Kutoka Filipi hadi Thesalonike
Kutoka Filipi kupitia Amfipoli na Apolonia hadi Thesalonike, ambako wanapingwa na Yasoni.
50 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi. 2 Kama desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko, 3 akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristo ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.” 4 Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri.
5 Lakini Wayahudi ambao hawakuwa wameamini wakawa na wivu, wakawakodi watu waovu kutoka sokoni, wakakutanisha umati wa watu, wakaanzisha ghasia mjini. Wakaenda mbio nyumbani kwa Yasoni wakiwatafuta Paulo na Sila ili kuwaleta nje penye ule umati wa watu. 6 Lakini walipowakosa wakamburuta Yasoni na ndugu wengine mbele ya maafisa wa mji, wakipiga kelele: “Watu hawa ni wale walioupindua ulimwengu wamekuja huku, 7 naye Yasoni amewakaribisha nyumbani mwake. Hawa wote wanaasi amri za Kaisari wakisema yuko mfalme mwingine aitwaye Yesu.” 8 Waliposikia haya, ule umati wa watu na maafisa wa mji wakaongeza ghasia. 9 Nao baada ya kuchukua dhamana kwa ajili ya Yasoni na wenzake wakawaacha waende zao.
Paulo awaandikia Wagalatia 51 BK
Paulo anawaandikia Wagalatia barua yake ili kuthibitisha, dhidi ya walimu wanaosisitiza kufuata desturi za Kiyahudi, kwamba imani katika Kristo, wala si utii wao usio mkamilifu kwa sheria ya taratibu za ibada, ndiyo iliyokuwa sababu ya wokovu wao.
Paulo awasalimu Wagalatia
Paulo anatetea utume wake na kuwasalimu ndugu.
1 Paulo mtume: si mtume wa wanadamu wala aliyetumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo na Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu; 2 na ndugu wote walio pamoja nami:
Kwa makanisa ya Galatia:
3 Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo, 4 aliyejitoa kwa ajili ya dhambi zetu ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu wa sasa ulio mbaya, sawasawa na mapenzi yake yeye aliye Mungu na Baba yetu. 5 Utukufu una yeye milele na milele. Amen.
Wagalatia wakemewa kwa kuiacha injili yake
Paulo anawakemea Wagalatia kwa kuiacha injili yake.
6 Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata Injili nyingine, 7 ambayo kwa kweli si Injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. 8 Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri Injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele! 9 Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu yeyote atawahubiria Injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!
10 Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Kristo.
Utume wa Paulo Ulitoka kwa Mungu
Akiwajibu walimu wa uongo, Paulo anasisitiza kwamba alipokea utume wake kutoka kwa Mungu, na anaeleza kuhusu kuongoka kwake, kupewa kwake utume, na mwenendo wa maisha yake kwa ujumla.
11 Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu. 12 Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo.
13 Ninyi mmekwisha kusikia juu ya maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kwa nguvu na kujaribu kuliangamiza. 14 Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika yangu maana nilijitahidi sana katika desturi za baba zangu. 15 Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake, 16 alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu yeyote, 17 wala sikupanda kwenda Yerusalemu kuwaona hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilikwenda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski.
18 Kisha baada ya miaka mitatu nilipanda kwenda Yerusalemu kuonana na Kefa na nilikaa naye siku kumi na tano. 19 Lakini sikumwona mtume mwingine yeyote isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. 20 Nawahakikishia mbele za Mungu kuwa ninayowaandikia si uongo. 21 Baadaye nilikwenda sehemu za Syria na Kilikia. 22 Lakini mimi binafsi sikujulikana kwa makanisa ya huko Uyahudi yaliyo katika Kristo. 23 Wao walisikia habari tu kwamba, “Mtu yule ambaye hapo kwanza alikuwa akitutesa sasa anahubiri imani ile ile aliyokuwa akijaribu kuiangamiza.” 24 Nao wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.
2:1 Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito ili awe pamoja nami. 2 Nilikwenda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure. 3 Lakini hata Tito ambaye alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa. 4 Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, wapate kututia utumwani, 5 hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili kwamba ukweli wa Injili ubaki nanyi.
6 Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea chochote. 7 Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi. 8 Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa. 9 Basi, Yakobo, Kefa na Yohana, walioonekana kama nguzo za kanisa, walitupa mkono wa shirika, mimi na Barnaba walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa na wao waende kwa Wayahudi. 10 Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.
Paulo amkemea Petro kwa kusisitiza desturi za Kiyahudi
Paulo anamkemea Petro kwa kusisitiza desturi za Kiyahudi. Anatetea fundisho la kuhesabiwa haki kwa imani. Anatoa hoja kwamba ikiwa Wayahudi walioukubali Ukristo walikuwa wamesadiki kwamba sheria ya taratibu za ibada haiwezi kuleta wokovu, haikuwezekana kutarajia watu wa Mataifa waishike, au sheria hiyo iwe ya lazima kwao.
11 Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi. 12 Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu wa Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara. 13 Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.
14 Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu wa Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?
15 “Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa, 16 bado tunajua ya kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hivyo sisi pia, tumemwamini Kristo Yesu ili tupate kuhesabiwa haki kwa njia ya imani katika Kristo, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.
17 “Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi. Je, ina maana kwamba Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha! 18 Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonyesha kwamba mimi ni mkosaji. 19 Kwa maana mimi kwa njia ya sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. 20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu. 21 Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure!”