Paulo Anawaandikia Wathesalonike
Paulo anawaandikia Wathesalonike barua yake ya kwanza ili kuwaimarisha katika imani walipokuwa wakishambuliwa na Wayahudi wasioamini, kwa kusisitiza uthibitisho wa ukweli wa Ukristo.
51 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Paulo Anawasalimu Wathesalonike
Utangulizi na salamu.
1 Paulo, Silvano na Timotheo:
Kwa kanisa la Wathesalonike, ninyi mlio ndani ya Mungu Baba yetu na ndani ya Bwana Yesu Kristo:
Neema iwe kwenu na amani.
2 Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima. 3 Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Yesu Kristo.
4 Ndugu zetu mpendwao na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua,
Hoja ya Kwanza ya Paulo: Karama za Miujiza
Paulo anatoa hoja yake ya kwanza kuhusu ukweli wa Ukristo kutokana na karama za miujiza za Roho Mtakatifu. Anafurahia ushikamanifu wao thabiti kwa imani ya Mkristo, na anaupongeza.
5 kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho Mtakatifu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda katikati yenu kwa ajili yenu. 6 Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho Mtakatifu. 7 Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waumini wote katika Makedonia na Akaya. 8 Kwa maana kutoka kwenu neno la Bwana limesikika, si katika Makedonia na Akaya tu, bali pia imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali kiasi kwamba hatuna haja ya kusema lolote kwa habari yake. 9 Kwa maana watu wa maeneo hayo wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli 10 na ili kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu: yaani, Yesu, yeye aliyetuokoa kutoka ghadhabu inayokuja.
Maisha ya Wahubiri Yanathibitisha Ukweli wa Injili
Kwa kuonyesha tabia, mwenendo na mateso ya wahubiri wa injili, Paulo anathibitisha ukweli wake. Anamshukuru Mungu kwamba Wathesalonike waliipokea si kama mfumo wa falsafa bali kama neno la Mungu, kama ilivyoonekana katika jinsi ilivyoathiri mwenendo wao.
1 Ndugu zangu, kwa kuwa ninyi wenyewe mnajua ya kwamba kuja kwetu kwenu hakukuwa bure, 2 kama vile mjuavyo, tulikuwa tumeteswa na kutukanwa huko Filipi, lakini hata hivyo, kwa msaada wa Mungu wetu, tulikuwa na ujasiri wa kuwaambia Injili ya Mungu ingawa kulikuwa na upinzani mkubwa. 3 Kwa maana himizo letu halikutokana na hila wala nia mbaya au udanganyifu. 4 Kinyume chake, tulinena kama watu tuliokubaliwa na Mungu tukakabidhiwa Injili. Sisi hatujaribu kuwapendeza wanadamu bali kumpendeza Mungu, yeye ayachunguzaye mawazo ya ndani sana ya mioyo yetu. 5 Kama mjuavyo, hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli ili kuficha tamaa mbaya: Mungu ndiye shahidi yetu. 6 Wala hatukuwa tunatafuta sifa kutoka kwa wanadamu, wala kutoka kwenu au kwa mtu mwingine awaye yote.
Kama mitume wa Kristo tungaliweza kuwa mzigo kwenu, 7 lakini tulikuwa wapole katikati yenu, kama mama anayewatunza watoto wake wadogo. 8 Tuliwapenda sana kiasi kwamba tulifurahia kushirikiana nanyi, si Injili ya Mungu tu, bali hata maisha yetu, kwa sababu mlikuwa wa thamani mno kwetu. 9 Ndugu zetu, mnakumbuka juhudi yetu na taabu yetu. Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusimlemee mtu yeyote wa kwenu wakati tulipokuwa tunawahubiria Injili ya Mungu.
10 Ninyi wenyewe ni mashahidi na Mungu pia, jinsi tulivyokuwa watakatifu, wenye haki na wasio na lawama miongoni mwenu ninyi mlioamini. 11 Maana mnajua kwamba tuliwatendea kila mmoja wenu kama vile baba awatendeavyo watoto wake. 12 Tuliwatia moyo, tuliwafariji na kuwahimiza kuishi maisha yampendezayo Mungu, anayewaita katika Ufalme na utukufu wake.
13 Nasi pia tunamshukuru Mungu bila kukoma kwa sababu mlipolipokea neno la Mungu mlilosikia kutoka kwetu, hamkulipokea kama neno la wanadamu, bali mlilipokea kama lilivyo hasa, neno la Mungu, litendalo kazi ndani yenu ninyi mnaoamini.
Roho ya Kuwatesa Wengine ya Wayahudi
Paulo anaonyesha roho ya Wayahudi ya kuwatesa wengine, inayojaribu nguvu ya injili na imani ya walioongoka. Anaonyesha uadui wao dhidi ya kuhubiriwa kwa injili kwa watu wa Mataifa, uovu wao, na kuangamizwa kwao. Anatangaza upendo wake kwa Wathesalonike na hamu yake ya kuwaona, ambayo imezuiwa tu na ushawishi wa Shetani juu ya mioyo ya wapinzani wake.
14 Kwa maana ninyi ndugu zetu, mlifanyika wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyoko ndani ya Kristo Yesu katika Uyahudi. Mlipata mateso yale yale kutoka kwa watu wenu wenyewe kama vile makanisa hayo yalivyoteswa na Wayahudi, 15 wale waliomuua Bwana Yesu na manabii, nasi wakatufukuza pia. Watu hao walimchukiza Mungu na tena ni adui wa watu wote, 16 wakijitahidi kutuzuia tusizungumze na watu wa Mataifa ili kwamba wapate kuokolewa. Kwa njia hii wanazidi kujilundikia dhambi zao hadi kikomo. Lakini hatimaye ghadhabu ya Mungu imewafikia.
17 Lakini ndugu zetu, tulipotenganishwa nanyi kwa kitambo kidogo (ingawa kutengana huko kulikuwa kwa mwili tu, si kwa moyo), tulizidi kuwa na shauku kubwa kuwaona uso kwa uso. 18 Maana tulitaka kuja kwenu, hasa mimi Paulo, nilitaka kuja tena na tena, lakini Shetani akatuzuia. 19 Kwa maana tumaini letu ni nini, au furaha yetu au taji yetu ya kujisifia mbele za Bwana Yesu Kristo wakati wa kuja kwake? Je, si ni ninyi? 20 Naam, ninyi ndio fahari yetu na furaha yetu.
Paulo Anamtuma Timotheo Kuwaimarisha
Paulo anaeleza wasiwasi wake kwa ajili ya Wathesalonike, na kuwakumbusha kwamba alikuwa amemtuma Timotheo kuimarisha imani yao na kuwafariji katika mateso mengi yanayowapata Wakristo wote, kama walivyokuwa wameonywa hapo awali.
1 Kwa hivyo tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliamua tubaki Athene peke yetu. 2 Tukamtuma Timotheo ambaye ni ndugu yetu na mtumishi mwenzetu wa Mungu katika kuieneza Injili ya Kristo, aje kuwaimarisha na kuwatia moyo katika imani yenu, 3 ili mtu yeyote asifadhaishwe na mateso haya. Mnajua vyema kwamba tumewekewa hayo mateso. 4 Kwa kweli, tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaambia mara kwa mara kwamba tutateswa na imekuwa hivyo kama mjuavyo. 5 Kwa sababu hii nilipokuwa siwezi kuvumilia zaidi, nilimtuma mtu ili nipate habari za imani yenu. Niliogopa kwamba kwa njia fulani yule mjaribu asiwe amewajaribu, nasi tukawa tumejitaabisha bure.
Taarifa ya Timotheo Inamfariji Paulo
Paulo anatangaza kwamba amefarijiwa na taarifa ya Timotheo kuwahusu. Anatamani kupata nafasi nyingine ya kuwaona tena, na anaomba wadumu katika utakatifu hadi kuja kwa Kristo.
6 Lakini sasa Timotheo ndiyo tu amerejea kwetu kutoka kwenu na ameleta habari njema kuhusu imani yenu na upendo wenu. Ametuambia kwamba siku zote mnatukumbuka kwa wema na kwamba mna shauku ya kutuona kama vile sisi tulivyo na shauku ya kuwaona ninyi. 7 Kwa hiyo, ndugu zetu, katika dhiki na mateso yetu yote tumefarijika kwa sababu ya imani yenu. 8 Sasa kwa kuwa hakika tunaishi, kwa kuwa ninyi mmesimama imara katika Bwana. 9 Je, tutawezaje kumshukuru Mungu kiasi cha kutosha kwa ajili yenu, kutokana na furaha tuliyo nayo mbele za Mungu wetu kwa sababu yenu? 10 Usiku na mchana tunaomba kwa bidii ili tupate kuwaona tena na kujaza kile kilichopungua katika imani yenu.
11 Basi Mungu wetu na Baba yetu mwenyewe na Bwana wetu Yesu atengeneze njia ya sisi kuja kwenu. 12 Bwana na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati yenu na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu. 13 Tunamwomba Mungu aimarishe mioyo yenu ili msiwe na lawama katika utakatifu mbele za Mungu wetu aliye Baba yetu wakati wa kuja kwake Bwana Yesu pamoja na watakatifu wote.