Sheria ni duni kuliko agano la injili

Paulo anaendelea na himizo lake kwa kutumia mfano kutoka Agano la Kale, akionyesha kwamba Sheria ni duni kuliko agano la injili.

51 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Wagalatia 4:21–31

21 Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je, hamjui sheria inavyosema? 22 Kwa maana imeandikwa kwamba Abrahamu alikuwa na wana wawili, mmoja wa mwanamke mtumwa na wa pili wa mwanamke huru. 23 Lakini, mtoto wa mwanamke mtumwa alizaliwa kwa mapenzi ya mwili, na yule mwingine wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.

24 Mambo haya yanaweza kuchukuliwa kama mfano. Kwa maana hao wanawake wawili ni mfano wa maagano mawili: Agano la kwanza, ni lile lililofanyika katika Mlima Sinai, lizaalo watoto wa utumwa. Hili ndilo huyo Hagari. 25 Basi Hagari anawakilisha Mlima Sinai ulioko Arabuni, na unafanana na Yerusalemu ya sasa ambayo iko utumwani pamoja na watoto wake. 26 Lakini Yerusalemu wa juu ni huru, nayo ndiye mama yetu. 27 Kwa maana imeandikwa:

“Furahi, ewe mwanamke tasa,

wewe usiyezaa;

paza sauti, na kuimba kwa furaha,

wewe usiyepatwa na utungu wa kuzaa;

kwa maana watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi

kuliko wa mwanamke mwenye mume.”

28 Basi, sisi ndugu zangu, ni kama Isaki, tu watoto wa ahadi. 29 Lakini, kama vile ilivyokuwa siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo hata sasa. 30 Lakini Maandiko yasemaje? “Mwondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe, kwa sababu mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwana wa aliye huru.” 31 Kwa hiyo ndugu zangu, sisi si watoto wa mwanamke mtumwa, bali wa yule aliye huru.

Wana Wajibu wa Kuitii Sheria Yote

Paulo anasisitiza kwamba wote wanaotegemea Sheria ya Wayahudi kwa ajili ya wokovu wanajinyima baraka ya utaratibu wa imani ya Mkristo, na wanakuwa na wajibu wa kuitii Sheria yote. Anawahimiza kuonyesha sifa njema na fadhila zinazotakiwa na dini ya kiroho ya injili. Wanapaswa kujihadhari na maovu ya kimaadili yaliyokatazwa na Sheria ya Mose, na kuzuia roho ya majivuno na tamaa ya kujitukuza zinazosababisha uchokozi na wivu mwingi miongoni mwa Wakristo.

Wagalatia 5

1 Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.

2 Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia chochote. 3 Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote. 4 Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu. 5 Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki. 6 Kwa maana ndani ya Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.

7 Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? 8 Ushawishi wa namna hiyo haukutokana na yule anayewaita. 9 “Chachu kidogo huchachua donge zima.” 10 Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. 11 Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. 12 Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!

13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 15 Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.

16 Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho. 26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.

Paulo Anahimiza Upendo wa Mkristo

Paulo anawahimiza kuwa na upendo wa Mkristo. Anaweka msingi wa himizo hilo katika udhaifu wao wenyewe, katika haja ya kuchunguza matendo yao, kwa kuwa wote watatoa hesabu kuhusu matendo hayo, na katika wajibu wa kuchangia kuendeleza huduma na kutimiza mahitaji ya wanadamu wote, hasa Wakristo wenzetu.

Wagalatia 6:1–10

1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo. 3 Kama mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. 4 Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine. 5 Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe. 6 Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

Paulo Ana Alama za Yesu

Paulo anamalizia kwa kuwakumbusha Wagalatia kwamba wale wenye bidii kwa ajili ya dini ya Kiyahudi hawakuishika Sheria, na walitaka wale waliowageuza waingie katika dini hiyo watahiriwe kwa kusudi moja tu: wao wenyewe waepuke mateso. Kwa upande wake, Paulo anatangaza kwamba hawezi kuongozwa na nia hizo za ubinafsi, kwa maana anabeba mwilini mwake alama za mateso aliyopata kwa ajili ya Bwana Yesu. Anashuhudia kwamba utakatifu pekee ndio wenye thamani mbele za Mungu. Anaomba baraka kwa ajili ya kanisa.

Wagalatia 6:11–18

11 Angalieni herufi kubwa nitumiazo ninapowaandikia kwa mkono wangu mwenyewe!

12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Kristo. 13 Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu. 14 Mungu apishie mbali nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. 15 Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! 16 Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, na juu ya Israeli wa Mungu.

17 Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu.

18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.