Israeli Bila Mfalme Baada ya Kifo cha Yeroboamu wa Pili
776 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Sikieni neno la Bwana, enyi Waisraeli,
kwa sababu Bwana analo shtaka
dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi:
“Hakuna uaminifu, hakuna upendo,
hakuna kumjua Mungu katika nchi.
2 Kuna kulaani tu, uongo na uuaji,
wizi na uzinzi,
bila kuwa na mipaka,
nao umwagaji damu mmoja
baada ya mwingine.
3 Kwa sababu hii nchi huomboleza,
wote waishio ndani mwake wanadhoofika,
wanyama wa kondeni, ndege wa angani
na samaki wa baharini wanakufa.
4 “Lakini mtu awaye yote na asilete shtaka,
mtu yeyote na asimlaumu mwenzake,
kwa maana watu wako ni kama wale
waletao mashtaka dhidi ya kuhani.
5 Unajikwaa usiku na mchana,
nao manabii hujikwaa pamoja nawe.
Kwa hiyo nitamwangamiza mama yako:
6 watu wangu wanaangamizwa
kwa kukosa maarifa,
“Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa,
mimi nami nitakukataa wewe
usiwe kuhani kwangu mimi;
kwa kuwa umeacha kuijali sheria ya Mungu wako
mimi nami sitawajali watoto wako.
7 Kadiri makuhani walivyoongezeka,
ndivyo walivyozidi kutenda dhambi dhidi yangu,
walibadilisha utukufu wao kwa kitu cha aibu.
8 Hujilisha dhambi za watu wangu
na kupendezwa na uovu wao.
9 Hata itakuwa: Kama walivyo watu,
ndivyo walivyo makuhani.
Nitawaadhibu wote wawili kwa ajili ya njia zao
na kuwalipa kwa matendo yao.
10 “Watakula lakini hawatashiba;
watajiingiza katika ukahaba
lakini hawataongezeka,
kwa sababu wamemwacha Bwana
na kujiingiza wenyewe
11 katika ukahaba,
divai ya zamani na divai mpya,
ambavyo huondoa ufahamu
12 wa watu wangu.
Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti
nao hujibiwa na fimbo ya mti.
Roho ya ukahaba imewapotosha,
hawana uaminifu kwa Mungu wao.
13 Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima
na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima,
chini ya mialoni, milibua na miela,
ambako kuna vivuli vizuri.
Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba
na wake za wana wenu uzinzi.
14 “Sitawaadhibu binti zenu wakati
wanapogeukia ukahaba,
wala wake za wana wenu
wanapofanya uzinzi,
kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya
na kutambikia pamoja na makahaba
wa mahali pa kuabudia miungu:
watu wasiokuwa na ufahamu
wataangamia!
15 “Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli,
Yuda naye asije akawa na hatia.
“Usiende Gilgali,
usipande kwenda Beth-Aveni
Wala usiape,
‘Hakika kama Bwana aishivyo!’
16 Waisraeli ni wakaidi,
kama mtamba wa ngʼombe ambaye ni mkaidi.
Ni jinsi gani basi Bwana anaweza kuwachunga
kama wana-kondoo
katika shamba la majani?
17 Efraimu amejiunga na sanamu,
ondokana naye!
18 Hata wakati wamemaliza vileo vyao
wanaendelea na ukahaba wao,
watawala wao hupenda sana
njia za aibu.
19 Kisulisuli kitawafagilia mbali
na dhabihu zao zitawaletea aibu.
Utawala wa Zekaria 773 KK
8 Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Zekaria mwana wa Yeroboamu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, naye akatawala miezi sita. 9 Akafanya maovu machoni pa Bwana, kama baba zake walivyofanya. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
10 Shalumu mwana wa Yabeshi akafanya shauri baya dhidi ya Zekaria. Akamshambulia mbele ya watu, akamuua na kuingia mahali pake kuwa mfalme. 11 Matukio mengine ya utawala wa Zekaria yameandikwa kwenye kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli. 12 Kwa hiyo neno la Bwana lililonenwa kwa Yehu likatimia, kwamba, “Wazao wako wataketi juu ya kiti cha enzi cha Israeli hadi kizazi cha nne.”
Utawala wa Shalumu 772 KK
13 Shalumu mwana wa Yabeshi akawa mfalme katika mwaka wa thelathini na tisa wa Uzia mfalme wa Yuda, naye akatawala katika Samaria kwa mwezi mmoja. 14 Kisha Menahemu mwana wa Gadi akaenda kutoka Tirsa mpaka Samaria. Akamshambulia Shalumu mwana wa Yabeshi huko Samaria, akamuua na kuingia mahali pake kuwa mfalme.
15 Matukio mengine ya utawala wa Shalumu, na mauaji aliyoyafanya, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.
Utawala wa Menahemu
16 Wakati ule, akianzia Tirsa, Menahemu alishambulia Tifsa na kila mtu ndani yake, na wale waliokuwa maeneo jirani, kwa sababu walikataa kufungua malango yao. Akaiangamiza Tifsa yote, na kuwapasua matumbo wanawake wote wenye mimba.
17 Katika mwaka wa thelathini na tisa wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi akawa mfalme wa Israeli, akatawala huko Samaria kwa miaka kumi. 18 Akatenda maovu machoni pa Bwana. Katika wakati wa utawala wake wote, hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati ambazo alisababisha Israeli kuzitenda.
19 Kisha Pulu mfalme wa Ashuru akaishambulia Israeli. Menahemu mfalme wa Israeli akampa talanta elfu moja za fedha ili amsaidie na kumwezesha katika utawala wake. 20 Menahemu akatoza fedha hizi kwa nguvu kutoka kwa Israeli. Kila mtu tajiri alilazimika kuchanga shekeli hamsini za fedha ambazo alipewa mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akajiondoa na hakuendelea kuikalia nchi.
21 Matukio mengine ya utawala wa Menahemu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? 22 Menahemu akalala pamoja na baba zake. Naye Pekahia mwanawe akawa mfalme baada yake.
Utawala wa Pekahia 768 KK
23 Katika mwaka wa hamsini wa utawala wa Azaria mfalme wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu akawa mfalme wa Israeli huko Samaria, akatawala miaka miwili. 24 Pekahia akafanya uovu machoni pa Bwana. Hakuziacha dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda. 25 Mmoja wa maafisa wake wakuu, Peka mwana wa Remalia, akafanya shauri baya dhidi yake. Akachukua watu hamsini wa Gileadi pamoja naye, akamuua Pekahia, pamoja na Argobu na Aria, katika ngome ya jumba la kifalme huko Samaria. Kwa hiyo Peka akamuua Pekahia, naye akaingia mahali pake kuwa mfalme.
26 Matukio mengine ya utawala wa Pekahia na yote aliyoyafanya yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli.