Sehemu ya 8: Utawala wa Yoashi

Ufalme wa Yuda

Miaka ya Mwanzo ya Utawala wa Yoashi

878 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 11:21–12:3

21 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.

12:1 Katika mwaka wa saba wa utawala wa Yehu, Yoashi alianza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka arobaini. Jina la mama yake aliitwa Sibia, kutoka Beer-Sheba. 2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana miaka yote ambayo Yehoyada kuhani alikuwa akimwelekeza. 3 Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.

2 Nyakati 23:16–21

16 Kisha Yehoyada akafanya agano kwamba yeye na watu wote na mfalme watakuwa watu wa Bwana. 17 Kisha watu wote wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu pamoja na sanamu na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu.

18 Kisha Yehoyada akaweka uangalizi wa Hekalu la Bwana mikononi mwa makuhani, waliokuwa Walawi, ambao Mfalme Daudi alikuwa amewagawa ili wahudumu hekaluni kwa ajili ya kutoa sadaka za kuteketezwa za Bwana kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, kwa kushangilia na kuimba kama Daudi alivyokuwa ameagiza. 19 Pia akawaweka mabawabu kwenye malango ya Hekalu la Bwana ili kwamba kwa vyovyote asije akaingia mtu yeyote aliye najisi.

20 Akawachukua majemadari wa mamia, watu waheshimiwa, viongozi wa watu pamoja na watu wote wa nchi na kumteremsha mfalme kutoka Hekalu la Bwana. Wakaingia kwenye jumba la mfalme kupitia Lango la Juu na kumkalisha mfalme kwenye kiti cha enzi, 21 nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga.

2 Nyakati 24:3

3 Yehoyada akamwoza wake wawili, akazaa watoto wa kiume na wa kike.

Hekalu Lakarabatiwa 856 KK

2 Nyakati 24:4–5

4 Baada ya muda, Yoashi akaamua kukarabati Hekalu la Bwana. 5 Akawaita pamoja makuhani na Walawi akawaambia, “Nendeni katika miji ya Yuda mkakusanye fedha wanazopaswa kulipa kila mwaka kutoka kwa Israeli wote, ili kukarabati Hekalu la Mungu wenu. Fanyeni hivyo sasa.” Lakini Walawi hawakufanya upesi.

2 Wafalme 12:4–6

4 Yoashi akawaambia makuhani, “Kusanyeni fedha zote ambazo zitaletwa kama sadaka takatifu kwenye Hekalu la Bwana, yaani fedha zilizokusanywa kama kodi, fedha zilizopokelewa kutokana na nadhiri za watu binafsi, na fedha zilizoletwa kwa hiari hekaluni. 5 Kila kuhani na apokee fedha kutoka kwa mmoja wa watunza hazina, nazo zitumike kukarabati uharibifu wowote unaoonekana katika Hekalu.”

6 Lakini ikawa kufikia mwaka wa ishirini na tatu wa utawala wake Mfalme Yoashi, makuhani walikuwa bado hawajalikarabati Hekalu.

2 Nyakati 24:6

6 Kwa hiyo mfalme akamwita Yehoyada kuhani mkuu na kumwambia, “Kwa nini hukuwaambia Walawi walete kutoka Yuda na Yerusalemu kodi iliyowekwa na Mose mtumishi wa Bwana pamoja na kusanyiko la Israeli kwa ajili ya Hema ya Ushuhuda?”

2 Wafalme 12:7–14

7 Kwa hiyo Mfalme Yoashi akamwita Yehoyada kuhani na makuhani wengine, akawauliza, “Kwa nini hamtengenezi uharibifu uliofanyika hekaluni? Msichukue fedha zaidi kutoka kwa watunza hazina wenu kwa ajili ya matumizi yenu, lakini kuanzia sasa ni lazima fedha yote itumike kwa ajili ya kukarabati Hekalu.” 8 Makuhani wakakubali kuwa hawatakusanya tena fedha kutoka kwa watu na kwamba hawatakarabati Hekalu wenyewe.

9 Yehoyada kuhani akachukua kisanduku na akatoboa tundu kwenye kifuniko chake. Akakiweka kando ya madhabahu upande wa kulia unapoingia hekaluni mwa Bwana. Makuhani waliolinda ingilio wakaweka ndani ya kisanduku fedha zote ambazo zililetwa katika Hekalu la Bwana. 10 Kila mara walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani ya kisanduku, mwandishi wa mfalme na kuhani mkuu walikuja, wakazihesabu fedha hizo zilizoletwa katika Hekalu la Bwana, na kuziweka katika mifuko. 11 Wakiisha kuthibitisha kiasi cha hizo fedha, waliwapa watu walioteuliwa kusimamia kazi katika Hekalu. Kwa fedha hizo, wakawalipa wale watu waliofanya kazi katika Hekalu la Bwana: yaani, maseremala na wajenzi, 12 waashi na wakata mawe. Walinunua mbao na mawe ya kuchongwa kwa ajili ya ukarabati wa Hekalu la Bwana, na kulipia gharama nyingine zote za kulitengeneza.

13 Fedha zilizoletwa kwenye Hekalu hazikutumiwa kutengenezea masinia ya fedha, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, tarumbeta wala vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au fedha kwa ajili ya Hekalu la Bwana; 14 zililipwa kwa wafanyakazi, ambao walizitumia kwa kukarabati Hekalu.

2 Nyakati 24:12–14

12 Mfalme na Yehoyada wakawapa wale watu waliofanya kazi iliyotakiwa katika Hekalu la Bwana. Wakawaajiri waashi na maseremala ili kutengeneza Hekalu la Bwana, pia wafanyakazi za chuma na shaba ili kukarabati Hekalu la Bwana.

13 Watu walioshughulika na kazi walikuwa wenye bidii, nayo kazi ya kukarabati ikaendelea vizuri mikononi mwao. Wakalitengeneza upya Hekalu la Bwana likarudi katika hali yake ya awali na kuliimarisha. 14 Walipokamilisha kazi hiyo ya kukarabati, wakaleta fedha zilizobaki wakampa mfalme na Yehoyada, nao kwa hizo wakatengeneza vyombo kwa ajili ya Hekalu la Bwana: Vyombo kwa ajili ya huduma na kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia mabakuli na vitu vingine vya dhahabu na fedha. Wakati wote Yehoyada alipokuwa hai, sadaka za kuteketezwa zilitolewa wakati wote katika Hekalu la Bwana.

2 Wafalme 12:15–16

15 Wao hawakudai kupewa hesabu ya fedha kutoka kwa wale waliowapa ili kuwalipa wafanyakazi, kwa sababu walifanya kwa uaminifu wote. 16 Fedha zilizopatikana kutokana na sadaka za hatia na sadaka za dhambi hazikuletwa katika Hekalu la Bwana; zilikuwa mali ya makuhani.