Sehemu ya 8: Kutangatanga Jangwani

Safari ya Kwanza: Kutoka Ramesesi hadi Sukothi

1491 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Hesabu 33:1–5

1 Hivi ndivyo vituo katika safari ya Waisraeli walipotoka Misri kwa vikosi chini ya uongozi wa Mose na Aroni. 2 Kwa agizo la Bwana, Mose aliweka kumbukumbu ya vituo katika safari yao. Hivi ndivyo vituo katika safari yao:

3 Waisraeli walisafiri kutoka Ramesesi katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza, siku iliyofuata Pasaka. Walitembea kwa ujasiri wazi mbele ya Wamisri wote, 4 waliokuwa wakizika wazaliwa wao wa kwanza wote, ambao Bwana alikuwa amewaua katikati yao, kwa kuwa Bwana alikuwa ameleta hukumu juu ya miungu yao.

5 Waisraeli waliondoka Ramesesi na kupiga kambi huko Sukothi.

Kutoka 12:37–39

37 Waisraeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi. Walikuwepo wanaume wapatao 600,000 waendao kwa miguu bila kuhesabu wanawake na watoto. 38 Watu wengine wengi wakafuatana nao, pamoja na makundi makubwa ya mifugo wakiwemo kondoo, mbuzi na ngʼombe. 39 Wakatengeneza maandazi yasiyotiwa chachu kwa ule unga uliokandwa waliokuwa wameutoa Misri, donge hilo la unga halikuwa limetiwa chachu, kwa kuwa walikuwa wameondolewa Misri kwa haraka nao hawakuwa na muda wa kuandaa chakula chao.

Amri ya Kuadhimisha Pasaka Inatolewa Tena

Kutoka 12:43–13:19

43 Bwana akamwambia Mose na Aroni, “Haya ndiyo masharti kwa ajili ya Pasaka:

“Mgeni hataruhusiwa kula Pasaka. 44 Mtumwa yeyote ambaye mmemnunua aweza kuila kama mmemtahiri, 45 lakini kibarua yeyote au msafiri haruhusiwi kula.

46 “Sharti iliwe ndani ya nyumba; msichukue nyama yoyote nje ya nyumba hiyo. Msiuvunje mfupa wowote. 47 Jumuiya yote ya Israeli ni lazima waiadhimishe Pasaka hiyo.

48 “Mgeni aishiye miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka ya Bwana ni lazima wanaume wote waliomo nyumbani mwake wawe wametahiriwa, ndipo aweze kushiriki kama mzawa. Mwanaume yeyote asiyetahiriwa haruhusiwi kuila. 49 Sheria iyo hiyo itamuhusu mzawa na mgeni anayeishi miongoni mwenu.”

50 Waisraeli wote walifanya kama vile Bwana alivyomwagiza Mose na Aroni. 51 Siku ile ile Bwana akawatoa Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.

13:1 Bwana akamwambia Mose, 2 “Niwekeeni wakfu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. Kila mtoto wa kwanza aliye kifungua tumbo miongoni mwa Waisraeli ni mali yangu, akiwa wa mwanadamu au wa mnyama.”

3 Ndipo Mose akawaambia watu, “Ikumbukeni siku hii, siku ambayo mlitoka katika nchi ya Misri, katika nchi ya utumwa, kwa sababu Bwana aliwatoa humo kwa mkono wenye nguvu. Msile chochote kilichotiwa chachu. 4 Leo, katika mwezi wa Abibu, mnatoka. 5 Bwana atakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Wahivi na Wayebusi, nchi aliyowaapia baba zako kukupa, nchi itiririkayo maziwa na asali, utaiadhimisha sikukuu hii katika mwezi huu: 6 Kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu na katika siku ya saba utamfanyia Bwana sikukuu. 7 Kwa muda wa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu, pasionekane kitu chochote kilicho na chachu miongoni mwako, wala chachu yoyote isionekane popote ndani ya mipaka yako. 8 Siku ile utamwambia mwanao, ‘Nafanya hivi kwa sababu ya jambo ambalo Bwana alinitendea nilipotoka katika nchi ya Misri.’ 9 Adhimisho hili, litakuwa kama alama kwenye mkono wako na ukumbusho katika paji lako la uso, kwamba sheria ya Bwana inapaswa iwe kinywani mwako. Kwa kuwa Bwana alikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu. 10 Ni lazima uishike amri hii kwa wakati uliopangwa mwaka baada ya mwaka.

11 “Baada ya Bwana kukuingiza katika nchi ya Wakanaani na kukupa nchi hiyo, kama alivyokuahidi kwa kiapo na kwa baba zako, 12 inakupasa kumtolea Bwana mzaliwa wa kwanza wa kila tumbo. Wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa mifugo yako ni mali ya Bwana. 13 Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo, lakini kama hukumkomboa, utamvunja shingo yake. Kila mzaliwa wa kwanza mwanaume miongoni mwa wana wenu utamkomboa.

14 “Katika siku zijazo, mwanao akikuuliza, ‘Hii ina maana gani?’ Mwambie, ‘Kwa mkono wenye nguvu Bwana alitutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. 15 Farao alipokataa kwa ukaidi kuturuhusu kuondoka, Bwana aliua kila mzaliwa wa kwanza wa Wamisri, mwanadamu na wa mnyama. Hii ndiyo sababu ninatoa dhabihu kwa Bwana mzaliwa wa kwanza wa kiume, wa kila tumbo na kumkomboa kila mzaliwa wa kwanza wa wana wangu.’ 16 Jambo hili litakuwa kama ishara kwenye mkono wako na kama alama kwenye paji la uso wako, kwamba Bwana alikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu.”

17 Farao alipowaachia watu waende, Mungu hakuwaongoza kufuata njia ipitiayo katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa fupi zaidi. Kwa maana Mungu alisema, “Wakikabiliana na vita, wanaweza kubadili mawazo yao na kurudi Misri.” 18 Kwa hiyo Mungu akawaongoza watu kupitia njia ya kuzunguka kupitia jangwani, kuelekea Bahari ya Shamu. Waisraeli walipanda kutoka nchi ya Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita.

19 Mose akachukua mifupa ya Yosefu kwa sababu Yosefu alikuwa amewaapisha wana wa Israeli. Alikuwa amewaambia, “Hakika Mungu atakuja kuwasaidia, nanyi ni lazima mwiichukue mifupa yangu mwende nayo kutoka mahali hapa.”