Sehemu ya 6: Mapigo Kumi Yanakamilika

Pigo la Tisa: Siku Tatu za Giza

1491 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Kutoka 10:21–27

21 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili giza litande katika nchi ya Misri, giza ambalo watu wanaweza kulipapasa na kulihisi.” 22 Kwa hiyo Mose akaunyoosha mkono wake kuelekea angani, na giza nene likafunika pote katika nchi ya Misri kwa muda wa siku tatu. 23 Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo yao waliyokuwa wanaishi.

24 Ndipo Farao akamwita Mose na kusema, “Nendeni, mkamwabudu Bwana. Hata wanawake na watoto wenu mwaweza kwenda nao pia, lakini kondoo, mbuzi na ngʼombe wenu waacheni.”

25 Lakini Mose akasema, “Huna budi kuturuhusu tuwe na dhabihu na sadaka za kuteketezwa za kutoa mbele za Bwana Mungu wetu. 26 Sisi ni lazima tuondoke na mifugo yetu pia, wala hakuna ukwato utakaoachwa nyuma. Inatupasa kutumia baadhi ya hiyo mifugo katika kumwabudu Bwana Mungu wetu, kwa kuwa mpaka tutakapofika huko hatutakuwa tumefahamu ni nini tutakachotumia katika kumwabudu Bwana.”

27 Lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, hakuwa radhi kuwaachia waondoke.

Pigo la Kumi: Wazaliwa wa Kwanza Wanauawa

Tishio la Kifo cha Wazaliwa wa Kwanza

Kutoka 11:1–8

1 Basi Bwana alikuwa amemwambia Mose, “Nitaleta pigo moja zaidi kwa Farao na katika nchi ya Misri. Baada ya hilo, atawaacha mwondoke hapa na atakapofanya hivyo, atawafukuza mtoke kabisa. 2 Waambie watu wote waume kwa wake wawaombe majirani zao vitu vya fedha na vya dhahabu.” 3 (Bwana akawafanya Wamisri wawe na moyo wa ukarimu kwa Waisraeli, naye Mose mwenyewe akaheshimiwa sana na maafisa wa Farao na watu wote katika nchi ya Misri.)

4 Kwa hiyo Mose akasema, “Hili ndilo Bwana asemalo: ‘Panapo usiku wa manane Mimi nitapita katika nchi yote ya Misri. 5 Kila mwanaume kifungua mimba katika Misri atakufa, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Farao, aketiye penye kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mtumwa wa kike, anayesaga nafaka kwa jiwe, pamoja na kila mzaliwa wa kwanza wa mifugo. 6 Patakuwepo kilio kikubwa katika nchi yote ya Misri, kilio kibaya ambacho hakijakuwepo wala kamwe hakitakuwepo tena. 7 Lakini miongoni mwa Waisraeli hakuna hata mbwa atakayembwekea mwanadamu wala mnyama yeyote.’ Ndipo mtakapojua kuwa Bwana huweka tofauti kati ya Misri na Israeli. 8 Maafisa hawa wako wote watanijia, wakisujudu mbele yangu, wakisema, ‘Ondoka, wewe pamoja na watu wako wote wanaokufuata!’ Baada ya haya nitaondoka.” Kisha Mose, huku akiwa amewaka hasira, akamwacha Farao.

Kutoka 10:28–29

28 Farao akamwambia Mose, “Ondoka mbele yangu! Hakikisha kuwa hutakuja mbele yangu tena! Siku ile utakapouona uso wangu utakufa.”

29 Mose akamjibu, “Iwe kama ulivyosema! Kamwe sitauona uso wako tena.”

Kutoka 11:9–10

9 Bwana alikuwa amemwambia Mose, “Farao atakataa kukusikiliza, ili maajabu yangu yapate kuongezeka katika nchi ya Misri.” 10 Mose na Aroni wakafanya maajabu haya yote mbele ya Farao, lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke katika nchi yake.

Pasaka Inaliwa

Kutoka 12:21–28

21 Ndipo Mose akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka. 22 Chukueni kitawi cha hisopo, kichovyeni kwenye damu iliyopo kwenye sinia na kuipaka baadhi ya hiyo damu kwenye vizingiti na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu yeyote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake mpaka asubuhi. 23 Bwana apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.

24 “Shikeni maagizo haya yawe kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu. 25 Mtakapoingia katika nchi Bwana atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii. 26 Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’ 27 Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa Bwana, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu. 28 Waisraeli wakafanya kama vile Bwana alivyomwagiza Mose na Aroni.

Wazaliwa wa Kwanza Wanauawa

Kutoka 12:29–30

29 Ilipofika usiku wa manane, Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia. 30 Farao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa haikuwepo nyumba ambayo hakufa mtu.