Wagalatia waiacha imani yao ya kwanza

Paulo anawakemea Wagalatia kwa kuziacha kanuni za msingi za imani yao kwa kudhani kwamba mpango mpya haukutosha kuleta wokovu, ingawa ulikuwa umethibitishwa kwao kwa baraka na karama za kiroho ambazo hazikujulikana chini ya Sheria ya Mose.

51 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Wagalatia 3:1–5

1 Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa. 2 Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? 3 Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? 4 Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! 5 Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?

Abrahamu ahesabiwa haki kwa imani

Paulo anathibitisha ukweli wa mafundisho yake kwa mfano wa Abrahamu, ambaye alihesabiwa haki kwa imani yake katika ahadi za Mungu.

Wagalatia 3:6–18

6 Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” 7 Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu. 8 Maandiko yakitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, alitangulia kumtangazia Abrahamu Injili akisema kwamba, “Kwa kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.” 9 Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani.

10 Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.” 11 Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.” 12 Lakini sheria haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” 13 Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.” 14 Alitukomboa ili kwamba baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.

15 Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. 16 Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa wazao,” likimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako,” yaani mtu mmoja, ndiye Kristo. 17 Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka 430 baadaye, haitangui Agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile. 18 Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kwa njia ya ahadi.

Kwa nini Sheria ya Mose ilitolewa

Paulo anatangaza kwamba kusudi la Sheria ya Mose lilikuwa kuwazuia Wayahudi, ambao Kristo angezaliwa kutoka kwao, wasifuate desturi na taratibu za kuabudu sanamu za wapagani, na kuwafundisha kuwa na tumaini na kumngojea Masiya aliyeahidiwa.

Wagalatia 3:19–29

19 Kwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa mpaka atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. 20 Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja.

21 Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria. 22 Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini.

23 Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. 24 Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. 25 Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria.

26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29 Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.

Paulo ahofia watarudi utumwani

Paulo anaongeza mfano mwingine unaoonyesha kusudi la Sheria, na anawakemea waongofu kutoka miongoni mwa Wayahudi na watu wa Mataifa kwa kutaka kujiweka tena utumwani. Anawahofia kwa sababu hiyo.

Wagalatia 4:1–11

1 Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote. 2 Yeye huwa yuko chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini mpaka ufike wakati uliowekwa na baba yake. 3 Vivyo hivyo na sisi, tulipokuwa bado watoto wadogo, tulikuwa utumwani chini ya taratibu za kawaida za ulimwengu. 4 Lakini ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe, ambaye alizaliwa na mwanamke, akazaliwa chini ya sheria, 5 kusudi awakomboe wale waliokuwa chini ya sheria, ili tupate kupokea zile haki kamili za kufanywa watoto wa Mungu. 6 Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba, Baba.” 7 Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mtoto, kwa kuwa wewe ni mtoto, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kwa kupitia Kristo.

8 Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu. 9 Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa? 10 Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka! 11 Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure.

Paulo awasihi kwa kuwakumbusha bidii yao ya zamani

Paulo anawasihi Wayahudi kwa kuwakumbusha bidii yao ya zamani na upendo wao kwake.

Wagalatia 4:12–20

12 Ndugu zangu, nawasihi mwe kama mimi, kwa sababu mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea jambo lolote baya. 13 Ninyi mwajua kwamba ni kwa ajili ya udhaifu wangu niliwahubiria Injili. 14 Ingawa hali yangu iliwatia majaribuni, hamkunidharau wala kunidhihaki, bali mlinikaribisha kama malaika wa Mungu, kama vile Kristo Yesu. 15 Ile hali ya furaha mliyokuwa nayo imekwenda wapi? Naweza kushuhudia kwamba, kama ingewezekana mngengʼoa macho yenu na kunipa mimi. 16 Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa kuwaambia kweli?

17 Hao wana shauku ya kuwapata lakini si kwa kusudi zuri. Wanachotaka ni kuwatenga mbali nasi, ili ninyi mpate kuwaonea wao shauku. 18 Ni vizuri wakati wote kuwa na shauku kwa ajili ya kusudi zuri, si wakati nikiwa pamoja nanyi tu. 19 Watoto wangu wapendwa, ambao kwa mara nyingine ninawaonea utungu, ninatamani kwamba Kristo aumbike ndani yenu. 20 Natamani kama ningekuwa pamoja nanyi sasa, pengine ningebadilisha sauti yangu. Kwa maana nina wasiwasi kwa ajili yenu.