Sehemu ya 7: Kutoka

1491 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Kutoka 12:31–36

31 Wakati huo Farao akawaita Mose na Aroni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni kwa watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabudu Bwana kama mlivyoomba. 32 Chukueni makundi yenu ya kondoo na mbuzi pamoja na ngʼombe, kama mlivyosema, nanyi mwende zenu. Nanyi pia mnibariki.”

33 Wamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke kwa haraka na kuacha nchi yao. Kwa kuwa walisema, “La sivyo, tutakufa wote!” 34 Hivyo watu wakachukua donge lao la unga kabla ya kutiwa chachu, wakaweka ndani ya mabakuli ya kukandia, wakayaviringisha katika vitambaa na kuyabeba mabegani mwao. 35 Waisraeli wakafanya kama Mose alivyowaelekeza, nao wakawaomba Wamisri wawapatie vitu vya fedha, dhahabu na nguo. 36 Basi Bwana alikuwa amewafanya Wamisri kuwa wakarimu kwa hawa watu, wakawapatia Waisraeli vile walivyotaka kwao; kwa hiyo wakawateka nyara Wamisri.

Kutoka 12:40–42

40 Waisraeli walikuwa wameishi Misri kwa muda wa miaka 430. 41 Ilikuwa ni siku ya mwisho ya hiyo miaka 430, vikosi vyote vya Bwana vilipokuwa vimeondoka Misri. 42 Kwa sababu Bwana aliutenga usiku ule ili kuwatoa Waisraeli katika nchi ya Misri, katika usiku huu Waisraeli wote wanapaswa kuadhimisha kwa kukesha ili kumheshimu Bwana katika vizazi vijavyo.