Waberoya Wako Tayari Kuipokea Injili
Kutoka Thesalonike kwenda Beroya. Sababu zinazowafanya Waberoya wawe na utayari wa kuipokea injili.
51 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
10 Usiku ule ule, wale ndugu walioamini wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi. 11 Hawa Waberoya walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli. 12 Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume wa Kiyunani wa tabaka la juu.
13 Lakini wale Wayahudi wa Thesalonike waliposikia kuwa Paulo anahubiri neno la Mungu huko Beroya, wakaenda huko ili kuwashawishi watu na kuwachochea. 14 Mara hiyo, wale ndugu wakamsafirisha Paulo hadi pwani, lakini Sila na Timotheo wakabaki Beroya.
Paulo Anawahubiria Wanafalsafa huko Athene
Akiwaacha Sila na Timotheo huko Beroya, Paulo anaendelea kwenda Athene, ambako anawahubiria wanafalsafa na wanafunzi.
15 Wale waliomsindikiza Paulo wakaenda naye mpaka Athene, kisha wakarudi Beroya wakiwa na maagizo kutoka kwa Paulo kuhusu Sila na Timotheo kwamba wamfuate upesi iwezekanavyo.
16 Paulo alipokuwa akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona vile mji huo ulivyojaa sanamu. 17 Hivyo akahojiana kwenye sinagogi na Wayahudi pamoja na Wayunani waliomcha Mungu, na pia sokoni kila siku na watu aliopatana nao huko. 18 Kisha baadhi ya Waepikureo na Wastoiko wenye falsafa wakakutana naye. Baadhi yao wakasema, “Je, huyu mpayukaji anajaribu kusema nini?” Wengine wakasema, “Inaonekana anasema habari za miungu ya kigeni.” Walisema haya kwa sababu Paulo alikuwa anahubiri habari njema kuhusu Yesu na ufufuo wa wafu. 19 Hivyo wakamchukua na kumleta kwenye mkutano wa Areopago, walikomwambia, “Je, tunaweza kujua mafundisho haya mapya unayofundisha ni nini? 20 Wewe unaleta mambo mapya masikioni mwetu, hivyo tungetaka kujua maana yake ni nini.” 21 (Waathene na wageni wote walioishi humo hawakutumia muda wao kufanya chochote kingine isipokuwa kueleza au kusikia mambo mapya).
22 Ndipo Paulo akasimama katikati ya Areopago akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana. 23 Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: Kwa Mungu Asiyejulikana. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.
24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’
29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. 30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”
32 Waliposikia habari za ufufuo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.” 33 Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao. 34 Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao alikuwepo Dionisio, Mwareopago na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari na wengine wengi.
Paulo Anafanya Kazi Kujipatia Riziki huko Korintho
Kutoka Athene Paulo anaendelea kwenda Korintho, ambako analazimika kufanya kazi ili kujipatia riziki. Sila na Timotheo wanajiunga naye huko Korintho.
1 Baada ya haya, Paulo akaondoka Athene akaenda Korintho. 2 Huko akakutana na Myahudi mmoja jina lake Akila, mwenyeji wa Ponto, ambaye alikuwa amewasili karibuni kutoka Italia pamoja na mkewe Prisila, kwa sababu Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo akaenda kuwaona, 3 naye kwa kuwa alikuwa mtengeneza mahema kama wao, akakaa na kufanya kazi pamoja nao. 4 Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi, akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani.
5 Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo