Wito wa Utakatifu na Usafi

Paulo anamwonyesha kila mtu wa Mataifa aliyeongoka kwamba lazima awe mtakatifu na safi, na anawaonya waongofu hao waepuke maovu waliyokuwa wamezoea hapo awali, ambayo wapagani bado walikuwa wakiyatenda. Anawahimiza kuwa na upendo wa kindugu na bidii katika kazi zao.

51 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wathesalonike 4:1–12

1 Hatimaye, ndugu, tuliwaomba na kuwasihi katika Bwana Yesu kwamba, kama mlivyojifunza kutoka kwetu jinsi iwapasavyo kuishi ili kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoishi, imewapasa mzidi sana kufanya hivyo. 2 Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

3 Mapenzi ya Mungu ni kwamba ninyi mtakaswe, ili kwamba mjiepushe na zinaa, 4 ili kwamba kila mmoja wenu ajifunze kuutawala mwili wake mwenyewe katika utakatifu na heshima, 5 si kwa tamaa mbaya kama watu wa Mataifa wasiomjua Mungu. 6 Katika jambo hili mtu asimkosee ndugu yake wala kumlaghai. Kwa kuwa Bwana ni mlipiza kisasi katika mambo haya yote, kama vile tulivyokwisha kuwaambia mapema na kuwaonya vikali. 7 Kwa maana Mungu hakutuitia uchafu, bali utakatifu. 8 Kwa hiyo, mtu yeyote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu, bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.

9 Sasa kuhusu upendo wa ndugu hamna haja mtu yeyote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. 10 Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.

11 Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza, 12 ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote.

Paulo Anaeleza Jinsi Wafu Watakavyofufuka

Paulo anawaonya dhidi ya Wayahudi wenye bidii ambao wangewanyang'anya tumaini lao la furaha ya wakati ujao. Wanaambiwa wasijiachilie, kama wapagani walivyofanya, katika huzuni iliyopitiliza kwa ajili ya wafu wao, ambao waliamini hawangefufuka. Kama uthibitisho zaidi wa ukweli mkuu wa ufufuo, Paulo anaeleza jinsi utakavyotokea, kama alivyofundishwa na Kristo mwenyewe.

1 Wathesalonike 4:13–18

13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini. 14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, na kwa hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini ndani yake. 15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia waliolala mauti. 16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza. 17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

Kuweni Tayari kwa Kuja kwa Kristo Ghafla

Paulo anaonyesha umuhimu wa utakatifu kwa kuzingatia kutokea kwa Kristo kwa ghafla na kwa kutisha, na kuangamizwa kwa hakika kwa waovu na wale ambao hawako tayari kwa siku ya kuja kwake. Wale wanaodumu imara katika imani na kuishi kulingana na injili wanafarijiwa kwa uhakikisho kwamba siku hiyo itakuwa siku ya wokovu kwao kupitia Yesu Kristo.

1 Wathesalonike 5:1–11

1 Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia, 2 kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku. 3 Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.

4 Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi. 5 Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku. 6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi. 7 Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku. 8 Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo. 9 Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. 10 Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye. 11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.

Mahimizo ya Mwisho ya Paulo kwa Wathesalonike

Paulo anawahimiza kuwaheshimu ipasavyo walimu wao wa kiroho, pamoja na kutoa mahimizo mengine mbalimbali ya dhati. Anamalizia kwa maombi na salamu.

1 Wathesalonike 5:12–28

12 Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya. 13 Waheshimuni sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi. 14 Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote. 15 Angalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.

16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.

19 Msiuzime moto wa Roho Mtakatifu; 20 msiyadharau maneno ya unabii. 21 Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema. 22 Jiepusheni na uovu wa kila namna.

23 Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Yesu Kristo. 24 Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.

25 Ndugu, tuombeeni. 26 Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu. 27 Nawaagizeni mbele za Bwana mhakikishe kuwa ndugu wote wanasomewa barua hii.

28 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amen.

Paulo Anabaki Korintho, Akiwahubiria watu wa Mataifa

Akiwa amekataliwa na Wayahudi, Paulo anaendelea kukaa Korintho, akiwahubiria watu wa Mataifa.

Matendo 18:6–11

6 Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakungʼuta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu wa Mataifa.”

7 Kisha akaondoka mle kwenye sinagogi, akaenda nyumbani kwa mtu mmoja jina lake Tito Yusto, aliyekuwa mcha Mungu. Nyumba yake ilikuwa karibu na sinagogi. 8 Kiongozi wa hilo sinagogi, aliyeitwa Krispo, akamwamini Bwana, yeye pamoja na watu wote wa nyumbani mwake. Nao Wakorintho wengi waliomsikia Paulo pia wakaamini na kubatizwa.

9 Usiku mmoja Bwana akamwambia Paulo katika maono, “Usiogope, lakini endelea kusema wala usinyamaze, 10 kwa maana mimi niko pamoja nawe, wala hakuna mtu atakayeweza kukushambulia ili kukudhuru, kwa kuwa ninao watu wengi katika mji huu ambao ni watu wangu.” 11 Hivyo Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, akiwafundisha neno la Mungu.