kusema ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.”

5 Bwana akasema nami tena:

6 “Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yatiririkayo taratibu

wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia,

7 kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao

mafuriko makubwa ya Mto:

yaani mfalme wa Ashuru na fahari yake yote.

Yatafurika juu ya mifereji yake yote,

yatamwagikia juu ya kingo zake zote,

8 na kufika hadi Yuda, yakizunguka kwa kasi juu yake,

yakipita katikati na yakifika hadi shingoni.

Mabawa yake yaliyokunjuliwa

yatafunika upana wa nchi yako,

Ee Imanueli!”

9 Inueni kilio cha vita, enyi mataifa,

na mkavunjwevunjwe!

Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali.

Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!

Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!

10 Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa;

fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa,

kwa maana Mungu yu pamoja nasi.

11 Bwana alisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema:

12 “Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina,

usiogope kile wanachokiogopa,

wala usikihofu.

13 Bwana Mwenye Nguvu Zote ndiye peke yake

ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu,

ndiye peke yake utakayemwogopa,

ndiye peke yake utakayemhofu,

14 naye atakuwa mahali patakatifu;

lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa

jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa

na mwamba wa kuwaangusha.

Kwa watu wa Yerusalemu,

atakuwa mtego na tanzi.

15 Wengi wao watajikwaa;

wataanguka na kuvunjika,

watategwa na kunaswa.”

16 Funga ushuhuda na kutia muhuri sheria

miongoni mwa wanafunzi wangu.

17 Nitamngojea Bwana,

ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake.

Nitaliweka tumaini langu kwake.

18 Niko hapa, pamoja na watoto ambao Bwana amenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote, anayeishi juu ya Mlima Sayuni.

19 Wakati watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunongʼona na kunungʼunika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai? 20 Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko. 21 Watazunguka katika nchi yote, wakiwa na dhiki na njaa. Watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, nao, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao. 22 Kisha wataangalia duniani na kuona tu dhiki na giza, hofu na huzuni tupu, nao watasukumiwa kwenye giza nene kabisa.